Habari, Utamaduni, Historia na Simulizi za Tanzania na Afrika Mashariki

Air France yaanzisha safari za moja kwa moja kati ya Paris na Dar-es-Salaam

Shirika la ndege la Ufaransa yaani Air France limezindua rasmi safari zake za moja kwa moja kati ya Dar Es Salaam (JNIA) na mji mkuu wa Ufaransa, Paris (Charles De Gaulle Airport).

Safari ya kwanza ilifanyika hapo jana tarehe 12 Juni 2023 kwa kutumia ndege aina ya Boeing Dreamliner B787-9 yenye usajili namba F-HRBD.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa aliongoza mapokezi ya ndege ya Airfrance katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Katika mapokezi hayo waziri Mbarawa alisema, maamuzi ya Air France kuanzisha safari katika Kiwanja hiki sio tu yatatoa nafasi kwa abiria kuweza kuchagua na kunufaika na usafiri wa moja kwa moja kutoka Dar es Salaam mpaka Paris, bali pia yataongeza tija na manufaa katika Nyanja za Utalii, biashara, na ajira na hivyo kukuza uchumi kwa nchi zote mbili.

Ujio wa ndege hii utapunguza adha ya usafiri kwa wasafiri ambao, hapo awali ili kwenda Ufaransa (Paris), walilazimika kupitia katika miji mingine kama vile Nairobi, Addis, Doha, Dubai, Amsterdam au Istanbul.

Hii ni kutokana na kutumia mashirika kama Kenya Airways, KLM, Etihad, Qatar, Emirates, Turkish na mengineyo ambayo safari zao zinapita katika miji mikuu yao ili kuunganisha ndege kwani mashirika hayo hayakuwa na safari za moja kwa moja kati ya DAR na Paris.

Pia itaongeza uchumi wa nchi yetu kupitia mapato mbalimbali hususani katika Sekta ya Usafiri wa Anga.

Ndege hiyo itakuwa ikifanya safari zake mara tatu kwa wiki ikipitia Zanzibar na kisha kuendelea na safari mpaka Dar Es Salaam.

Ndege itaondoka uwanja wa ndege wa Paris Charles de Gaulle (CDG) saa nne na dakika ishirini asubuhi siku za Jumatatu, Jumatano na Jumamosi kama safari namba AF876.

Itatua Zanzibar saa mbili na robo usiku na kukaa hapo kwa saa moja na nusu, kisha itaondoka saa tatu na dk 45 usiku kuelekea DAR na kutua saa nne na dk 20 za usiku siku hiyohiyo.

Safari ya kurudi Paris itaanzia Dar Es Salaam (JNIA) majira ya saa tano na dk 45 usiku huohuo na kuwasili Paris (CDG) saa moja na dk 55 asubuhi siku inayofuata.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari