Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Arusha kufuta magari madogo ya abiria kutoka kwenye sekta ya usafirishaji Jijini

Mamlaka ya udhibiti wa usafiri nchi kavu yaani LATRA, imeagiza wamiliki wa magari ya abiria mkoani Arusha kubadilisha magari madogo yanatotumika sasa na kuingiza mabasi ya saizi ya kati kwa ajili ya safari za katikati ya jijini.

Hivi sasa magari yanayotumika ni Vans au magari madogo aina ya Toyota Hiace, Nissan Caravan na Isuzu Fargo (Como).

Mamlaka inataka mabasi ya saizi ya kati Mini-bus ndio yaanze kutumuka kwa safari hizo jijini Arusha.

Wakati huo huo LATRA imegomea maombi ya wafanyabiashara wapya wa daladala kuongezwa kwenye idadi ya watoa huduma ya usafiri wa vyombo hivyo ndani ya jiji la Arusha.

LATRA imegomea ombi hilo mbele ya naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi, Atupele Mwakibete aliyekuwa kwenye ziara jijini Arusha hivi karibuni, kusikiliza kero za wasafirishaji, abiria na wananchi kwa ujumla.

Mmoja wa wafanyabiashara wa magari madogo ya abiria maarufu kama vifodi au daladala Jijini Arusha, Alex Kimaro analalamika kuwa mamlaka husika imezifungia baadhi ya njia zenye wateja wengi wanaohitaji wa huduma za usafiri huku wao wakikwama kiuchumi kwa kuwakosa abiria hao.

” Mimi natokea umoja wa SACCOS ya Friends Corner, tunaomba Waziri utusaidie kutuombea kwa mamlaka husika watufungulie baadhi ya ruti na kuongeza zingine hasa kutoka muorombo kwenda Chekereni.”

Wafanyabiashara hao pia wanataka barabara ya Muriet ifunguliwe kwa vibali vya usafirushaji kwani wamechukua mkopo wa zaidi milioni 100, kununua magari hivyo wanashindwa kufanya marejesho.

“Sisi tumechukua mikopo na tumenunua magari lakini tunanyimwa leseni za njia husika kutoka LATRA.”

Akitakiwa kujibu swala hilo, ofisa mfawidhi wa Latra mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela alisema kuwa wamefunga ruti hizo kutokana na idadi ya daladala kwenye maeneo hayo kujitosheleza.

Mwakalebela anawataka watoa huduma hizo kuhamia barabara za pembezoni mwa mji ikiwemo barabara ya Afrika mashariki kuelekea nadosoito, Mkonoo na Oljoro.

“Barabara nilizozitaja bado zina nafasi kwa sasa lakini zinaombwa sana, na mkichelewa mtakuta zimejaa huku mnapoomba mko zaidi ya 200 sasa wewe uliyesimama tukikupa upendeleo utasababisha wale wengine waliotanguliza maombi nao waje na hatuna nafasi hiyo kutokana na zilizopo tu zenyewe zinasababisha msongamano mkubwa sana hasa asubuhi na jioni!”

Amani Mwakalebela

Zaidi ya hayo, Mwakalebela pia aliwataka wafanyabiashara kusitisha kununua daladala ndani ya jiji la Arusha kwani zimejaa na wanaelekea kuzipiga marufuku vyombo hivyo kutoa huduma za usafirishaji ndani ya jiji la Arusha badala yake wanazipa kipaumbele mabasi ya saizi ya kati yaani Toyota Coaster, Isuzu Journey au Nissan Civilian.

“Arusha Kwa sasa ni jiji na lazima tuipe heshima yake kama jiji ambapo ndani ya miaka hii mitatu tutasitisha daladala kutoa huduma badala yake wapishe magari makubwa yanayochukua idadi kubwa ya watu Ili kupunguza msongamano usio na ulazima”

Alisema kuwa katika mabadiliko hayo yatasaidia pia kupunguza ajali za mara kwa mara kutokana na kutoa masharti ya wamiliki wote lazima wafunge vizibiti mwendo kwenye magari yao lakini pia kutoa tiketi za kimtandao hasa zile zinazokwenda masafa marefu.

Kwa Upande wake Waziri Mwakibete akikubaliana na hoja hiyo ya Latra, aliwataka wafanyabiashara hao kufuata sheria na kanuni hizo ili kuleta tija ya huduma hiyo nchini.

“Sasa changamkieni fursa zilizopo sio kung’ang’ania zilizokwisha katazwa ikiwemo hiyo ruti mpya ya Barabara ya Afrika mashariki lakini pia ukiona huwezi uza daladala nunua basi kubwa usajiliwe haraka kabla hizo nafasi hazijajaa kwa sababu lengo la serikali ni kusaidia wananchi wake basi na nyie wasaidieni wale wa nje ya mji kupata huduma” alisema Mwakibete