Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mimea Vamizi Na athari zake dhidi ya Binadamu, Wanyama na Mazingira katika uwanda wa Burunge

Mimea migeni na vamizi inayochipuka kwa wingi katika maeneo ya hifadhi ya wanyamapori ya Burunge, imeshamiri kwa kasi na inadaiwa kuwa hatua za haraka zisipochukuliwa itasababisha hifadhi hiyo kuathirika vibaya.

Kwa mujibu wa Katibu wa Jumuiya hiyo ya Jamii ya Burunge, Benson Mwaise, mimea vamizi inayoota katika sehemu za hifadhi huathiri maeneo ya malisho hivyo kulazimisha wanyama kuhama kutoka sehemu iliyotingwa na majani hayo mageni na kwenda kutafuta maeneo mengine ya malisho.

Burunge ni hifadhi ya kijamii inayoundwa na vijiji kumi, vikiwemo Magara, Mwada, Sangaiwe, Ngolley, Vilima Vitatu, Kakoi, Minjingu, Olasiti, Maweni na Manyara.

Vijiji hivyo kumi vyote vimo ndani ya kata tatu za Mwada, Magara na Nkaiti, wilayani Babati.

Burunge kwa Sasa inakabiliwa na aina tano za mimea hiyo, ambayo ni Mundu wa Marekani (Senna obtusifolia), Mnili (Indigofera spp ), Mbaruti (Agemona Mexicana) , Datura (Datura stramonium) na Calotrops procera, amesema Mwaise.

Ameongeza kuwa, athari zilizopo ni wanyama kukosa maeneo ya malisho na makazi jambo linalowafanya wanyama kutoka nje ya hifadhi, na kwenda katika maeneo ya nje na kuharibu shughuli mbalimbali za binadamu.

“Ushoroba uko hatarini kupoteza wanyama na baadhi ya mimea ya asili kama hatua za haraka za kukabiliana na mimea hii hazitochukuliwa, kwani baadhi ya mimea hii huchukua nafasi kubwa katika kustawi kwake na kusababisha mimea mingine kutostawi vizuri na kufa, amesema Mwaise.

Mimea vamizi pia imeathiri kwa kiasi kikubwa eneo la Malisho katika hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) ambako awali, kamishna msaidizin wa uhifadhi, Yustina Kiwango alibainisha kuwa Zaidi ya asilimia 17 ya hifadhi hiyo imefunikwa na magugu hayo.

“Mimea vamizi, yakiwemo ‘matufaa ya sodoma,’ marufu kama Ndulele, imeoteana ndani ya eneo lenye ukubwa wa Kilometa za Mraba 55,” alisema Kiwango na kuongeza kuwa Hifadhi ya Taifa ya Arusha (National Park), ina ukubwa wa Kilometa za Mraba 332.

Pamoja na kufunika kabisa maeneo ya malisho ya wanyamapori, mimea vamizi pia imetengeneza vichaka vya miiba ambavyo vimekuwa vikifunga maeneo ya mapito ya wanyama na kusababisha baadhi ya viumbe hao kuhamia nje ya hifadhi na hata kwenye makazi ya watu.

Sehemu nyingine iliyoathirika na mimea vamizi ni eneo la hifadhi jumuishi ya Ngorongoro (NCA) ambako pia magugu mengine mageni yaliyopewa jina la Makutiani yamechipuka katika sehemu mbalimbali ikiwemo ndani ya bonde maarufu yaani Kreta.

“Hivi sasa tunashirikiana na watafiti kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, ili kubaini upana wa tatizo pamoja na ukubwa wa maeneo yaliyoathirika,” alisema Mwaise na kuongeza kuwa hiyo ni pamoja na kutafuta njia sahihi za kukabiliana na mimea hiyo vamizi katika hifadhi.

Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (WMA), iliyoanzishwa kupitia muungano wa vijiji kumi, impo katikati ya mapito au ushoroba wa wanyamapori ujulikanao kama Kwakuchinja.

Ushoroba Kwakuchinja (Corridor) ni mapito ya asili ya wanyamapori yanayounganisha hifadhi mbili za taifa za Tarangire na Ziwa Manyara, pamoja na shamba kuu la Manyara Ranch, zote hizo zikiwa katika mikoa ya Arusha na Manyara.

Ushoroba wa Kwakuchinja una ukubwa wa Kilometa za Mraba 6,000, na pia umepakana na maziwa mawili ya Burunge na Manyara.

Hivi karibuni waandishi wa habari walitembelea eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mafunzo maalum ya mazingira na hifadhi ya Bioanuwai yanayoendeshwa na Taasisi ya Nukta Afrika, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), kupitia mradi wake wa ‘USAID Tuhifadhi Maliasili!’ na kubaini uwepo wa changamoto lukuki katika ushoroba huo ikiwemo mimea hiyo vamizi.

Hifadhi ya Burunge (WMA) ambayo imo ndani ya ushoroba wa Kwakuchinja, yenyewe ina ukubwa wa kilometa za mraba 283 na imepakana na eneo la Mswakini Chini.

Na wataalamu wanakiri kuwa eneo hilo muhimu kwa hifadhi ya mazingira, mapito ya wanyama pamoja na shughuli za kitalii, limeathirika sana na uoto wa mimea migeni vamizi inayotishia afya za wanyamapori pamoja na wale wa kufuga.

Hivi karibuni Wizara ya Maliasili na Utalii ilibainisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa hadi sasa kuna aina 47 za mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula alisema sababu zinazopelekea kushamiri kwa mimea vamizi ni pamoja na uingizaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa, shughuli za binadamu na kuhama kwa viumbepori kutoka sehemu moja kwenda nyingine.