Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Chui na Duma sasa kufanyiwa Sensa Maalum kutambua idadi yao Tanzania

Tanzania kupitia taasisi ya utafiti wa wanyama pori Tanzania (TAWIRI) imeanza kufanya sensa maalum kwa wanyama aina ya Duma na Chui ambao wametajwa wako katika hatari ya kutoweka.

Lengo la kufanya hivyo ni kwa ajili ya kuwahifadhi lakini pia kutunza bionuai zao kwa ajili ya kuongezeka.

Hayo yamejiri baada ya Taasisi ya Kimataifa inayohusika na Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) kutoa orodha ya aina 87 za wanyama walio hatarini kutoweka duniani.

Miongoni mwa wanyama hatarini kutoweka zaidi ni pamoja na Mbwa mwitu, Duma, Chui, Sokwe mtu, Kifaru, na inzi wa maua.

Akizungumza na waandishi wa habari,  mkurugenzi wa utafiti katika taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) Dk. Julius Keyyu alisema wamenza na kuwahesabu kujua idadi yao nchini Tanzania itakayosaidia  kuhifadhi bionuai zao.

“Wanyama hawa ingawa wako hatarini kutoweka duniani lakini Tanzania bado wapo na hii imetokana na kugundua mapema hali hiyo na kuanza kuwahifadhi kupitia mpango mkakati, na sasa tumeamua kuhifadhi bionuwai zao”

Alisema walianza kuwawekea mpango mkakati wa kuwanusu wanyama hao kuanzia mwaka 1993 ambapo kwa sasa mafanikio yameonekana kutoka Mbwa mwitu chini ya 50 na sasa wako zaidi ya 184 hasa hifadhi ya Serengeti.

Kwa upande wa Sokwe mtu alisema walikuwa wachache sana bila kutaja idadi ambapo kwa sasa wako zaidi 2600, huku Duma na Chui wakiongezeka kwa kasi.

“Duma na Chui kujua idadi yao inahitaji mbinu tofauti kuwapata lakini wapo wengi wanaotosha kwa watumizi ya utalii na mazingira na uzuri TAWIRI tumeanza kuwafanyia utafiti wa sensa yao katika hifadhi ya Mwalim Nyerere na Ruaha” alisema mtafiti huyo.

Alisema kuwa kwa upande Chui tuliwekeza nguvu ya ziada ya kuhifadhi maeneo yake ambapo kwa duniani asilimia 10 ya maeneo yanayofaa kwa mnyama huyo yako Tanzania, na  walifanya hivyo baada ya kuona zaidi ya asilimia 75 ya watalii wanaokuja nchini wanataka kumuona.

Akizungumzia sababu za wanyama hao kutoweka, mkurugenzi wa TAWIRI, Dk. Ernest Mjingo alisema ni kutokana na maeneo yao ya asili waliyokuwa wanaishi kutoweka kwa kuvamiwa na shughuli za binadam kwa makazi, kilimo au ufugaji.

Alisema sababu nyingine inayowapoteza ni migongano ya wanyama hao na binadamu kwa ujangili au kufa kwa magonjwa kutokana na mfumo wa ikolojia.

“Sababu kuu nyingine ni kuziba kwa shoroba zao hasa wanapohama kwenda mahali mbali kutafuta mahitaji yao, wanashindwa kurudi kutokana na njia zao kukuta zimezibwa na shughuli za binadamu” alisema mkurugenzi huyo.

Alisema kutokana na hatari hiyo kutikisa dunia, wanatarajia mwaka 2024 kuanza mchakato wa kuhuisha mipango mikakati wa kuhifadhi wanyama hao, ambao nyingi zimekwisha mda wake ili kuwaokoa na wazidi kuongeza Tanzania.

Sababu ndogo ndogo ni mabadiliko ya Tabia ya nchi ambayo huibua mimea vamizi ambayo haina manufaa kwa wanyama ikiwemo Ile ambayo haihitajiki kwa chakula wala hifadhi.

Akizungumzia hali hiyo, mkurugenzi wa taasisi ya wanawake na utalii, Mercy Michael alisema kuwa inahitajika jitihada za makusudi kuokoa wanyama hao nchini wasipotee kutokana na kuwa tegemezi kwa sekta yao.

“Watalii zaidi ya asilimia 90 wanaokuja nchini wanataka kuona wanyama na Chui ni mmoja wanyama pendwa hivyo tuko tiyari kuunga mkono jitihada zozote za kunusuru kizazi chao ili wasipotee nchini”

Aidha kutokana na hayo, Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bioanuwai (COP 15), uliofanyika Desemba mwaka jana nchini Canada, walifikia makubaliano ya kulinda thuluthi moja ya ardhi na maji ya dunia hii hadi mwisho wa muongo huo.

Mkutano huo uliozikutanisha serikali kutoka duniani kote na wadau wengine muhimu ulilenga kuafikiana malengo mapya yatakayoiongoza dunia katika hatua za kubadili mwelekeo na kusitisha upotevu wa bionuai ambayo ni tegemeo la viumbe na mazingira ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa bionuai (CBD) upotevu huo wa bionuai unaongezeka kwa kasi ambayo inatishia mustakabali wa dunia na matendo ya wanadamu ndio chachu ya upotevu huo.