Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Fundi Ujenzi Afariki baada ya kuangukia Panga Lake Mwenyewe wakati akikwepa Mti aliokuwa anaukata

Serengeti, Mara

Fundi ujenzi Bahati Mkirya aliyekuwa na umri wa miaka 28, mkazi wa Kijiji cha Rung’abure wilayani Serengeti anadaiwa kupoteza maisha baada ya kuangukia panga lake mwenyewe ambalo lilimtoboa kifuani.

Taarifa kutoka wilayani Serengeti, Mkoani Mara, zinaeleza kuwa Marehemu Mkirya alichomwa na panga hilo kifuani baada ya kuliangukia wakati akijaribu kukwepa kuangukiwa na mti mkubwa wa mwembe aliokuwa anaukata.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Rung’abure  Joseph Meng’anyi amethibitisha tukio hilo ambalo kwa mujibu wa kiongozi huyo, lilitokea siku ya Ijumaa ya Tarehe 6 Januari 2023 majira ya saa 6 mchana.

Ajali hiyo ya kusikitisha ilitokea  katika Kitongoji cha Kwanina, na kwamba mtoto wa marehemu ndiye aliyetoa taarifa ya kifo cha Bahati Mkirya.

Taarifa za awali ni kwamba Fundi Ujenzi huyo alikuwa ameangukia panga alilokuwa nalo wakati anakwepa kuangukiwa na mti aina ya mwembe aliokuwa akiukata.

“Sisi kwanza tulisikia yowe basi tukakimbilia eneo la tukio ili kujua kulikoni,” alisema kijana huyo.

“Basi tulipofika ndipo tukamkuta Mkirya amelala chini huku akiwa na jeraha kubwa kifuani pake.”

Inadaiwa kuwa hadi watu wanawasili eneo latuki, Fundi huyo alikuwa tayari amekata roho.

Walikuta amelowa damu huku panga alilokuwa analitumia kukata miti, likiwa pembeni mwa mwili wake.

Vile vile, ule mti wa mwembe uliokuwa jirani na nyumba ya mama yake na ambao hasa alikuwa akiukata nao ulikuwa umeangukia karibu na mwili wa marehemu.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto wake wa kiume, ambaye ana umri wa miaka sita aliyeshuhudia tukio zima anasema kuwa baba yake alianguka chini wakati anakimbia ili asiangukiwe na mti aliokuwa anaukata.

Baada ya kuanguka, inadaiwa kuwa Mkirya alionekana akijitahidi kuamka tena lakini ghafla akaishiwa nguvu na kuanguka kwa mara ya pili.

Basi, mtoto kuona hivyo akakimbia kwenda kumuita bibi yake, yaani Mama wa Marehemu.

“Mama huyo alipofika eneo la tukio alimkuta mwanaye amekwisha kupoteza maisha ndipo akaanza kupiga yowe kuomba msaada,” alifafanua Mwenyekiti.

“Kwa kweli fundi alikuwa na jeraha kubwa kifuani, na inaonekana kuwa wakati anajaribu kukwepa huo mti usimwangukie aliliangukia panga lake mwenyewe ambalo lilimjeruhi vibaya kifuani.”

Kifo chake kinaelezewa kusababishwa na damu iliyovuja kwa wingi ndani na nje ya mwili wa fundi huyo.

Meng’anyi ameiambia Serengeti Media kuwa ameishajulisha Polisi ili wafike eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo,kwa mjibu wa Polisi wilayani hapa wamekiri kupata taarifa na wameenda eneo la tukio.