Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Kilimo cha Michikichi: Tanzania sasa Kuzalisha Miche Laki Tatu kwa Mwaka

Wakala wa Mbegu za Kilimo Tanzania (ASA) imejipanga kuongeza uzalishaji wa miche ya zao la michikichi hadi kufikia zaidi ya miche 300,000 kwa mwaka ili kusaidia kupunguza wimbi la uingizaji wa mafuta ya kula nchini.

Hatua hiyo, kwa kiasi fulani inatokana na maagizo ya Waziri wa Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu hitaji la kuboreshwa kwa uzalishaji wa miche hiyo muhimu kama ajiili ya kuwawezesha wakulima wengi zaidi kushiriki katika uzalishaji mkubwa wa zao hilo ghafi la kuzalisha mafuta ya kula.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Tanzania inatumia zaidi ya Shilingi bilioni 470 kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi kila mwaka wakati nchi ina uwezo wa kulima mazao mbalimbali ya kuzalisha mafuta ya kula, ikiwa ni pamoja na zao la michikichi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini (ASA) Dk.Sophia Kashenge akitoa maelezo kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya kuhusu maendeleo ya kazi za upanuzi wa Shamba la Mbegu la Mbozi. Picha: Valentine Oforo
 

Mkurugenzi Mtendaji wa ASA, Dokta Sophia Kashenge amesema kwa sasa Wakala unafanya kazi ya kuimarisha vitalu vya uzalishaji wa miche ya michikichi kwenye mashamba yake makuu matatu.

Hadi sasa, Dkt Kashenge amesema kuwa ASA imeanzisha vitalu vya kuzalisha miche ya michikichi katika mashamba yake ya Bugaga (Kigoma), shamba la Mwele (Tanga) na shamba la Msimba lililopo mkoani Morogoro.

“Mashamba makubwa matatu yanajumuisha vitalu muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa miche ya michikichi na kwa sasa tunafanya kazi ya kuweka skimu za kisasa za umwagiliaji na nyumba za kijani (green houses) katika maeneo hayo ili kuhakikisha tunaongeza uzalishaji,” alisema.

Sambamba na hilo, Dk.Kashenge aliongeza kuwa Wakala wa mbegu utaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi ili kuongeza wigo katika zalishaji wa miche hiyo.

“Sisi ASA tunaishukuru sana serikali kwa kuendelea kutuamini katika jukumu hili kubwa na muhimu la kuzalisha na kusambaza mbegu, na tutaendelea kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wakulima kote nchini wanapata mbegu za kutosha za mazao mbalimbali, ikiwemo zao la michikichi,” alihakikishia.

Jumapili iliyopita katika kikao chake na wadau mbalimbali wa zao la michikichi kilichofanyika mkoani Kigoma, pamoja na mambo mengine, Waziri Majaliwa aliagiza taasisi za uzalishaji wa mbegu, ikiwemo ASA, kuongeza kasi na kiwango cha uzalishaji wa miche ya michikichi ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia hapa nchini.

Pamoja na hayo, waziri Majaliwa aliwaagiza wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kuangalia uwezekano wa kuzalisha zao hilo la mchikichi katika maeneo yao, iwapo hali ya hewa na asili ya udongo inaruhusu.

 “Viongozi wote wa mikoa, wilaya na vyama vya siasa wana majukwaa ya kukutana na wananchi wakati wote. Twendeni tukawatie moyo kulima michikichi kwa sababu ni zao ambalo litawapatia fedha kwa muda mrefu,” Majaliwa.

Kikao hicho, kilikuwa na lengo la kujadili changamoto zinazowakabili wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha zao la michikichi, na njia za kuhakikisha nchi inakuwa na kiasi cha kutosha cha michikichi, maendeleo ambayo waziri Majaliwa alieleza yatalisaidia taifa kupuguza kuagiza kiasi kikubwa cha michikichi kutoka nje ya nchi.

Kulingana na Waziri Mkuu, kwa sasa mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanafikia zaidi ya tani 650,000 kila mwaka wakati uzalishaji unakadiriwa kuwa tani 290,000 pekee.

“Kiasi cha tani 360,000 sawa na asilimia 55.4 huagizwa kutoka nje ya nchi na kuigharimu serikali takriban shilingi bilioni 470 kila mwaka. Tunahitaji pesa hizo kutumika kwa maendeleo ya nchi,” alifafanua.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alieleza kuwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na makampuni mengine binafsi wamekuja na uzalishaji wa mbegu bora za michikichi iitwayo TENERA, aina nzuri yenye uwezo wa kuzalisha mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo hutumiwa na takriban asilimia 90 ya wakulima.

“Hadi kufikia Januari, 2023, TARI kwa kushirikiana na kampuni binafsi imezalisha jumla ya mbegu milioni 14.14, ambapo kati ya takwimu hizo mbegu milioni 11.59 zimezalishwa na TARI pekee na mbegu milioni 2.54 na makampuni binafsi yakiwemo FELISA, NDF na Yangu Macho Group Ltd,” alifahamisha.

Aidha, alibainisha kuwa kati ya mbegu milioni 14.14 zilizozalishwa, mbegu milioni 9.60 zimesambazwa kwa taasisi mbalimbali zikiwemo JKT na Magereza na halmashauri zote nane za Mkoa wa Kigoma.