Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Madiwani Karatu Waja Juu wilaya kushika Mkia katika mitihani ya Taifa Arusha

Wilaya ya Karatu ambayo imekuwa ikishika nafasi ya saba kimkoa katika mitihani ya kitaifa imegundua ghafla kuwa hiyo namba saba hasa ndio ya mwisho mkoani.

Mkoa wa Arusha una wilaya saba, zikiwemo Meru, Arusha Mjini, Arusha Vijijini (DC), Longido, Monduli, Karatu na Ngorongoro.

Sasa madiwani wanabainisha kuwa mara nyingi wakisikia kuwa Karatu imeshika nafasi ya saba, watu hudhani wilaya iko juu kwenye kumi bora, kumbe katika mkoa wenye wilaya saba, nafasi ya saba hasa ndio ya mwisho kabisa.

Wakati huo huo wenyeviti wa vitongoji wilayani Karatu mkoani Arusha wametakiwa kushirikiana na watendaji wa vijiji kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga sekondari wanaripoti mashuleni mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na afisa mtendaji mamlaka ya mji mdogo wa Karatu Jacob Gadiye wakati akizungumza na wenyeviti hao katika kikao Cha Baraza la mamlaka hiyo.

Aliwataka wenyeviti hao kupita katika shule zao za msingi na secondary  wakishirikiana na watendaji kuangalia wanafunzi ambao hawajaripoti na kuwachukulia hatua wazazi ambao wamekaidi kuwapeleka watoto shule.

Sambamba na Hilo pia aliwataka kuwahamasisha wazazi kuchangia chakula Cha wanafunzi ili kuondokana na alama wanayopata kiwilaya ya namba Saba Kila mwaka katika mitihani ya kidato Cha nne na darasa la Saba.

“Tunaomba tushirikiane katika kuongeza ufaulu katika wilaya kwani Kila matokeo yakitoka ya darasa la Saba au kidato Cha nne tunasikia wilaya Ni ya Saba kumbe namba hiyo ndo ya mwisho ” alisema Gadiye.

Kwa upande wake makamu  mwenyekiti wa halmashauri John Bayyo aliwaomba wenyeviti hao kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ikiwemo kuvunja vijiwe vyote vinavyodaiwa kukusanya vibaka .

“Kuna maeneo ya vijiwe vya chezo wa ‘Pool Table,’ Drafti’ na michezo mingine. Sasa vijana wetu wanashinda kutwa katika hivyo vijiwe,” alibainisha Bayo.

Bayo anasema kuwa vijana hupoteza muda kwenye vijiwe vya michezo hiyo kuanzia asubuhi hadi jioni.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri ameongeza kuwa kuna uwezekano wa vijiwe hivyo kuzalisha wahalifu au kutima kupanga mipango ya uhalifu mjini Karatu.