Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mafuriko ya Mto Wami yaleta Kizaazaa Kilosa, Morogoro

Huku janga la maporomoko ya miamba kutoka Mlima Hanang’ likiendelea kuwaumiza wakazi wa Katesh na vijiji jirani, ambako mpaka sasa idadi ya vifo ikikaribia 70, Mafuriko Mengine Makubwa yametokea Mkoani Morogoro.

Taarifa kutoka Wilayani Kilosa zinasema kuwa Mvua kubwa iliyoshuka usiku wa kuamkia tarehe 5 Desemba, imesababisha mto Wami kujaa pomoni na kutapika na mafuriko hayo kuathiri maeneo ya Rudewa ambako nyumba na mashamba yamefunikwa kwa maji.

Hata hivyo habari zaidi kutoka Kilosa zinadai kuwa wingi wa maji ya mafuriko ulitokea Milimani, kule Morogoro, kama ilivyokuwa kule Katesh, Hanang, Mkoani Manyara Juzi.

Hivyo kuanzia nyakati za alfajiri ya Jumanne, Disemba 5, 2023 huko Rudewa Kilosa Morogoro kumekuwa na mafuriko ya maji, mawe na magogo yakisukumwa kwenye makazi ya watu na mkondo wa mto Wami upitao hapo.

“Hii ni kutokana na mvua kubwa inayonyesha zaidi huko milimani utokeapo mto huo na mvua kubwa za hapo Rudewa,” taarifa zaidi zinafafanua.

Hata hivyo bado haijajulikana kama kuna vifo au majeruhi kutokana na mafuriko hayo ya Mto Wami, Rudewa.

Lakini baadhi ya ripoti zilizokuwa zinasambaa kwenye mitandao zimekuwa zikiwachanganya watu hasa pale eneo la Rudewa lilipokuwa linatajwa na watu wasiokuwa na ufahamu mzuri wa Jiografia.

Hii ni kwa sababu kuna maeneo mengine nchini yanayojulikana pia kwa jina hilo.

Kwa mfano, Morogoro kuna Rudewa, wilayani Kilosa, lakini pia kule Njombe kuna sehemeu inayojulikana kama ‘Ludewa,’ na vivyo hivyo kule wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya kuna eneo jingine linaloitwa ‘Rujewa.’

Lakini kwa Mafuriko yaliyotokea tarehe 5 Desemba ni ya eneo la Rudewa, wilayani Kilosa mkoani Morogoro na maeneo yaliyoathirika ni yale yanayopitiwa na Mto Mkubwa wa Wami ambao pia hutiririka hadi maeneo ya Pwani na Dar-es-salaam kama Mto Ruvu.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa mafuriko kutokea mkoani Morogoro mwaka huu, mara ya kwanza matukio kama hayo kuripotiwa ilikuwa ni Januari 2023.

Matukio ya mafuriko yatokanayo na mvua za El-Nino mwaka huu yanaendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini hii ikiwa ni pamoja na Arusha, Simiyu, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Morogoro na Dar-es-salaam.