Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

“Mimi sio Mwanachama wa Chama Chochote Cha Siasa!” Dokta Slaa asisitiza akihutubia Karatu

Mbunge mstaafu wa jimbo la Karatu ambaye pia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dokta Wilbroad Slaa amesisitiza kuwa bado hajajiunga na chama chochote cha siasa.

Hata hivyo, Dokta Slaa aliitikia mwito wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Karatu ambako alihutubia katika moja ya vikao vya Chama Hicho.

Kabla ya kustaafu siasa mwaka 2015, Balozi Slaa alikuwa mwanachama wa CHADEMA na hata kuwa mgombea wake wa Urais mwaka 2010.

Wilbroad Slaa awalisili mjini Karatu kwa mara ya Kwanza  na kufanya mikutano ya ndani katika wilaya yake  baada ya kurejea kutoka ubalozini.

Dkt Slaa  ambaye alialikwa na CHADEMA wilaya katika hotuba yake aliwashukuru wananchi wa Karatu kwa misimamo yao ya kubaki kuwa wapinzani na kuendelea kupigania haki ya wananchi.

Lakini mara alipotakiwa kueleza yeye ni mwanachama wa chama gani, Slaa alisema  kuwa bado hajafungamana na chama chochote cha siasa kwa Sasa.

“Lakini ikiwa Chama Chochote kitanialika kwa ajili ya kuchangia jambo lolote, hususan ushauri, mimi niko tayari kabisa,” Slaa alisema.

Hata hivyo amekisifu chama chake hicho cha zamani kwa uvumilivu mkubwa wa kuendeleza siasa hata baada ya kupitia masahibu mazito na magumu, katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Dkt Slaa amelaani kitendo Cha serikali kuingilia mradi wa maji wa Karatu yaani KAVIWASU, ulioasisiwa na wakazi wa mji huo.

Mradi wa Kaviwasu uliunganishwa na Mamlaka ya maji inayoendeshwa na serikali yaani KARUWASA.

Alisema kuwa amekuwa akipokea simu nyingi kutoka Karatu kwa wananchi wakilalamika kuhusu mradi wa maji wa KAVIWASU Kunyanganywa na serikali bila wananchi kushirikishwa.

Dk Slaa alieleza history ya KAVIWASU kuwa ni mradi wa vijiji sita ambao walitumia fedha zao, nguvu zao kutembea Hadi msitu wa Ngorongoro na kufikisha KAVIWASU ikiwa na mtandao mkubwa wa kuhudumia wananchi wa vijiji hivyo,

“Ndugu zangu kumbukeni wakati maji yalikuwa ya shida watoto wa  kike walikuwa wakifanyiwa vitendo vichafu na vijana wakiwa kwenye foleni ya maji,” alifoka.

Aliongeza kuwa awali wanafunzi wa shule walikuwa wakikesha na kulazimika, kukosa masomo siku inayofuata kwa ajili ya kusaka maji.

“Nashaangaa leo baada ya wananchi wenyewe kutengeneza mradi wao wa maji serikali inakuja kuuvamia bila kuwashirikisha wakazi wa Karatu hao ambao ndio hasa walikuwa waanzilishi,” alisema Dkt Slaa.

Amelaani baadhi ya viongozi wa wilaya kuwapotosha viongozi wa Taifa kuhusu mradi wa wananchi wa KAVUWASU Jambo ambalo Sasa inawarudisha wananchi walikotoka wa ukosefu wa maji na kufikia hatua ya maji kuuzwa Shilingi 500 kwa unit moja.