Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Nyumba N’tobhu ndoa ya mila ambayo hustua wasioifahamu

Nyumba N’tobhu ni mila inayopatikana huko mkoani Mara, wilayani Tarime katika kabila la wakurya.

Hata kwa upande wa nchi jirani ya Kenya katika kaunti ya Migori hufahamika kama I’nyumba Mboke ambapo mwanamke huoa mwanamke mwenziwe.

Kwa wengi hii hushangaza na hata kushtua.

Mara nyingi mwanamke anayeoa huwa ni mtu mzima ukilinganisha na muolewaji, binti mdogo.

Kinachofanyika, mwanamke huyo ‘muoaji’ akishaona windo basi angeifuata familia husika, akikubaliwa atalipa mahari na kumchukua binti kama mkewe. Binti anayeolewa huitwa Mokamoona.

Hapa kuna makundi yanapingana. Kuna wanaodai sio hiyari kwa Mokamoona kuolewa na wengine wanasema ni hiyari.

Inawezakana ni hiyari kweli kwa baadhi yao hasa wale wasio na dosari za kijamii lakini wapo wanaolazimishwa kama sehemu ya adhabu kutoka kwa wazazi wao.

Hawa ni wale walioshindwa shule ama waliozalia nyumbani.

Sababu zinazopelekea mwanamke huyo kuoa binti ni pale ambapo mume wake alifariki akamuacha na mali na kwa bahati mbaya hana mtoto wa kusimamia (aghalabu ni mwanaume) au mume alimuacha na watoto lakini wote ni wa kike sasa anahitaji mtoto wa kiume nk.

Mokamoona (Mukamwana) akishaingia ndani ya ndoa atapewa ahadi kedekede ikiwemo kuishi ki-malikia kama mke, wajibu wake pekee ni kuzaa.

Watoto wakizaliwa huwa wa mwanamke ‘muoaji’, hata ubini huwa wa huyo bi’ mkubwa. Unajiuliza watapataje watoto ilhali wote wako chini ya miliki ya jinsia moja? 

Ili kupata watoto sasa kuna namna mbili, mosi ni Mokamoona mwenyewe kutafuta kijana atakayependezwa naye kwa ajili ya tendo la ndoa.

Pili, bi’ mkubwa hutafuta kijana amtakaye kwa lengo lilelile. Kubwa tu linalozingatiwa hapa, kijana huyo hatakiwi kuwa wa maeneo ya jirani na wakati mwingine hatakiwi kufahamika kabisa kijijini hapo.

Inasadikika kuwa vijana waliofaa zaidi kwa ‘uzalishaji’, mbali na kutoka nje ya eneo, lakini pia huwa ni wale wasiomudu majukumu yao.

Hivyo, iliaminika baada ya kutia ujauzito kijana huyo hatarudi kusumbua.

Kwahiyo, akishafanya tendo la ndoa na Mokamoona hutakiwa kuondoka na asigeuke nyuma maana hakuna alichosahau. Vijana hawa hufanya kazi hiyo kwa ujira ‘uchwara’ tu, chakula ama mbuzi mmoja. 

Wanandoa hawa wakihitaji mtoto mwingine, mwendo ni uleule.

Mabinti wengi walioolewa kwa hiyari ni wale wapenda ‘mseleleko’.

Shida inakuja pale umri wa bi’mkubwa unapokwenda machweo, zile huduma kwa Mokamoona hukoma taratibu na hatimaye kwisha kabisa.

Binti atatakiwa kujikimu na hakuzoea. Ndoa hugeuka shubiri, masimango, kejeli,matusi nk. wakati mwingine hufukuzwa katika himaya.

Mara nyingi ndoa hii haina tofauti na zile rasmi au ziitwazo halali.

Sheria, taratibu na kanuni ni zilezile, hawa kina mama waoaji wana wivu na Mokamoona kama ambavyo mwanaume anamuonea wivu mkewe. Wapo Mokamoona waliopitia madhila mazito kisa tu “ulikuwa wapi mpaka saa hizi.”

Mwaka 2018, huko katika kijiji cha Marrenga, wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Mokamoona aliyetambulika kwa jina la Mugabe Ryoba (23) alichomwa na kitu chenye ncha kali na kufariki dunia na ‘mumewe’ akatokomea.

Hatari  nyingine wanazokumbana nazo Mokamoona katika ndoa hizi ni maradhi kama UKIMWI na kansa ya kizazi kwa sababu hulazimika kushiriki tendo na wanaume tofauti-tofauti bila kinga.

Yaani akishiriki na kijana moja mara kadhaa na bado ngoma ‘ikabuma’ atalazimika kutafuta mwingine.

Wakati serikali ikipiga vita ukeketaji, Nyumba N’tobhu ni kichocheo kingine cha mila hiyo ya hovyo.

Unaambiwa Mokamoona aliyekeketwa ni ‘dili’ sana na ikitokea ‘waoaji’ wakagongana, watapandishiana dau mpaka aibuke mtabe.

Nikauliza, “huyu mwanamke ana uhakika gani akioa atapata mtoto wa kiume?” Nikajibiwa, “Kuna ‘manjegeka’ wanafanya…mara nyingi hawakosei!”