Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Tanzania kuuza nje bidhaa za kilimo zenye thamani ya Bilioni 5/- ifikapo mwaka 2030

Tanzania inatarajia kuongeza thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 5 kutoka kutoka dola bilioni 1.2 ambazo ndio thamani ya mauzo ya nje ya nchi kwa sasa.

Naibu waziri wa Kilimo, David Silinde amesema kuwa sambamba na ongezeko la thamani ya mauzo, sekta hiyo pia inatarajiwa kuzalisha ajira zipatazo milioni 8 itakapofika mwaka 2030.

Naibu waziri wa kilimo alibainisha hayo hivi karibuni wakati wa hafla ya kukabidhi magari na vifaa vingine kwa ajili ya mradi wa Kuboresha afya ya mimea kwa ajili ya usalama wa chakula.

Shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na serikali ya Tanzania walifanya makabidhiano hayo ya magari na vifaa mkoani Arusha, hivi karibuni.

Ni vifaa vilivyogharibu shilingi Bilioni 2.2 ambavyo vitatumika katika kuimarisha afya ya mimea na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi katika mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania TPHPA.

mradi wa Kuboresha afya ya mimea kwa ajili ya usalama wa chakula (STREPHIT) mradi unaoendeshwa kwa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, FAO na Tanzania kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 27.

Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja na magari saba, pikipiki kumi na tisa, vishikwambi, friji kumi na saba, kompyuta 34, dekoda za kusambaza intaneti kumi na saba, mashine nyuki pamoja na vifaa vingine ambavyo vimegharimu kiasi cha fedha  bilioni 2.2

Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Kilimo David Ernest Silinde amesema amefurahishwa na jitihada zinazoendelea katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Aidha amesema kuwa kilimo kina mchango mkubwa nchini kwani sekta hiyo imeajiri asilimia 70 ya watanzania.

Ilielezwa pia kuwa asilimia 65 ya malighafi zinazotumika katika uzalishaji viwandani pia hutokana na mazao ya kilimo.

kwa mwaka na kutosheleza mahitaji ya chakula nchini kwa asilimia mia moja, ambapo katika uzalishaji wa chakula 2021/2022 ulikua ni tani milioni 17.4 mahitaji ni tani milioni 15.7 na ziada ni tani milioni 2.33 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kilimo huchangia mauzo ya nje  kwa asilimia 20 kwa mwaka.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania TPHPA Profesa Joseph Ndunguru amesema maboresho katika sekta ya kilimo yatasaidi kukuza sekta hiyo.

 Ameongeza pia TPHPA imepata mafanikio makubwa hivi sasa ambapo mamlaka  imeweza kusajili jumla viwatilifu vipya 602, imefanya uchambuzi wa sampuli 1950, ambapo kati ya hizo sampuli 1891 zilikidhi viwango na sampuli 3 hazikukidhi viwango,

Mwakilishi wa FAO nchini, Nyabeni Tipo ameiomba Tanzania kuisaidia TPHPA kwa ufadhili wa kutosha ili mamlaka hii iweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake mwakilishi wa umoja wa ulaya Lamine Diallo amesema kupitia mradi huu wa STREPHIT unaofadhiliwa na EU na FAO pamoja na serikali ya Tanzania ni uthibitisho tosha wa dhamira ya pamoja ya kuendeleza kanuni za kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula kwa soko la ndani na nje.