Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Tanzania sasa kuongoza Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori barani Afrika hadi mwaka 2025

Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya 24 ya Misitu na Wanyamapori Barani Afrika, katika uchaguzi uliofanyika jijini Arusha wakati wa mkutano wa kamisheni hiyo kwenye Hoteli ya Gran Melia.

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forestry Services) Profesa Dos Santos Silayo ndiye atakuwa kiongozi wa kamisheni hiyo akiiwakilisha Tanzania.

Profesa Silayo atashika wadhifa wa uenyekiti wa kamisheni ya Misitu na Wanyamapori barani Afrika kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2023 hadi 2025.

Kwa nafasi za Makamu Mwenyekiti, nchi za Mali na Malawi zitashika nafasi hizo za Makamu Mwenyekiti wa Kwanza na Wapili wa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika kwa kipindi cha miaka miwili hiyo hiyo, hadi 2025.

Awali wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema kuwa vikao hivyo vitakuwa na manufaa makubwa kwa nchi na bara la Afrika kutokana na fursa ya majadiliano mahususi ya sekta ya wanyamapori na misitu hususan biashara ya hewa ukaa.

Katika Kikao hicho cha 24 cha Tume ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC 24) na Wiki ya 8 ya Misitu na Wanyamapori Waziri wa Utalii na Maliasili, Kairuki alibainisha kuwa biashara ya Kaboni ni fursa muhimu katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana kupunguza athari za hewa ukaa.

Tanzania imeendelea kuchukua hatua kadhaa za kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu na wanyamapori  kwa ajili ya kusaidia mifumo ikolojia inayostahimili hali ya maisha pamoja na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi.

“Niwashukuru wajumbe kwa kuchagua Tanzania kuwa mwenyeji na sisi kama nchi tutaendelea kusisitiza juhudi za uhifadhi na maendeleo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,”

“Kama mnavyojua TFS imeendelea kufanya majadiliano na wadau katika biashara ya hewa ukaa lakini pia wana misitu, wanaweza kupanda miti ikatunzwa, ikahifadhiwa bila kukatwa na bado wakalipwa fedha kutoka kwa wawekezaji duniani wenye mapenzi mema na biashara ya hewa ukaa” anasema.

Kwa upande wa Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS Prof. Dos Santos Silayo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kwanza wa Kamisheni hiyo amesema kwamba Mkutano huo wa 24 unahudhuriwa na nchi 40 huku ukiwa na mawaziri, wakurugenzi na wadau wa sekta za misitu fursa za kubadilisha uzoefu katika usimamizi wa rasilimali za misitu na wanyamapori lakini pia kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto za sekta hizo.

Anataja moja ya changamoto wanayokumbana nayo ni mabadiliko ya tabianchi ambapo mataifa ya Afrika yanapaswa kuweka mikakati ya pamoja kwa sababu faida za rasilimali misitu zinavuka mipaka.

Prof. Silayo amesema,  lengo la Mkutano huo ni kubadilishana uzoefu wa pamoja ili waweze kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya misitu na wanyamapori.

“Hadi sasa tuna washiriki takriban 300, lakini wapo pia wanaoshiriki kupitia njia ya mtandao. Tunaamini  kupitia majadiliano nchi washiriki zitakwenda kunufaika lakini hasa sisi watanzania, na moja ya majadiliano tutakayofanya ni juu ya biashara nzima ya hewa ukaa ambayo sasa kama nchi tunakwenda kunufaika nayo.”

Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) nchini, Dk Nyabenyi Tipo aliipongeza Tanzania kwa kuingiza ajenda ya mazingira na aliwapa changamoto washiriki waliokusanyika katika mkutano huo kuongoza mapambano ya kuokoa dunia.

Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori ya Afrika ilianzishwa na Mkutano wa FAO mwaka 1959 na inatoa jukwaa la sera na kiufundi kwa nchi za kanda ya Afrika kujadili na kushughulikia masuala ya misitu kwa misingi ya kikanda chini ya kaulimbiu “Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Misitu na Wanyamapori Afrika, Kukuza Usalama wa Chakula na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu”.

Mkutano huo wa 24 wa kamisheni ya Afrika inayosimamia Misitu pamoja na wanyamapori kutoka nchi 53 unaondelea Jijini Arusha kwa siku tano ulianza kufanyika tokea miaka ya 1960 na hii ni takribani miaka 63 ndio Tanzania inapata fursa ya kufanyika mkutano huo.