Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Uwanja wa Ndege Sumbawanga kuwa wa Kisasa Zaidi

Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga unatarijiwa kubadilika na kuwa wa kisasa zaidi kufuatia mkataba rasmi wa kuujenga upya ulitiwa saini wiki chache zilizopita.

Tanzania kupitia Wakala ya Barabara Tanzania TANROADS imesaini mkataba wenye thamani ya shilingi Bilioni 55.908 na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group kutoka China ili kutekeleza Ujenzi, upanuzi na ukarabati wa uwanja wa Ndege wa Sumbawanga mkoani Rukwa.

Awali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa kipindi cha utekelezaji wa mradi huo ni miezi 18 na muda wa uangalizi (defects notification period) wa mradi ni miezi 12. 6.

Amesema kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga kwa sasa kina barabara ya kuruka na kutua Ndege ya kiwango cha changarawe yenye urefu wa meta 1,516 na upana wa meta 30, na kwamba Kupitia mradi huu, barabara hiyo itaboreshwa kufikia urefu wa meta 1,750, 

Aidha upana wa meta 30 kwa kiwango cha lami na uboreshaji wa kiwanja utahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, ununuzi na usimikaji wa taa za kuongozea ndege (AGL) na mitambo ya Usalama (DVOR/DME), barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani, maegesho ya magari na uzio wa usalama.

Waziri Mbarawa ametoa rai kwa viongozi na wananchi wa Rukwa kumpa Mkandarasi ushirikiano wa kutosha ili aweze kukamilisha Mradi huo kwa wakati kulingana na Mkataba.

Pia amewataka kusimamia ulinzi wa mradi na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi na kusisitiza wananchi wanaozunguka eneo la mradi kuepukana na uhalifu wa namna yoyote katika mradi badala yake waulinde  ili wafaidike na fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.

Kwa ushirikishwaji huo, mradi utakapokuwa unaendelea kutekelezwa utasaidia kulinda thamani halisi ya mradi lakini pia kukamilika kwa wakati na ubora.

Wakati huo huo Waziri Mbarawa amewaagiza Wataalam wa Wizara, TANROADS, TAA, TCAA na TMA na wadau wote kufanya kazi kwa weledi na kusimamia utekelezaji wa mradi huo  ili kuhakikisha kuwa Mradi unakamilika kwa wakati.

Mbawara alitoa wito kwa Mkandarasi na Mhandisi Mshauri kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu ili kazi zikamilike ndani ya muda kwa viwango na gharama zilizokubalika.