Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Vifo Barabarani: Magari dhidi ya Wanyamapori

Ni siku ya kawaida kabisa katika barabara inayounganisha mikoa ya Arusha na Manyara kupitia Makuyuni, Minjingu na Babati.

Kundi la wanyamapori wakiwemo pundamilia linaonekana likivuka kutoka upande mmoja wa barabara kuelekea upande wa pili katika eneo la Mwada huku wanyama hao wakitembea taratibu.

Hata hivyo, licha ya kuwa baadhi ya wanyamapori kuonekana wakivuka barabara, madereva walio nyuma ya sukani za magari yanapita kwa kasi eneo hilo, hawaoneshi kujali, maana vyombo hivyo vya moto wala havipunguzi mwendo.

Ikifikia hatua hiyo, kundi la wanyama wanaovuka inabidi kutawanyika, wengine wakikimbilia upande wa pili kwa hofu, huku wenzao wakibaki nyuma kuogopa kuwafuata waliotanguli na hata kuna baadhi wanageuka kurudi walikotoka.

Kwa lugha rahisi ni kwamba madereva hapa wanatishia uhai wa wanyamapori hao.

Barabara ya Arusha-Babati ni sehemu ya njia kuu ya Kaskazini, maarufu kama ‘Great North Road,’ inayounganisha majiji ya Cape-Town, Afrika Kusini na Cairo, Misri kupitia Tanzania.

Hapa nchini, barabara hiyo ni kiungo muhimu cha usafiri kati ya mikoa ya kaskazini, kanda ya ziwa na maeneo ya kusini.

Lakini kwa upande wa Kaskazini mwa Tanzania, sehemu ya barabara hiyo hutumika na magari yanayosafiri kati ya mikoa ya Arusha, Manyara, Mwanza, Singida, Dodoma, Iringa na Mbeya, mengi yakiwa ni malori makubwa ya shehena pamoja na mabasi ya abiria.

Katikati ya Arusha na Babati Barabara hiyo hupita ndani ya eneo la shoroba la Kwakuchinja.

Kwakuchinja ni njia kuu ya wanyamapori wakipita kutoka hifadhi ya Tarangire kuelekea Ziwa Manyara na kurudi.

Mara nyingi sehemu za barabara zinazopita katikati ya maeneo ya hifadhi huwa na matuta kwa ajili ya kupunguza mwendo wa magari na pia vibao vya tahadhari kwa madereva.

Sasa sehemu ya barabara ya Arusha hadi Babati, inayopita katikati ya shoroba haina vibao vya tahadhari dhidi ya wanyama wavukao wala matuta ya kutosha kudhibiti kasi ya magari.

Matokeo yake ni kwamba kipande cha kilomita 80 kwenye barabara hiyo kuanzia Makuyuni hadi Magugu kimekuwa ni sehemu ya chinja-chinja kwa wanyamapori.

“Nimewahi kuona vifo vya Pundamilia wawili waliogongwa na magari wakati wa kuvuka barabara,” anasema Joseph Mwinje kutoka Kijiji cha mwada kwenye kata ya Ngoley.

Mwada ni moja ya vijiji vinavyounda Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori Burunge (WMA).

Baba huyo wa watoto wanne anasema matukio kama haya yakitokea huwa anatoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zingine ziweze kuchukuliwa.

Uongozi wa Jumuiya ya Burunge WMA unaeleza kuwa vifo vya wanyamapori vimekuwa vikitokea mara kwa mara katika njia kuu inayopita katikati ya mapitio haya.

“Zaidi ya wanyama 350 huuawa kila mwaka kwa kugongwa na magari wakati wakivuka barabara ambayop hasa ndio inayokatiza katika maeneo yao ya mapito ya asili,” anasema Katibu wa Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori Burunge, Benson Mwaise.

Inadaiwa kuwa ajali nyingi zinazogharimu maisha ya wanyamapori katika eneo la Kwakuchinja hutokea nyakati za asubuhi na jioni.

Wahifadhi wanaeleza kuwa wanyama wanaokufa wakati wa kuvuka ni kutokana na ajali zinazosababishwa na mwendo kasi wa magari na madereva kutokuwa makini barabarani.

 “Wanyamapori wanakutana na hatari nyingi, kwanza ujangili na sasa pia ajali za barabarani,” anasema Martin Mng’ong’o, Meneja Miradi kutoka taasisi ya Chem-Chem inalojihusisha na utalii pamoja uhifadhi wa katika eneo la Burunge.

Magari dhidi ya wanyamapori

Tatizo hili pia linaikumba Mikumi ambako barabara kuu inayounganisha Dar-es-salaam na mikoa ya kusini, kupitia Morogoro inakatisha ndani ya hifadhi hiyo ya taifa.

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa wastani wa wanyama 200 wa aina tofauti hufa kwa kugongwa na magari katika eneo la hifadhi ambalo hupitiwa na barabara kuu ya Dar es Salaam hadi Zambia.

“Vifo vyote hivyo husababishwa na mwendokasi, japo tunatoza faini kwa kila mnyama anapopoteza uhai lakini haitoshi, madereva wanapaswa kuzingatia sheria za barabara katika maeneo ya hifadhi,” Damian Saru mmoja wa wahifadhi kutoka shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) aliainisha katika moja za vikao vya uhifadhi.

Mbali na Mikumi kumekuwepo na ripoti za tembo kugongwa na treni katika ushoroba wa Nyerere-Selous-Udzungwa.

Tembo hutumia ushoroba huo wakienda na kurudi kati ya Hifadhi za Taifa za Milima ya Udzungwa na Nyerere ambapo hulazimika kuvuka njia ya reli ya TAZARA.

John Noronha, Mtaalamu wa Uhifadhi anaonya kuwa vifo vya wanyamapori katika njia za magari na treni vinapunguza kwa kasi idadi ya viumbe hao muhimu.

Anabainisha kuwa ni muhimu wanyamapori kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine idadi ya wanyamapori na kutokuwepo kwa mwingiliano mzuri wa wanyamapori (gene flow) kama wataendelea kugongwa na kufa pindi wanapovuka barabara kutoka hifadhi moja kwenda nyingine.

Anaongeza kuwa madhara mengine ni kubadilika kwa tabia za wanyamapori, mfano kuwa waoga jambo linaloweza kuleta tabia tofauti ambayo inaweza kuwa changamoto katika maisha ya wanyama hawa.

Kutokana na ukubwa wa tatizo, utafiti uliofanywa na jopo la watafiti kutoka katika Chuo cha Wanyamapori Mweka na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), umebaini kuwa wanyama wanaokufa zaidi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ni Swala kwa asilimia 27.6, Pundamilia (asilimia 3.4), Duma (3.4%), Digidigi 3.4%), Nyumbu (3.6%), Fisi (3.4%), Nyani (3.4%) na wanyama wa aina nyingine.

‘Haraka haraka haina Baraka’

Ili kutokomeza tatizo hilo, utafiti huo uliochapishwa mwaka 2022 na Jarida la Kimataifa la Bioanuwai na Uhifadhi, (Academic Journal, International Journal of Biodiversity and Conservation), umependekeza madereva kuzingatia mwendo uliowekwa na wahifadhi wa kasi ya kilomita 50 kwa saa ili kuwasaidia kuona hata wale wanyama wadogo wanaovuka barabara pia wasimamizi wa hifadhi waongeze alama za barabarani katika maeneo hayo.

Katika moja ya mafunzo ya uhifadhi na Baionuwai yanayoendeshwa na kamouni ya Nukta Afrika, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili waandishi wa habari nchini wametembelea baadhi ya shoroba za wanyamapori zinazopitiwa na barabara kuu nchini.

Katika mafunzo hayo wataalam walishauri wakala wa barabara nchini TANROADS kuweka matuta katika barabara  katika ushorona wa Kwakuchinja ili kuwanusuru wanyama na vifo vya barabarani.

Mbali na kufuata alama za barabarani wataalamu wengine wawasihi wadau wa uhifadhi na usalama barabarani kutokuchoka kutoa elimu kwa madereva wa vyombo.

“Kikubwa ni kuendelea kutoa elimu kwa madereva wanaotumia barabara hizo zinazopita katikati ya hifadhi hasa shoroba, kuwa makini, kujua mwendo wanaotumia, pia suala  hili linahitaji kutafutiwa suluhu na pande zote, wahifadhi, TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania), polisi wa barabarani na Serikali,” amesema Noronha.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoani Manyara, mhandisi Dutu Masele anafafanua kuhusu kugongwa kwa wanyama katika ushoroba wa Kwakuchinja ambao umo ndani ya kipande cha barabara cha Bereko-Babati-Minjingu.

Anasema kuwa kwamba suluhisho lake ni pamoja na Kutoa elimu kwa madereva kuhusu alama za barabaran hususani katika ushoroba wa Wanyamapori.

“Vile vile kushirikisha wananchi na vyombo vya usalama barabarani katika kutoa taarifa za matukio ya vifo vya Wanyamapori; Kuweka alama maalum ili kutambulisha mipaka ya Hifadhi na Kujenga njia za chini kwa ajili ya mapito ya wanyama (Under pass) katika barabara zilizopita kwenye Hifadhi,” anaongeza Injinia Masele huyo katika taarifa yake.

Hivi karibuni Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dk Fortunata Msoffe alizindua kivuko maalum cha kuwezesha tembo kupita kwenye handaki la chini ya barabara katika eneo la hifadhi ya Udzungwa.

Wahalifu hung’oa alama za barabarani

 “Matuta inawezekana ni machache kwenye maeneo kama hayo, hilo tunaliangalia lakini alama za barabarani kwa ujumla tumejitahidi sasa kuziweka kuwalinda watumiaji wa barabara ila kuna wahalifu huviondoa na kusababisha uvunjifu wa sheria,” anafafanua Meneja wa TANROADS, Manyara.