Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Vitabu 3000 vyenye mbinu Asili za Kuhifadhi Mazingira vyaanza kutolewa Vijijini

Wakati ulimwengu mzima ukijitahidi kutumia njia mbalimbali za kupambana na ongezeko la joto pamopja na mabadiliko ya tabia ya nchi duniani, Tanzania imezindua andiko maalum ya mbinu za asili za kuhifadhi mazingira.

Shirika la wanahabari la kusaidia jamii za Pembezoni (MAIPAC) limeanza kusambaza vitabu vya maarifa ya asili katika utunzaji wa Mazingira, misitu na Vyanzo vya maji, katika makundi mbalimbali ikiwepo mashuleni,kwa vijana na makundi mengine.

Vitabu hivyo,vilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dr Seleman Jafo jijini Arusha.

Vitabu hivyo, ni machapisho yanayotokana na simulizi la viongozi wa Mila ya kimasai, wakiwemo wazee, wanawake na vijana.

Viliandaliwa kama sehemu ya mradi wa Uhifadhi na utunzwaji Mazingira kwa maarifa ya Asili ambao unaofadhiliwa na mfuko wa Mazingira duniani (GEF) kupitia shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) katika program ya miradi midogo.

Vitabu 3000 vinatarajiwa kusambazwa katika wilaya za Longido, Monduli na Longido lakini pia katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi ndani na nje ya nchi.

Akizindua vitabu hivyo,Waziri Dk Jafu alisema vitakuwa na Msaada mkubwa kwani jamii kwa Sasa imeanza kusahau maarifa ya asili katika. mambo mbalimbali ya kijamii ikiwepo utunzwaji wa Mazingira.

MAIPAC wanasema kuwa kitabu hicho,kitapelekwa kwa wataalam wengine Ili kuona kinaweza kutumika zaidi katika eneo lipi.

Mfuko wa Mazingira dunian (GEF) na shirika la maendeleo la Umnoja wa Mataifa (UNDP) kupitia mpango wa kusaidia mashirika madogo katika miradi ya utunzaji Mazingira umefadhili mradi huo katika maeneo yanayogusa wananchi.

“Nawaomba UNDP na GEF kuendelea kusaidia MAIPAC ma wengine katika miradi hii kwani hali ya uhalibufu Mazingira ni mbaya Dunia na jitihada kubwa zinahitajika kwa kushirikiana wadau mbalimbali “alisema

Mratibu wa program  ya midogo ya Mazingira kupitia GEF ambayo inasimamiwa  na shirika la UNDP , Faustine Ninga alisema vitabu hivyo vitasaidia kurithisha maarifa ya asili kutoka vizazi vya Sasa na vijavyo.

Afisa Utawala wa MAIPAC Andrea Ngobole amesema shirika la MAIPAC wa kushirikiana na shirika la CILAO pia wametengeneza makala ndefu na fupi za video za maarifa ya asili ambazo zitaendea kusambaza kwenye vyombo vya habari .

“Vitabu hivi tunatarajia vitasomwa na Wanafunzi,vijana , wanawake na makundi mengine katika jamii ikiwepo watungaji wa sera Ili kusaidia kutunzwa Mazingira “amesema

Wakizungumza baada ya kupokea vitabu mwalimu wa shule ya msingi Olbomba Lekishoni Mollel alipongeza MAIPAC Kwa kusambaza vitabu.

“Vitabu hivi nimesoma kidogo ni vizuri na tutawapa vijana wawe wanajisomea haya maarifa ya asili katika uhifadhi wa Mazingira”alisema

Diwani wa Kata ya Olbomba Ndiono Mollel pia Akizungumza baada ya kupokea vitabu hivyo,alipongeza MAIPAC kurejesha vijijini vitabu hivyo.

“Vitabu hivi ni muhimu sana kwani wilaya yetu ya Monduli imeathirika sana na mabadiliko ya tabianchi hivyo wanafunzi na vijana wakisoma vitasaidia kutunza Mazingira “amesema.

Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa Arusha,Blandina Nkini alipongeza pia MAIPAC kuwa na mradi wa kipekee wa Uhifadhi Mazingira kwa maarifa ya asili.

Amesema shirika hilo ni limetumia njia mbadala wa kuibua njia tofauti za kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Maipac ni moja ya mashirika 1114 yasiyo ya kiserekali mkoani Arusha ambalo linafanya kazi ya kuhimiza utunzaji Mazingira kwa maarifa ya asili.

Mradi huu wa maarifa ya asili katika uhifadhi pia umeshirikisha maarifa wa  Halmashauri za Monduli, Longido na Ngorongoro katika hatua zote ikiwepo uhakiki wa taarifa za maarifa ya asili .