Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Wakazi wa Babati wafungwa Miaka 20 kwa kukutwa na Pembe za Ndovu, Manyara

Wakazi wawili wa kijiji cha Endagire wilayani Babati mkoani Manyara ambao hivi karibuni walikamatwa wakiwa na nyara za serikali kinyume cha sheria, wamehukumiwa kutumikia miaka 20 jela kila mmoja.

Hii ni baada ya mahakama kuwatia hatiani kwa kosa la uwindaji haramu.

Waliohukumiwa kifungo hicho na mahakama ya wilaya ya Babati ni John Lulu (42) na Zebedayo Safari (34).

Awali, kwa mujibu wa hati ya mashitaka wakazi hao wawili kwa pamoja walikutwa wakiwa na vipande vya pembe za ndovu bila kuwa na kibali cha uwindaji.

Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi Victor Kimario alisema washtakiwa hao wametiwa hatiani kwa kosa la kumiliki pembe mbili za Tembo kinyume cha sheria.

Pembe za ndovu, ngozi za wanyamapori na vipusa vingine hutambulika kama nyara za serikali. Ni kosa la jinai kukutwa na vitu hivyo bila kuwa na vibali maalum.

Hakimu Kimario alisema kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Octoba 23 mwaka 2022 wakiwa katika kijiji cha Burukeli wilaya ya Babati.

Katika hukumu hiyo alisema washtakiwa hao walikamatwa wakiwa wanasafirisha vipande viwili vya meno ya tembo yenye thamani ya shilingi million 35.1 ambayo ni sawa na tembo mzima.

“Baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka uliowasilisha vielelezo tisa ambavyo vilithibitisha mahakama hiyo kuwa washtakiwa walikutwa na nyara za serikali na kisha kusikiliza upande wa utetezi mahakama imejiridhisha pasipo na shaka kwamba walitenda kosa hilo.”

“Kutokana na kosa hilo mahakama hii inawatia hatiani kwa kukiuka kifungu cha 86 (1) (2) (b) cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori sura ya 283 ya sheria iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kabla ya kusomwa hukumu hiyo wakili wa serikali Rusticus Mahundi akisaidiwa na wakili Abood Komanya alidai mahakamani humo kuwa washtakiwa hawana rekodi ya kufanya makosa ya uhalifu ila kwa kuwa Wanyamapori wana mchango mkubwa katika pato la Taifa ni vyema mahakama hiyo ikawapa adhabu wanayostahili iwe fundisho kwa watu wengine.

Mamlaka za serikali ikiwepo, Mamlaka ya usimamizi wanyamapori (TAWA) ,Hifadhi ya Taifa ya Tarangire , Mwekezaji  sekta ya Utalii taasisi chem chem , Burunge WMA  na halmashauri Babati wamekuwa wakiendesha ulinzi wa pamoja kupambana na matukio ya ujangili.

Hadi Sasa watuhumiwa kadhaa wa ujangili  wa Tembo na Twiga wamekamatwa na kufikishwa mahakamani mkoani Manyara.