Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Pale Wanyamapori Wanapovamia Makazi ya watu Usiku Wakitafuta Maji, kipindi cha ukame Monduli

Moja ya mabwawa ya maji yaliyokauka Monduli

Monduli, moja ya wilaya saba zinazounda Mkoa wa Arusha hukaliwa zaidi na jamii za wafugaji.

Na sehemu kubwa ya wilaya ya monduli ni maeneo ya wazi na shoroba ambamo kuna kila aina za wanyamapori na mara nyingi wakazi wa wilaya hii hujikuta wakikabiliana na viumbe hawa mwitu, hasa pale ambapo mahitaji muhimu kwa pande zote mbili, kama vile maji na maeneo ya malisho yanapoadimika.

Athari za ukame

Hivi sasa wakazi wa vijiji nane, katika kata ya Lepurko na Sepeko wanalazimika kushesha wakijihami baada ya makundi ya wanyamapori kuvamia maeneo yao wakitafuta maji.

Hii ni kufuatia ukame mkali unaoathiri maeneo mengi ya Kaskazini mwa Tanzania, ikiwemo wilaya ya Monduli.

Wanyama hao ni pamoja na Tembo, ambao wamenza kuvamia nyumba za wakazi na kufanya uharibifu mkubwa, kwa kuvunja nyumba na kuharibu matanki ya kuhifadhia maji kwa kuyavuta kutoka kwenye mapaa ya nyumba kwa kutumia mikonga yao na kuyaangusha chini.

Matenki yakipasuka Tembo hao hunywa maji yanayomwagika ardhini.

Wengine ni fisi wanaovamia mazizi na kuua, pamoja na kuwala mifugo kama mbuzi, kondoo na hata ng’ombe wadogo (Ndama), baada ya kukosa mawindo maporini.

Na kwa Zaidi ya wakazi 40,000 wa vijiji hivyo nane wilayani Monduli, wanadai kuwa maisha yao kwa sasa ni mateso.

Wanaume hukesha usiku kucha wakilinda nyumba na mifugo yao dhidi ya wanyama vamizi huku wanawake wakisafiri umbali mrefu kwenda kutafuta maji, kwa ajili ya matumizi.

Wilaya imebaki na vidimbwi na mabwawa machache baada vyanzo vingi vya maji kukauka kutokana na hali ya ukame iliyoikumba wilaya hiyo.

Wanawake na watoto mara nyingi ndio wenye jukumu la kutafuta maji kwa mwendo wa zaidi ya kilomita 15 hadi 20 huku wakipitia hatari mbali mbali za wanyama wakali kama tembo, fisi na Simba.

Kuna suala pia la wasichana kuwa katika hatari ya kuvamiwa na wahuni katika safari zao za kwenda kutafuta maji.

“Ukame umekuwa tishio kubwa sana kwetu, hii imesababishwa na hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi kwani hatujapata mvua tangu mwaka jana iliyopaswa kunyesha mwezi novemba ambayo kikawaida hufululiza hadi mwezi wa kwanza kabla ya kukatika na baadae kuendelea tena mwezi wa tatu hadi wa sita” alisema mwenyekiti wa Kijiji cha Nanja, Yamati Lemomo.

Alisema kuwa hali hiyo imepelekea vyanzo vingi vya maji kukauka ikiwemo chemchem, makorongo na mabwawa ambayo ndio tegemezi kwa wananchi wengi wa wilaya hiyo hivyo kutaabika kusaka maji m’badala ambayo hata hivyo ni machafu na hayafai kwa matumizi ya binadamu lakini hulazimika kuyatumia kujikoa uhai.

“Mabwawa yetu tunayotegemea hapa kama Kilotorok na Lesimingori yamekauka hivyo tunalazimika kufuata maji zaidi ya kilomita 15 katika bwawa pekee lililobakia la Nanja ambayo tulazimika kuchanganya na Unga kidogo wa ugali au majivu kisha kufunika na mfuniko yatulie ili tope lijichuje kwenda chini na yafae kwa matumizi” alisema Naserian Mebukori.

Alisema kuwa wanawake wanakusanyana pamoja na watoto ili kutengeneza kundi kubwa Kwa ajili ya kuamshana saa tisa usiku kufuata maji katika bwawa la Nanja na kurudi asubuhi saa tatu au nne lengo ikiwa kukabiliana na hatari za njiani ikiwemo wanyama wakali lakini pia matukio ya ubakaji.

Kwa Upande wake mwenyekiti wa Kijiji Cha Lepurko, Lendo Melembuki alisema kuwa Kijiji chake chenye zaidi ya wananchi 1138 wanategemea maji Kutoka bwawa la Losikito ambalo limekauka mwezi julai kutokana na mmomonyoko wa udongo.

“Hapa karibu yalikuwepo mabwawa zaidi ya 15 ambayo wananchi wanapata maji lakini yamekauka yote hivyo hulazimika kufuata maji katika Bwawa la Nanja ambalo nalo liko hatarini kukauka kutokana na wingi wa watu wanaochota maji pale lakini pia mmomonyoko wa udongo unaotoka pembezoni mwa Kingo zake na milimani kujaa ndani yake” alisema Melembuki.

“Mateso haya yametufanya tuone kuoga Kila siku ni anasa badala yake tunaoga mara Moja Kwa wiki, lakini hii imetengeneza fursa pia kwa watu wenye uwezo kifedha, wananunua matenki na kukodisha magari ya boza na kwenda kusomba maji masafi Jijini Arusha na kuja kuwauzia wananchi kwa shilingi 1000 kwa ndoo, hivyo tununua kwa ajili ya kunywa tu huku ukiweka marufuku Mtu kunywa zaidi ya kikombe cha robo lita kwa siku”

Mzee Isack Kismo

Akizungumzia hali hiyo, meneja wa mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira vijijini ‘RUWASA’, Neville Msaki alisema kuwa wameiona hali hiyo na wameanza kusambaza maji kwa kutumia magari (maboza) Kwa ajili ya kuwapa afueni wananchi wasinunue tena maji ya kunywa.

“Tuliona tatizo na kufanya tathmini ambapo tuligundua vijiji nane ndio waathirika wakubwa Kutokana na vyanzo vyao vyote vya karibu kukauka, ambapo tuliomba fedha serikali kuu kupitia Waziri wetu wa maji na tukapewa kiasi cha shilingi milioni 100 kutekeleza mpango huo wa dharura”

Alisema kwa Sasa wamefanikiwa kununua matenki 20 ya Lita 5000 kila moja ambayo wamesambaza katika vijiji waathirika na wanaomba maji Kutoka AUWSA na kupeleka kwa magari kila siku Lita 60,000 utekelezaji utakaodumu kwa mwezi mmoja wanaotarajia mvua zitaanza kunyesha.

Alisema katika wilaya ya Monduli kuna Kuna zaidi ya vyanzo vya maji 64, lakini 61 vimeshakauka.

Kwa sasa yamebaki mabwawa matatu pekee ambayo nayo Yako hatarini kukauka kutokana na kuzidiwa uwezo wa matumizi lakini udongo kujaa.

Picha Zote na Bertha Mollel.