Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Kisiba: Ziwa Lenye Chungu Cha Hazina inayolindwa na Joka Kubwa lenye vichwa Viwili

Pengine mmewahi kusoma simulizi maarufu duniani iitwayo ‘Kisiwa Chenye Hazina,’ katika kitabu kilichoandikwa na Robert Luis Stevenson zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Lakini sasa nchini Tanzania kuna Ziwa ambalo linasadikiwa kuwa na Hazina, au walau sanduku lenye vito vya maji.

Ziwa hilo linajulikana kama Ziwa Kisiba au Kisibha, ingawa pia kuna watu huliita Ziwa Masoko, kwa sababu liko sehemu iitwayo ‘Masoko,’ moja ya tarafa zinazopatikana wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.

Katika lugha ya Kinyakyusa, ‘Kisiba,’ maana yake ni ‘Kisima!’

Na hilo ziwa ndio sababu ya kata hiyo pia kuitwa Kisiba, lililopo eneo maarufu kama ‘Pakati,’ kwa kiswahili ni ‘Katikati.’

Eneo la Kisiba lipo kilomita ishirini kutoka Mjini Tukuyu. Sasa Tukuyu ndio makao makuu ya wilaya ya Rungwe.

Ni mwendo wa kama nusu saa hivi au dakika arobaini kwa usafiri wa gari.

Ni kweli kuna hazina ndani ya kina cha ziwa Kisiba?

Kuna simulizi nyingi kuhusu hazina hiyo, lakini ile inayojulikana sana ni ile ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Inadaiwa kuwa baada ya wakoloni wa kijerumani kushindwa vita, walilazima kuikimbia nchi ya Tanganyika.

Ila kabla ya kuondoka, walihakikisha wanaficha mali na vitu vingine vya thamani katika maeneo mengi nchini, kabla ya kuwapisha waingereza ambao walikabidhiwa nchini baada ya vita vikuu vya pili.

Hata hivyo baadhi watu bado hupenda kufurahia maji ya ziwa kisiba bila woga

Kihistoria pia inasemekana kuwa hata kipindi cha Vita ya Kwanza ya Dunia, baadhi ya wazungu walificha mali, hasa madini na vito vya thamani kwa kuyachimbia ardhini au kwenye mahandaki yaliko sehemu zisizofikika kirahisi.

Watu hupenda kwenda kuogelea katika ziwa Kisiba.

Kulikuwa kuna sehemu maalum za kuoga na kuogelea kwa wenyeji, kama vile ‘Masoko,’ ‘Resthouse,’ ‘Lwifwa,’ na ‘Mibula.’

Sasa haya maeneo ni kwamba yana vina vifupi kidogo vya maji, hivyo basi inakuwa salama kwa watu kujirusha humo kwa ajili ya burudani ya kupiga mbizi.

Lakini sehemu iliyokuwa na kina kifupi zaidi ni ile ya LWIFWA, ambako pia kabla hujafika kwenye ukingo wa maji unapita kwenye eneo lenye uwanja, au tambarare.

Hapo sasa ndio eneo ambalo wazungu walikuwa wakifika na kufanya tafiti zao, wakati mwingine kwa kigezo cha kufanya utalii.

Hadi leo, Lwifwa ni sehemu maarufu kwa wageni kutoka nje ya nchi, hususan, wazungu, wakiwemo wajerumani, waingereza na hata wamarekani.

Lakini pia mkabala na eneo hilo, kuna sehemu ambayo walizikwa watu watatu, wote wakiwa ni raia wa Ujerumani.

Sehemu hiyo waliyozikwa wajerumani huitwa ‘Bomani.’ Na makaburi yenyewe yako hapo maalum kwa ajili ya ukumbusho,

Sasa inadaiwa kuwa wajerumani kadhaa walifia katika maeneo hayo kipindi cha vita.

Waliuawa wakati wakipambana na waingereza waliokuwa wanajaribu kuwatoa hapo kwa nguvu.

Mjerumani mwingine anadaiwa kupoteza maisha wakati akipambana na Joka Kubwa lililokuwa linalinda hilo ziwa.

Haijulikani ilikuwaje, lakini hilo Joka, linalodaiwa kuwa na vichwa viwili, linasemekana kuwepo katika ziwa hilo hadi leo, maana ni kiumbe wa miujiza.

Joka hilo lipo katikati ya ziwa hilo la KISIBA ni linadaiwa kuwa ni likubwa sana.

Linaishi katikati ya kina cha ziwa Kisiba, ambako kwa mujibu wa wenyeji, ni sehemu yenye Sanduku Kubwa lililojaa madini ya thamani pamoja na Chungu kikubwa kilichosheheni fedha za kijerumani, ziitwazo ‘Rupia.’

 Rupia hupendwa sana na waganga wa kienyeji, wao wanadai kuwa sarafu hizo zina nguvu ya ziada ya kimiujiza.

 Mwaka 1996, mwezi Agosti, Kuna Wazungu walifika eneo la Kisiba.

Wenyeji wanahisi kuwa walikwenda kuchukua SANDUKU hilo, ingawa walikuja nyuma ya pazia ya kufanya utafiti wao katika ziwa hilo,

Sasa utafiti ule ulihusisha kuweka mashine katikati ya ziwa. Ili kujua wana lichukuaje hilo SANDUKU,

Inadaiwa kuwa sarafu hizo za Rupia bado zina thamani kubwa sana.

Hata hivyo wakati wanajiandaa kuweka mitambo yao kule ziwani, ghfla likaibuka lile joka lenye vichwa viwili.

Basi bwana. Ikabidi watupe kila kitu na kukimbia na hawakuahi kurudi tena, katika ziwa lile.

Maajabu mengine ni kwamba Kila Ifikapo Saa 12 Jioni, huwa unaibuka mstari mmoja mrefu sana katika ziwa Kisiba.

Mstari huo wa kwenye maji huwa unaanzia eneo la LWIFWA, kuelekea BOMANI usawa wa eneo ambalo yako yale makaburi matatu ya wazungu.

Ni mstari wa ajabu ambao hakuna ajuaye husababishwa na kitu gani.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari