Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Benki Kuu ya Tanzania yapata Gavana Mpya

Benki Kuu ya Tanzania (Bank of Tanzania) imepata Gavana Mpya kufuatia teuzi mpya zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu iliyoifikia Taifa Tanzania, Rais Samia amefanya uteuzi wa viongozi na wakuu wa taasisi muhimu za umma kama ifuatavyo.

Rais Samia amemteua Bwana Emmanuel Mpawe Tutuba, kuwa Gavana Mpya wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Emmanuel Tutuba ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anapokea nafasi hiyo ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kutoka kwa Profesa Florens Luoga.

Emmanuel Tutuba

Taarifa hiyo rasmi kutoka Ikulu inaeleza kuwa Profesa Florens Luoga amemaliza kipindi chake kama mkuu wa hazina ya taifa.

Itaumbukwa kuwa Profesa Luoga, aliyeteuliwa na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli, aliipokea nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Benno Ndulu.

Katika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Bwana Emmanuel Tutuba, Rais Samia Suluhu Hassan pia amemteua Daktari Natu El- Maamry Mwamba kuwa Katibu Mkuu mpya katika Wizara ya Fedha na Mipango.

Dokta Mwamba alikuwa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kabla ya uteuzi wake, Mwamba alikuwa pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) yaani Kilimanjaro Airports Development Company (KADCO).

Kwa sasa Dokta Mwamba ndiye anachukua nafasi ya Bw Emmanuel Tutuba ambaye ameteuliwa kuwa Gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari