Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Michuano ya Tenisi Afrika Yaanza Burundi Huku Tanzania ikiwakilishwa na Vijana tisa

mchezaji wa tennis kutoka Rwanda katika michuano ya Afrika nchini Burundi

Tanzania imeteua wachezaji tisa vijana wa mchezo wa tenisi kuunda timu ya taifa itakayowakilisha nchi katika mashindano ya vijana ya Afrika Mashariki yaliyoanza jijini Bujumbura Burundi na ambayo yatashirikisha zaidi ya nchi kumi.

Michuano hiyo ya Tenisi inayodhaminiwa na shirikisho la mchezo huo barani Afrika (CAT) yanafanyika kwa wiki mbili kuanzia Januari 7 hadi Januari 15 Mwaka 2023.

Mashindano hayo ya mchezo wa Tenisi chini ya uongozi wa shirikisho la tenisi duniani (ITF) ni maalum kwa vijana walio na umri chini ya miaka 14 na 16 na  yatashirikisha jumla ya nchi 11 kutoka ukanda wa Afrika mashariki na Kati.

Miongoni mwa wachezaji watakaoiwakilisha Tanzania, watano ni kutoka Arusha, watatu kutoka Kilimanjaro na mchezaji mmoja kutoka klabu ya Gymkhana Jijini Dar-es-salaam.

Wote hao tayari wameanza michuano hiyo jijini Bujumbura nchini Burundi.

Wachezaji hao ni Fred Ongige, Faith Nyamakula na Hadija Said, Elia Balthazar na David Tarimo ,Nasha Singo na Rachel Swai, Eunice Kimaro na Happy David wameambatana na viongozi wawili ambao ni Kocha wao, Goodluck Mollel na Matroni Faraja Yindi.

Michuano hiyo ya kimataifa imeandaliwa na Shirikisho la Tenisi Afrika (CAT) kwa ushirikiano na Shirikisho la Tenisi la Kimataifa (ITF) na Shirikisho la Tenisi la Burundi (BTF).

Nchi zitakazoshiriki ni Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Tanzania, Eritrea, Djibouti, Comoro, Shelisheli ,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mwenyeji Burundi.

Kwa mujibu wa waandaaji, kila nchi shiriki ina haki ya kupeleka timu itakayojumuisha wachezaji wasiozidi 12 kwa ajili ya mashindano ya vijana kwa umri huo wa  chini ya miaka 14 na 16 ambao watadhaminiwa na CAT.

Lakini kwa upande wa Tanzania waliamua kupeleka  wachezaji tisa tu kwa sababu fedha hazikutosha kulipia idadi ya awali ya  watu 15 ambao walikuwa wachezaji 12 na viongozi watatu.

Nicholas Leringa ni Kocha wa Tenisi wa Klabu ya Arusha Gymkhana alisema kuwa mashindano hayo ni katika kusaka nafasi ya kufuzu kwa Mashindano ya Tenisi ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari