Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Rais Samia aombwa kuingilia sakata la hati ya Kampuni ya Uchukuzi Iringa

Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Uchukuzi na Biashara Iringa, Caroline Mwakabungu amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kupata hati yao iliyochukuliwa mwaka 2019.

Hati ya umiliki wa kampuni hiyo ijulikanayo kama Iringa Transport and Trade Company Limited inadaiwa kutwaliwa na watu waliojitambulisha kuwa wanatokea katika Tume ya uchunguzi wa mali za serikali kipindi cha awamu iliyopita ya tano.

Mkurugenzi Caroline Mwakabungu

Mwakabungu, alitoa ombi jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usumbufu pamoja na matatizo ambayo wamekuwa wakiyapata kutoka kwa wanasiasa na mamlaka mbalimbali za serikali.

Alisema anamuomba Rais Samia kumsadia kupata hati hiyo ya umiliki ambayo ilichukuliwa mikononi mwa marehemu baba yake Dakta Lucas Hale Mwakabungu, aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi.

Maafisa walioichukua hati hiyo walidai kuwa wanakwenda kuifanyia ukaguzi.

“Mwaka 2019 walikuja watu kutoka Tume ya uchunguzi mali za serikali iliyoundwa wakati wa utawala wa hayati Rais John Magufuli na kufanya ukaguzi,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo kampuni hiyo awali ilikuwa ikimilikiwa na Serikali ikijulikana kama Iringa RETCO na baadae kununuliwa na Baba yake pamoja na wenzake kadhaa.

Hiyo ilikuwa ni kipindi cha awamu ya tatu, ya Rais Benjamin William Mkapa, ambapo mashirika mengi ya umma yalibinafsishwa.

“Walipokuja mwaka 2019 wakadai kuwa wao ni tume ya serikali ambayo inakagua mali za serikali kama ziliuzwa kihali baba alijaribu kugoma kutoa hati ile lakini walimlazimisha kutoa hati hiyo wakimtisha kwamba ikiwa ataendelea kukaidi wangempa kesi ya uhujumu uchumi,”

Ndipo ikabidi Dakta Mwakabungu aitoe ile hati lakini hadi leo haijulikani ilipelekwa wapi.

Mwaka mmoja baadae baba yake, yaani Lucas, alifariki dunia.

Kwa mujibu wa Caroline, wamejaribu kuifuatilia hati hiyo hadi hazina lakini kule nako wanadai kwamba haipo na haikuwahi kupelekwa hapo.

Mkurugenzi huyoi anabainisha kuwa kutokana na hali hiyo hawajui nini hatima yao kwakua kuchukuliwa kwa hati kumekuwa ndiyo chanzo cha wao kupata usumbufu na vitisho kutoka kwa baadhi ya viongoi wa serikali kutaka waondoke katika kampuni hiyo kinyume cha utaratibu.

“Mimi ni mtoto wa marehemu nilichaguliwa kama mkurugenzi mtendaji na mwanahisa,”

Nina hisa nyingi na ninawakilisha kundi la watu wenye hisa nyingi kwenye kampuni lakini napata misukosuko mingi kutoka kwa watu mbalimbali  kinyume na sheria ya makampuni binafsi.

“Hata hivi ninavyozungumza na nyinyi hapa ninayo barua ya mkuu wa mkoa ambayo inanitaka nikabidhi ofisi ndani ya saa 48 kwa kamati ambayo sijui hata imeundwa na nani na jambo la ajabu ni kwamba hii ni kampuni binafsi inakuaje mamlaka za serikali zinaingilia kinyume na sheria ya kampuni binafsi kuna siri gani nyuma ya pazia?” alihoji

Kadhalika, alisema anamuomba Rais Samia kuingilia kati mgogoro huo kwakua unakatisha tamaa kwa wawekezaji wazawa kinyume na jitihada zake ambazo amekuwa akizifanya kuweka mazingira wezeshi hasa kwa wanawake.

Pia, alisema kuchukuliwa kwa hati hiyo kumesababisha mambo mengi kukwama ikiwemo kushindwa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha ili kufanya uwekezaji.

“Tunafanya kazi tukiwa hatujui nini hatma ya kampuni hii kwani toka kupokonywa hati imekuwa domant (haiendelei) kwakuwa tunashindwa hata kuingia ubia na wawekezaji wengine,kukopa fedha hivyo kukosesha mtaji wa kujiendesha na kuikosesha mapato serikali”alisema

Naye, Mwanasheria wa kampuni hiyo Mpeli Mwabungu alisema wanaiomba serikali kuingilia kati sakata hilo kutokana na uwepo wa tabia ya baadhi ya viongozi kuingilia maamuzi kwa kutoa matamuko ya kisiasa ambayo yanasababisha baadhi ya wapangaji wao kugoma kulipa kodi kwa madai kuwa hilo ni eneo la serikali.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari