Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Kuadimika kwa Sauti Nzito katika nyimbo za nyakati hizi, ni Kupotea kwa ladha ya Muziki

Je. Inaashiria kifo cha Muziki Halisi?

Katika fani ya Muziki Halisi ambao hapa Tanzania unaitwa ‘wa dansi,’ kuliwahi kuwa na waimbaji wa sauti zenye kilo nyingi, wengi hawapo tena wachache wamebaki ingawa baadhi hawaimbi tena.

Waimbaji waliokuwa na sauti nzito (wengine wakiziita bezi) ni pamoja na Muhidin Mwalimu ambaye jina lake la ‘Gurumo,’ wengi walilichukulia kama utambulishi wa sauti yake hiyo.

Halafu yupo Cosmas Thobias Chidumule. Huyu Chidumule, mbali na kuwa na sauti nzito, pia anasemekana kuwa ndiye muimbaji aliye na sauti ya kipekee nchini isiyoweza kuigwa na mtu mwingine yeyote.

Mwenzake Chidumule enzi za Sikinde na baadae Safari Sound, alikuwa ni Max Bushoke, naye akiwa na sauti nzito ingawa laini.

Kisha akaja Jerry Nashon ambaye ilibidi apachikwe jina la utani “Dudumizi,” na Hemed Maneti, kutokana na sauti yake ya kutetemesha.

Maneti pia tunaweza kumuweka kwenye kundi la watu wenye sauti nzito. Hata Marijani Rajabu ambaye aliweza kuimba sauti zote za juu na chini.

Na katika kundi lao hilo anaingia Kikumbi Mwanza Mpango, maarufu kama King Kiki.

Wengine ni pamoja na Mikidadi Seif, Hamza Kalala (ingawa huyu mara nyingi alikuwa na mpiga gitaa la solo), Mzee Kitenzogu Makassy na Dokta Remmy Ongala.

Freddy Ndala Kasheba ingawa hakuimba sana lakini alikuwa na sauti nzito kama inavyosikika kwenye “Hasira za Chunusi.”

Na yupo pia Mobali Jumbe aliyetamba na OSS. Enzi za Maquis du Zaire alikuwepo Nkurlu wa Bangoiye.

Idadi yao inajumuisha wanamuziki wengine wengi wa zamani akiwemo Hamis Amigolas, na pia Rogath Hegga Caterpillar wa miaka ya hivi karibuni.

Cosmas Chidumule (Kushoto) na Muhidin Mwalimu Gurumo

Kwenye miziki ya taarab kulikuwa na Mzee Issa Matona na Ally Star, hawa pia waliimba kwa sauti nzito.

Katika kizazi kipya yupo Kijana Enock Bella akiwa na Yamoto Band alijitahidi kuimba kwa sauti ya kilo nyingi, ingawa baada ya kujitenga na kuwa peke yake siku hizi ameiacha sauti hiyo.

Jirani ya Tanzania, yaani Kenya alikuwepo Kasongo wa Kanema na Moreno wa Batamba, ambao hata hivyo awali walikuwa hapa Tanzania.

Pia kule DRC alikuwepo Muzola Ngunga (Orchestra Kiam), Nzaya Nzayadi (Lipualipua), Mopero chini ya kinara mwenyewe Lwambo Lwanzo Makiadi.

Kwingine Afrika walikuwepo pia waimbaji wa sauti nzito. Tukianza na Pat Shange wa Afrika Kusini, pamoja na Lucky Dube.

Magharibi mwa Afrika undemkuta Manu Dibango na Fela Anikulapo Kuti miongoni mwa wengi. Hawa pia sauti zao zilikuwa hazibebeki kwa uzito.

Nje ya Afrika nako kulikuwa na kina Rick Astley, Colonel Abraham, Bob Farrel, Lionel Richie, Julio Iglessious na wengine.

Nyongeza nyingine katika hili andiko ni kutoka kwa Marc Nkwame