Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Jinsi ya Kuupandisha juu tena Muziki wa Dansi Ulioporomoka

Wakati mwanamuzi Hemedi Maneti Ulaya, anafariki mwaka 1990 wananchi wa Kenya waliomboleza sana.

Na ilifikia kiasi cha wao kutuma barua nyingi kuelezea masikitiko yako kwenye vyombo vya habari vya nchi hiyo, yakiwemo magazeti na redio.

Ni wakenya wachache sana waliofahamu kuwa Hemedi, aliyejulikana kama ‘Chiriku Maneti,’ alikuwa ni mtanzania.

Hii ni kwa sababu bendi ya muziki aliyokuwa anaitumikia, yaani Vijana Orchestra tangu enzi za Vijana Jazz, ilikuwa maarufu sana Kenya kiasi cha kuwafanya watu wengi nchini humo kuamini kuwa maneti alikuwa ni mkazi wa Nairobi.

Na siyo Vijana Orchestra tu, bali hata DDC Mlimani Park, Juwata Jazz (siku hizi msondo), Remmy Ongala na Super Matimila, pamoja na Dar International ya Marijani Rajabu.

Nyimbo za bendi hizo ndizo zilikuwa zinapamba vipindi vya Redio na Televisheni za Kenya enzi za ‘Sauti ya Kenya,’ (VOK) hadi KBC.

Wakati muziki wa Tanzania ukitawala anga zima la Afrika Mashariki kwenye miaka ya 70, 80 hadi vipindi vya mwanzo vya 90, bendi hizo pia zilikuwa zinatesa kwenye kumbi za starehe za miji mikubwa nchini, hasa Dar-es-salaam, Mwanza na Arusha.

Kama alivyoimba Kikumbi Mwanza Mpango (King Kiki), alipokuwa na Orchestra Safari Sound mwaka 1979;

Mtoto wa mjini ninayo sababu ya kuringa; roho yanigonga gonga sijui raha nimkabidhi nani.

“Oh Dar-es-salaam yachemka kama bahari jamani, kumbi za starehe huko na huko nifanyeje, magoma motomoto sehemu sehemu nisemeje?”

OSS-Mtoto wa Mjini

Na kweli karibu kila ukumbi dar ulifurika watu enzi hizo bendi zikifanya maonesho; iwe ni Amana Ilala, White House Ubungo, DDC Magomeni au Kariakoo, Vijana Social Hall, Legho Hotel na hata New African ghorofani.

Kwa mujibu wa King Kiki, “Ukiwakosa wana Kamanyola (Maquis), pitia Sikinde ngoma ya Ukae (Mlimani), usisahau wana msondo ngoma ….”

Halafu anaendelea kuzitaja bendi zilizokuwepo; Mwenge Mashujaa, Dar International (Super Bomboka), Urafiki (Chakachua), Uda Jazz (Bayankata), Matimila (Talakaka) na zinginezo.

Bendi zote hizo, zilikuwa na mashabiki wengi kiasi cha kuziwezesha kuwalipa wanamuziki wake kwa viimgilio vya kumbini tu.

Mkumbuke zamani hakukuwa na CD wala kaseti (tapes) na ni bendi chache to ziliweza kurekodi kazi zao kwenye santuri.

Asilimia kubwa ya muziki wa bendi nchini ulirekodiwa katika studio za Radio Tanzania Dar-es-salaam (RTD) barabara ya Pugu.

Hizo zilitumika kwenye vipindi kadhaa za stesheni hiyo ya taifa ambayo kwa bahati nzuri ilikuwa inasikika katika eneo zima la maziwa makuu; Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Zaire (Congo) na sehemu chache za Malawi na Zambia.

Redio za nchi zingine zilikuwa zinakuja kutafuta nyimbo za Tanzania ili kutumbuiza wasikilizaji wake

Kutokana na jaribio la Mapinduzi lililolenga kumng’oa Rais Dabiel Arap Moi wa Kenya mwaka 1982 serikali ya nchi hiyo ilipiga marufuku stesheni zake za Redio kecheza nyimbo zilizoimbwa kilingala au lugha zingine za ughaibuni, lengo likiwa ni kujenga umoja wa kitaifa kwa kupitia Kiswahili.

Kenya ilikuwa na vikundi vidogo vidogo vya muziki vilivyoimba nyimbo za kikabila zaidi na hii pia haikumfurahisha Moi wala serikali yake na akaagiza stesheni ya taifa kuachana na miziki ya kikikuyu, kikamba, kijaluo na ki kalenjini na badala yake kupiga nyimbo za Kiswahili tu.

Hatua hiyo ilichangia sana katika kufanya redio za nchi hiyo kujaza maktaba zake kwa nyimbo kutoka Dar-es-salaam, hadi amri hiyo ilipotenguliwa tena mwaka 1984.

Na zuio liliondolewa baada ya mwanamuziki nguli wa Zaire (Congo), Tabuley kuubadilisha wimbo ulioitwa ‘Nakei Nairobi,’ na kuwa kurekodiwa upya ukiitwa ‘Baba Moi Nairobi,” kwa mashairi ya kumsifia Rais Moi.

Sasa ikiwa bendi za Tanzania zilikuwa maarufu kiasi hicho, ni kwa nini siku hizi miziki ya dansi inashindwa kufurukuta?

Hapa ‘Muziki wa Dansi,’ ukitafsiriwa kuwa ndio muziki halisi unaopigwa kwa vyombo mbalimbali vya muziki na kushirikisha wanamuzi wenye vipaji na uelewa wa fani hiyo.

Kwa sasa bendi za muziki, hazipati wahudhuriaji wengi wa maonesho yao kama zamani.

Siku hizi unaweza kukuta bendi inapiga baa, kiingilio kikiwa ni kinywaji chako tu; soda, bia au chupa ya maji.

Halafu tena unakuta bendi inapiga huku mwenye baa pia kawasha televisheni.

Hapo anadai kuwa kuna wapenzi wa muziki na vile vile wapo wateja wanaotaka kuangalia mpira au taarifa za habari, kama siyo vipindi vya National Geographic kwenye runinga.

Na ukiwauliza wanamuziki wengi nchini wataanza kusingizia stesheni za redio, nyingi zikiwa zile za masafa mafupi yaani FM, kwamba zinatumia muda mwingi kupiga nyimbo hafifu za ‘bongo fleva,’ na kuacha muziki halisi wa bendi.

Hata hivyo ukiangalia uwezo wa redio hizi utitiri za FM kuweza kukuza wimbo wowote sio mkubwa; kwanza kila stesheni inapiga nyimbo zake, pili uwezekano wa stesheni moja kufikia watu wengi kwa wakati mmoja ni mdogo.

Halafu tofauti za zamani, enzi za Radio Tanzania na Sauti ya Kenya, watu hawaziamini sana stesheni za FM za siku hizi kuwa ndio neno la mwisho kuhusu kipi chema au kibaya.

Ila ukifuatilia vizuri utaona kuwa idadi ya wahudhuriaji wa maonesho ya bendi za muziki inapungua kutokana na mabadiliko ya hali za maisha.

Zamani watu walikuwa wakiishi kwa wingi sehemu moja lakini siku hizi watu wamesambaa maeneo mbalimbali.

Kwa mfano eneo la Kariakoo, Dar-es-salaam lilikuwa makazi ya watu siku za nyuma, lakini sasa biashara ndizo zinatawala pale. 

Kwa hiyo wale watu ambao zamani wangeujaza ukumbi wa DDC Kariakoo wamehamia mbali, Mbagala, Mbezi na hata kibaha.

Kariakoo imebaki na watu 9000 tu, na sio wote wanataka muziki.

Sababu nyingine ni kwamba, siku zimebadilika. Watu wana uwezo wa kupata maonesho ya muziki wakiwa ndani ya nyumba zao. 

Televisheni zilizoungwa kwenye setelaiti na Intaneti zinaweza kuleta tamasha zima ndani ya sebule na kuiwezesha familia nzima kuhudhuria muziki bila kutoka nje ya mlango wao.

Ili kunusuru muziki wa dansi

Wakati zamani kumbi za muziki zilikuwa maalum kwa muziki tu, sasa bendi zinatakiwa kujitanua kidogo, warejee maonesho ya zamani ya Klab Raha Leo, Redio Tanzania.

Marehemu Julius Nyaisanga (Uncle J) yeye alikuwa anaalika bendi moja, kisa watazamaji wanakuwa wafanyakazi wa taasisi au kampuni mojawapo nchini.

Halafu mbali na muziki, alichanganya vichekesho na maigizo mafupi hivyo kufanya hata watu walioko majumbani kufurahia kipindi kupitia sauti za redio tu bila hata kuona.

Msondo, Sikinde, Wazee Sugu (Capitale) na Banana Zorro wanatakiwa kuongeza vionjo kwenye matamasha yao, muziki uwepo lakini vichekesho, tamthilia fupi za jukwaani na chemsha bongo.

Tayari bendi zina kete kubwa zaidi ya ‘Bongo Fleva,’ wao wana wapiga vyombo, wana waimbaji wa ukweli na muziki wao unaweza kusikilizwa na watu wote, wakubwa kwa wadogo, lililobaki ni kuongeza vionjo kidogo tu.

Labda sasa bendi zijiongeze na kuiga mfumo wa kujitangaza kidijitali.

Lakini pia kuanza kuwaonesha watu umuhimu wa vyombo vya muziki.

Warekodi video zinazoonesha wapiga vyombo wakiwa kazini, ili kuwe na washabiki wa saxophone, gitaa, ngoma, sambamba na waimbaji.