Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mfuko wa Hifadhi za Jamii Kutoa Mikopo, Mashine Kusaidia Uwekezaji Katika Viwanda Vidogo nchini

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeandaa mpango maalum wa kutoa mikopo ya mitaji kwa wawekezaji wadogo nchini ili waweze kuanzisha viwanda vipya vidogo na vya kati.

Kwa mujibu wa uongozi wa NSSF lengo ni kuwasaidia watanzania kupanua wigo wa ajira, kuongeza vipato vyao na pia kukuza uchumi wa Taifa, huku mfuko huo na ukiongeza idadi ya wananchama.

Meneja wa NSSF mkoani Arusha, Josephat Komba anaelezea kuwa mfuko huo pia una majukumu yaa kuwainua wawekezaji wa Tanzania ikiwa ni njia mojawapo ya kuisaidia jamii husika.

Komba alikuwa akizungumza na wawakilishi wa vyombo vya habari jijini Arusha wakati wa maonesho maalum ya ubunifu na ujasiriamali yaliyoandaliwa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo na vya kati (SIDO) Kanda ya kaskazini.

Mpango huu wa NSSF, kwa mujibu wa meneja huyo ni mpya na maalumu katika kuwasaidia wajasiriamali kupata mtaji wa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.

“Hii ni katika kusaidia kukabiliana na tatizo la ajira nchini na pia kujenga uchumi wa watu binafsi, kuleta na kuiongezea serikali mapato kupitia ulipaji wa kodi,” alisema Komba.

“Katika Mpango huu tunashirikiana na wadau wengine ambapo mbali na Serikali, wamo pia benki ya Azania wanaoratibu mikopo hiyo, sambamba na Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo vodogo (SIDO) na Veta wanaosaidia kuunda vikundi na kuwapatia elimu ya ujasiriamali ili kukidhi sifa ya kupata mkopo huo!”

Josephat Komba – Meneja NSSF

Alisema kuwa katika utelekezaji wa mpango huo, wameweza kutoa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 858 kwa vikundi 18 huku wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi waliomo katika sekta isiyo rasmi.

Kupitia mpango huu mpya NSSF wanalenga kuhakikisha kuwa wawekezaji wadogo wanapata msukumo wa kuweka akiba kwenye mifuko hii ya jamii.

Kwa sasa mfuko huo, mbali na mafao, unatoa huduma zingine za zaida zikiwemo bima za afya, bima za biashara, mitaji ya uwekezaji na mikopo.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru Richard Ruyango yeye anashauri kuwa pamoja na kuwasaidia wajasiriamali kupata mikopo hiyo ya mitaji, kuna umuhimu wa taasisi za fedha na mabenki kupunguza viwango vya riba za mikopo.

“Ili hawa wajasiriamali ili waweze kuendesha biashara zao hadi ifikie asilimia chini ya kumi kuliko sasa hivi mnawapiga kuanzia asilimia 13 hadi 15” alisema DC Ruyango.

Meneja wa SIDO, Mkoa wa Arusha Jalphary Donge alisema lengo la maonyesho hayo ni kuwakutanisha wajasiriamali kwa ajili ya kuhamasisha ubora wa bidhaa wanazotengeneza.

Malengo mengine ni pamoja na kukuza soko la wajasiriamali Kanda ya kaskazini na pia kuhamasisha watu waweze kupenda bidhaa za ndani baada ya kufika na kujionea ubora wa vitu husika.

“Maonyesho haya ni mpango wa kuwasaidia vijana kukabiliana na tatizo la ajira na ukuzaji wa uchumi nchini ambao unawasaidia kuwakutanisha na taasisi, makampuni na mashirika binafsi yanayohudumia wajasiriamali ikiwemo Mikopo, Masoko na Bima!”