Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Tatizo la Umeme nchini mbioni kuisha kabisa

Baada ya miezi kadha ya sintofahamu, hali ya umeme sasa imeanza kuboreka nchini.

Na itakapofika mwezi ujao wa Machi, pengine tatizo la kukatika kwa umeme litakuwa limekwisha kabisa.

Upungufu wa nishati hiyo tayari umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mikakati inayochukuliwa na shirika linaloshughulikia huduma za umeme nchini.

Taarifa rasmi kutoka kurugenzi ya mawasiliano ya shirika hilo (TANESCO) inafafanua kuwa mwaka uliopita wa 2022 nchi ilikuwa na upungufu wa umeme wa kati ya megawati 200 hadi megawati 300.

Kwa mujibu wa shirika hilo, ukosefu wa nishati hiyo umepungua kwa kiasi kikubwa na kufanya hali ya upatikanaji wa umeme kuboreka zaidi, kutokana mipango ya muda mfupi na ya kati.

Baadhi ya mipango ya muda mfupi ni pamoja na kukamilika kwa matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kinyerezi namba II ambao umeshaanza kuzalisha megawati 45 za umeme.

Umeme huo ulianza kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 24 Novemba 2022.

Shirika la Umeme pia linadai kukamilisha matengenezo ya mitambo miwili iliyopo katika kituo cha Ubungo namba III ambayo pia imeshaanza kuzalisha kati ya megawati 35 na 40 za umeme kwenye Gridi ya Taifa tarehe 25 Novemba mwaka jana.

Vile vile TANESCO wanasema kuwa wameshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kidatu na umeshaanza kuzalisha megawati 50 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 30 Novemba 2022.

Pia, ufungaji wa mitambo mitatu iliyopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I (Kinyerezi I Extension) umekamilika na tayari mashine hizo zinaingiza megawati 120 za umeme kwenye Gridi ya Taifa.

Mipango ya muda wa kati ambayo inafanyika na inategemewa kukamilika hivi karibuni ni pamoja na majaribio ya mtambo mmoja uliopo katika kituo cha Ubungo namba III ambayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari 2023.

Kwa mujibu wa TANESCO, shirika linategemea mtambo wa mwisho uliopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I (Kinyerezi I Extension) utaanza kuzalisha megawati 45 za umeme kwenye Gridi ya Taifa ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari 2023.

Licha ya kwamba hali ya upatikanaji umeme imeboreka, Shirika limeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya umeme kutoka asilimia 6 hadi 11 kwa mwaka, ongezeko hili limeshuhudiwa katika kipindi cha miaka miwili kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Vilevile, mvua za vuli zilizonyesha hivi karibuni hazikuwa toshelevu kama ilivyolegemwa. Aidha, Shirika litaendelea kufanya matengenezo ya mitambo yake ambayo haikufanyiwa matengenezo kwa muda mrefu pale nafasi inapopatikana na tutawajulisha wateja kuwa yanafanyika.

Na ili hali hii izidi kuboreka na iwe ya kudumu, Shirika linaendelea na ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ambalo limefikia asilimia 80.22 hadi kufikia tarehe 31 Disemba 2022.

TANESCO wanasema kuwa ongezeko la urefu wa kina cha maji katika bwawa hilo jipya unaridhisha.

Kina cha maji katika bwawa la Nyerere kwa sasa umefikia mita 126.12 kutoka usawa wa bahari.

Shirika la Umeme nchini kwa sasa pia limeanza kutekeleza miradi ya vituo vipya vya kutumia gesi na umeme jadidifu.