Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Wanyamapori sasa ni tishio kubwa dhidi ya Maisha ya wakazi wa wilaya ya Karatu

Madiwani kutoka kata zote za halmashauri wilaya ya Karatu, wamuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Karia Magaro kuchukua hatua za haraka dhidi ya matukio ya wakazi wa maeneo yao kuvamiwa na kuuawa na wanyamapori.

Madiwani hao wamemtaka Mkurugenzi ahakikishe kuwa idara ya wanyamapori inakuwa na vifaa vyote muhimu vya kupambana na wanyama wanaovamia makazi na kuua au kuwajeruhi watu.

Wamedai kuwa kwa miaka mingi, na hadi sasa, wanyamapori, wamekuwa wakivamia maeneo yanayokaliwa na watu na kuharibu mashamba, kula mimea na vile vile kuwashambulia wakazi na kusababisha vifo.

Sasa katika kikao chao cha Baraza la Madiwani, wawakilishi hao wa wananchi wamewasilisha kero hiyo na kutaka usuluhishi wa haraka.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Karatu, John Lucian amesema kuwa idara ya wanyamapori kwa sasa haina silaha za moto kwa ajili ya ajili ya kuzuia wanyama wakali wanaovamia makazi, mashamba na maeneo mengine ya shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Lucian, watumishi wa Idara ya wanyamapori pia hawana nyenzo za usafiri kama magari au hata pikipiki kuwawezesha kufika maeneo ya tukio kwa wakati.

Hivyo basi, Baraza la Madiwani limemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu kufuatilia kwa karibu suala la upatikanaji wa Bunduki iliyolipiwa kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita ili wakazi wa eneo hilo waweze kuishgi kwa amani bila hofu ya kushambuliwa na wanyama wakali wakati wowote.

Matukio ya wanyama wakali kuwashambulia na kuua wakazi wa maeneo yanayopakana na msitu wa nyanda za juu kaskazini unaotenganisha mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na maeneo ya Mbulumbulu yamekuwa yakiongezeka.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa halmashauri, maeneo mengi ya karatu yamepakana na hifadhi za Manyara na Ngorongoro yanayosimamiwa na NCAA pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na visa vya watu kuuawa na wanyama kama Tembo, Nyati (Mbogo) au Chui sasa vimekuwa ni vya kawaida sana.

“Ni muhimu sasa kwa mkurugenzi kufuatilia suala la silaha pamoja na usafiri kwa ajili ya idara ya wanyamapori la sivyo kila siku kutakuwa na misiba, vilio na uharibifu wa mali za wananchi,” alisema.

“Nimekuwa nikihudhuria mazishi ya waliouawa na Tembo au Mbogo Sasa inatia Hadi aibu Kama mwenyekiti wa halmashauri kuona watu wakiuawa, bila sisi kuchukua hatua yeyote,” aliongeza.

“Kwa hiyo Mkurugenzi tunakuagiza chukua hatua za haraka ili idara hiyo ipate Bunduki. Imefika muda sasa wakazi wa maeneo haya waanze kuona juhudi za serikali kujitokeza kuwasaidia pale wanapopata matatizo,” alisema John.

Pia wamemwagiza mkurugenzi kutafuta muafaka wa mashamba ya mkataba ambayo yamegeuka kuwa mapori na kwamba wanyama wakali hujificha humo.

Taarifa zinasema kuwa kuna mashamba kadhaa ya mikataba ambayo mengi yametelekezwa wilayani karatu na kugeuka kuwa vichaka vya kutisha, vikihifadhi wanyama wakali wa kila aina, wakiwemo hadi nyoka.

Inadaiwa kuwawamiliki wa mashamba hayo ni wajeuri na wamekuwa wakitoa maneno ya kejeli kwa viongozi kuwa maeneo hayo ni yao na hayawahusu watu wasiohusika hivyo wayaache yalivyo.

“Tunaomba Mkurugenzi uchukue hatua za haraka ili mapori yaliyoibuka katika mashamba hayo yafyekwe na mashamba kusafishwa ili kuokoa maisha ya wananchi.”

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Karatu, Karia Magaro amesema kuwa suala la Bunduki tayari liko mikononi mwa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

“Tayari Halmashauri imekamilisha hatua zote za wilaya kuhusu upatikanaji wa silaha,” alisema.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo ameahidi kufuatilia tena kwa Karibu ili waweze kupewa majibu kuhusu hatua iliyofikiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Kuhusu suala la usafiri kwa watumishi wa idara ya wanyamapori, Mkurugenzi Magaro amesema kuwa kutokana na uhaba wa magari katika Halmshauri amelazimika kuomba msaada wa gari kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

“Pale inapotokea kuwa kuna tukio la dharura la wanyama kuvamia maeneo ya makazi, tutalazimika kuomba msaada wa gari au magari kutoka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, hili pia nalifuatilia kwa karibu!”