Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Utapeli Mpya waibukia kwenye Miamala ya Benki

Kuna aina mpya ya udanganyifu ulioibuka mwaka huu 2023 unaohusisha miamala ya benki, hususan kupitia fedha zinazotumwa kutoka nje ya nchi kwa mfumo wa SWIFT.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Benki kuu ya Tanzania (BOT), taasisi hiyo ya fedha imetoa tahadhari juu ya Kuongezeka kwa udanganyifu wa miamala ya kwenye akaunti za watu mbalimbali.

“Benki Kuu ya Tanzania imebaini kuongezeka kwa udanganyifu wa fedha nchini unaohusisha mwananchi kupokea taarifa(hati au barua pepe) inayodai kuwa ni uthibitisho wa malipo kupitia SWIFT,” Taarifa ya BOT inabainisha.

Kwa Mujibu wa Benki Kuu, udanganyifu huo pia unatumika katika mifumo mingine ya uhamishaji fedha.

Inaelezwa kuwa Mpokeaji anafahamishwa kuwa fedha zimeingizwa kwenye benki au akaunti katika taasisi ya fedha nchini Tanzania.

Pia wakati mwingine, mpokeaji fedha anaelekezwa kulipa kiasi fulani cha fedha kuwezesha kupata fedha hizo nyingi.

Matukio mengi ya taarifa hizo yanahusisha kiasi kikubwa cha pesa kinachodaiwa kuletwa kwa ajili ya ufadhili wa mradi au matumizi binafsi.

“Kutokana na hali hiyo, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kwamba taarifa hizo ni za kughushi na za kubuni.”

BOT imewashauri wananchi pamoja na watumiaji wa huduma za benki kwa ujumla kuwa waangalifu na kuacha kujihusisha na miamala hiyo ambayo kwa kawaida inalenga kuwatapeli fedha.

“Pia, wananchi mnakumbushwa kuzingatia kanuni bora za kufanya miamala ya fedha ili kuepuka upotevu wa fedha ambazo ni pamoja na Kuhakikisha usalama wa taarifa za fedha wakati wa kutoa taarifa binafsi mtandaoni (tovuti, mitandao ya kijamii).”

Wananchi pia wametahadharishwa kutojihusisha kujibu barua pepe, barua au simu zinazoahidi kupokea fedha kutoka kwa watu au kampuni wasizozifahamu vizuri.

Sambamba na hayo watu wote wanashauriwa kuwa waangalifu mnapofanya malipo ya mtandaoni kwa kufanya uhakiki wa mshirika wa kibiashara (mtu au kampuni) kabla ya kutoa maelezo au kufanya malipo.

Aidha, wananchi wote ambao huenda tayari wametapeliwa au kukumbwa na matatizo hayo kwa namna yeyote ile wanashauriwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama kwa ajili ya kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa.