Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Wakazi wa Mara waiburuza Barrick Gold Mahakamani Nchini Canada

Watanzania wapatao 21 wameuburuza uongozi wa mgodi wa North Mara na wamiliki wake Barrick Gold mahakamani, nchini Canada.

Raia hao wa Tanzania waliojitambulisha kama wananchi kutoka jamii ya Wakuria, mkoani Mara, wamefungua kesi hiyo dhidi ya Kampuni ya Madini ya Barrick Gold katika Mahakama Kuu ya Ontario (Superior Court).

Watanzania hao wanawakilishwa na kampuni mbili za wanasheria za Canada, yaani Camp Fiorante Matthews Mogerman LLP pamoja na Waddell Phillips.

Katika kesi hiyo, wananchi hao kutoka jamii ya Wakurya nchini Tanzania, wanaituhumu Kampuni ya Barrick Gold ya Canada kwa vitendo vya kikatili na uhalifu dhidi ya wakazi wa Mkoa wa Mara.

Katika suala hilo la kisheria, wananchi hao wameanisha makossa kadhaa ya ukatili dhidi yao pamoja na uvunjifu wa haki za kibinadamu.

Jalada lao limejumuisha matukio ya kufukuzwa na kufyatuliwa risasi hovyo hali inayowafanya watu wa maeneo hayo waishi kwa uwoga na kukosa amani muda wote.

Pia kuna vitendo vya mauaji ya kutisha, watu kujeruhiwa vibaya, tena kwa makusudi na mateso makali wanayoyapata raia wasio na hatia wanaokamatwa wakipita karibu na migodi hiyo ya Barrick.

Mgodi wa North Mara

Hii inakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Makampuni ya Canada, kuburuzwa mahakamani kwa kosa ambalo taasisi au Kampuni ya nchi hiyo imelitenda nje ya mipaka, kwa wenyeji wa eneo ambalo kampuni husika imewekeza.

Watanzania hao wanadai kuwa vitendo hivyo vya kikatili hutekelezwa na uongozi wa Mgodi wa North Mara kwa kushirikiana na askari polisi.

Siku chache zilizopita, taasisi ya haki za binadamu ya Raid ya Uingereza ilitoa ripoti ya hali ya mateso katika machimbo yaliyopo barani Afrika.

Katika ripoti hiyo, Raid waliandika kuwa mgodi wa North Mara ni miongoni mwa maeneo hatari.

Ripoti ya Raid ilidai kuwa Zaidi ya watu 77 wamepoteza maisha huku wengine 304 wakijeruhiwa vibaya sana ndani ya mgodi pamoja na maeneo yanayouzunguka North Mara Barrick Gold.

Inadaiwa kuwa matukio mengi yalianza mwaka 2006 baada ya Kampuni ya Barrick Gold kuchukua migodi hiyo ya North Mara.

Kampuni inadaiwa kuajiri askari 150 chini ya mkataba maalum na Jeshi la Polisi, Tanzania.