Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Safari ya Mji wa Mbulu kuwa Kitovu Cha Michezo Mkoani Manyara Yaanza na Ukarabati wa Viwanja

Wakazi wa Mji wa Mbulu katika moja ya mikutano ya hadhara

Iliwahi kuwa chimbuko la wanariadha mahiri nchini, na sasa Wilaya ya Mbulu kupitia Halmashauri ya Mji wa Mbulu inajifua kuwa kituo muhimu cha michezo yote mkoani Manyara.

Na katika kutekeleza azma hiyo Halmashauri ya mji wa Mbulu imeanza kuvikarabati viwanja kadhaa vya michezo katika mkakati wa kuifanya wilaya hiyo kuwa ni kituo maalumu cha michezo.

Kwa mujibu wa Ofisa michezo wa halmsahauri ya mji wa Mbulu, Benson Maneno  viwanja vinavyokarabatiwa ni pamoja na kile cha michezo Mbulu mjini na kilichopo kwenye shule ya sekondari Chief Sarwat.

Benson Maneno: Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Mkoani Manyara

Shule ya sekondari ya chief Sarwat ni miongoni mwa shule 56 teule nchini zilizoteuliwa kuwa vituo maalumu kwa ajili ya kukuza michezo kwa wanafunzi pamoja na vijana.

Hivi karibuni Chief Sarwatt ilikuwa miongoni mwa shule zilizoteuliwa na serikali kushiriki mafunzo maalum ya michezo yaliyoendeshwa na Baraza la michezo Tanzania kupitia wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Yalifanyika pia kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) huku yakijumuisha zaidi ya washiriki 60 wengi wakiwa ni waalimu kutoka Shule 56 Tanzania.

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wa Jinsi ya Kuendesha Michezo Katika shule hizo.

Afisa michezo wa  mji wa Mbulu, Benson Maneno anafafanua zaidi kwamba wao waliwakilishwa na mwalimu Vicent Yahaya ambae ndiye watashirikiana naye katika kujenga uwezo wa vijana wa Wilaya hiyo kwenye michezo.

Mwalimu Yahaya atahakikisha kuwa maelekezo yote juu ya kuzingatia michezo kwa kuibua vipaji  shuleni yanazingazitwa na kwa sasa tayari tumeanza kukarabati miundombinu ya viwanja.

“Sisi kama Mbulu maelekezo yote kutoka kwa mwalimu huyu katika  shule yetu ya sekondari ya Chief Sarwat tumeyapokea na tunaahidi kuyatekeleza katika kuwaibua vijana wenye vipaji kutoka katika michezo mbalimbali.” Anaongeza Benson Maneno.

Mmoja wa walimu hao  waliopatiwa mafunzo hayo kutoka shule ya sekondari ya Chief Sarwat iliyopo Mbulu, yaani Vincent Yahaya  alisema mafunzo hayo yalikuwa kwa ajili ya kutambua vipaji vya vijana katika kuvilea ili kuboresha michezo shuleni.

“Tumepata mafunzo na tumeelewa  vizuri  jinsi ya kutambua vipaji  katika shule zetu na kuwawezesha  wanafunzi wenye  vipaji kukua katika mazingira ya kimichezo hivyo tunaimani yale yote tuliyojifunza  taifa  lijiandae kupokea vijana ambao watakuwa wamenolewa vilivyo na watakaokuwa na vipaji .” Anafafanua Mwalimu Yahaya.

Aliongeza kuwa katika shule hiyo  vipaji vitanolewa na taifa litarudisha hadhi ya michezo.