Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Sakata la Mauaji ya Polisi Loliondo: Watuhumiwa 24 Waachiwa Huru Arusha

baadhi ya akina mama na watoto wakiwa njia panda kufuatia vurugu za mwezi Juni 2022

Mahakama ya hakimu mkazi Arusha imewaachia huru watuhumiwa 24 kutoka tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro ambao walikuwa anakabiliwa na Kesi ya Mauaji.

Mingoni mwa watuhumiwa hao ambao ni wakazi wa kijiji cha Ololosokwan, ni pamoja na madiwani tisa.

Raia hao 24 wakiwemo viongozi wao tisa walikamatwa mwezi Juni, 2022 baada ya fujo kuzuka katika tarafa ya loliondo na kusababisha kifo cha askari polisi na majeruhi kadhaa.

Hata hivyo wakati Mahakama ikipanga kusikiliza kesi hiyo ya mauaji namba 11/2022, jijini Arusha, ikaletwa taarifa kwamba serikali haikuwa na nia ya kuendelea nayo tena.

Wakili wa Serikali Upendo Shemkole aliieleza mahakama kuwa mkurugenzi wa mashitaka nchini (DPP) hakuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo tena.

Wakili huyo aliieleza mahakama kuwa wanaiondoa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Hakimu Mkazi Herieth Mhenga, aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo aliwaachia huru washitakiwa hao 24 ambao ni wanavijiji 15 na madiwani 9.

Ikumbukwe kuwa Wananchi hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambalo ni kupanga njama ya mauaji na kuua ambapo inadaiwa kuwa walifanya makosa hayo mnamo June 10, 2022.

Katika kipindi hicho kwenye eneo la Serie, kijijini Ololosokwani katika tarafa ya Loliondo, Askari Polisi Koplo Garlus Mwita alipoteza maisha wakati vurugu zilipoibuka wilayani Ngorongoro.

Ilikuwa ni katika zoezi la kuweka alama za mipaka kuzunga eneo lakilometa za mraba 1500 ambalo baadae lilifanywa kuwa pori tengefu la Pololeti.

Mawakili upande wa utetezi nao wameeleza furaha yao baada ya tamko hilo kwani ni jambo walilokuwa wakilisubiri kwa muda mrefu.

Wanasheria hao pia wamesema kuwa  wapo tayari kushirikiana na washtakiwa ikiwa watahitaji kufungua kesi ya madai dhidi ya  serikali ili kudai fidia ya mateso waliyoyapata kwa kipindi chote walichokuwa gerezani.

Nao wananchi na viongozi waliokuwa wakistakiwa katika kesi hiyo wameeleza furaha yao baada ya kuachiwa huku wakimshukuru mungu na kueleza kuwa wako salama