Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Sakata la Kampuni ya Vasso: Mahakama ya Rufaa yazuia kuuzwa kwa shamba lililoajiri watu 1000

Kibosho, Moshi.

Zaidi ya wafanyakazi 1000 wa shamba la maua  na viungo mkoani Kilimanjaro  wamehakikishiwa usalama wa ajira zao  baada ya mahakama ya rufaa kuzuia kuuzwa kwa kampuni yao.

Kwa mujibu wa wakili wa kampuni hiyo ya Vasso Agroventures Limited, Elias Ngereza ambaye alifafanua kuwa mahakama ya rufaa imetoa agizo maalumu kuwa shughuli zote za shambani hapo pamoja na shughuli za kusindika mazao kwa ajili ya kusafirisha nje ziendelee kama kawaida.

“Tunawahakikishia wafanyakazi wa hapa wameajiriwa takribani takribani 1000  ajira yao itakuwa salama,ajira yao itaendelea na wataendelea kulipwa mishahara yao mwisho wa mwezi kama kawaida maana kampuni inaendelea kama kawaida,” alisema Wakili Ngereza.

Alieleza kuwa Agizo hilo la mahakama ya rufaa lina maana kuwa kila kitu kitaendelea kama kilivyokuwa.

Wakili Ngereza amesema kuwa waliotaka kuuza shamba ni viongozi wa zamani wa kampouni hiyo ambao ni wageni walijiandaa kulipiga mnada ili warudi kwao ulaya.

Akizungumzia sakata hilo mkurugenzi wa kampuni ya Vasso Agroventure Limited, Alphonsus Nijenhuis, alisema kuna baadhi ya raia wa kigeni waliingilia kati kutaka kuuza shamba na mali za kampuni hiyo kwa madai kuwa wana haki nalo hadi kulazimika kupeleka suala hilo mahakamani.

“Hata hapa tulipo tulikuwa mbioni kutoa ajira zingine 1000 hususani kwa wanawake na malengo ya baadae ni kuongeza wafanyakazi zaidi ya elfu nne baada ya kuwapa wakazi wa eneo hili mafunzo ya kilimo na usindikaji wa mazao…”

“… Kwa hiyo madai ya kuwa shamba lilikuwa linafilisika sio ya kweli,”aliongeza Nijenhuis.

Kampuni yake imekuwa ikipeleka mazao ya kilimo, yaani mbegu za mboga, viungo, maharage pamoja na maua katika nchi kadhaa barani ulaya pamoja na Thailand na kwa Zaidi ya miaka 20, shamba hilo limekuwa kiungo muhimu kwa uchumi wa eneo la Kibosho, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Prisca Massawe amesema kuwa wamepata tetesi kuwa shamba lao lilikuwa linafungwa na habari hizo ziliwastua sana lakini sasa wamefarijika baada ya uongozi wa kampuni kuwahakikishia kuwa shughuli zinaendelea.

“Hata hivyo tunaiomba serikali ihakikisha kuwa watu wanaotaka kulihujumu shamba wanachukuliwa hatua kwa sababu kampuni hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa na ajira kwa sisi wanawake,” alisema Prisca.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari