Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Burigi-Chato yatumia Bilioni 3.3 kujenga barabara, madaraja na Kambi za Watalii Hifadhini

Hifadhi ya Taifa ya Burigi -Chato imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 3.3 kuimarisha Miundombinu ndani ya hifadhi ili kuvutia watalii ambao sasa wameanza kutembelea hifadhi hiyo mpya kwa wingi.

Burigi-Chato ni moja ya hifadhi za hivi karibuni zilizoanzishwa mwaka 2019 na kufanya idadi ya hifadhi zote nchini kuwa 21.

Akizungumza na waandishi wa habari, wilayani Biharamulo, Mkuu wa hifadhi ya Burigi-Chato, Kamishna Msaidizi Ismaili Omari alisema Maboresho ya Miundombinu ya hifadhi ni jitihada zinazofanywa na Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA ).

“Ni moja ya hatua zinazochukuliwa kuhakikisha kuwa barabara na miundombinu mingine katika hifadhi hii ya Burigi Chato inakuwa katika kiwango cha ubora kwa ajili kurahisisha safari za wageni ili hifadhi iweze kusaidi serikali kufikia malengo iliyojiwekea ya kupokea watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025,” aliongeza mhifadhi huyo.

Kwa mujibu wa Omar hadi kufikia Februari 2024 barabara zenye urefu wa kilomita 97.5 zimekwisha kujengwa hifadhini hapo. Na miundombinu mingine ni pamoja na madaraja na vivuko katika maeneo ya mito.

Vile vile Burigi-Chato imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa kambi kadhaa za Utalii na maeneo ya makazi ya bei nafuu kwa ajili ya watanzania wanaotaka kufanya utalii bila kulazimika kutumia gharama kubwa.

“Tumejenga barabara zinapitika wakati wote lakini pia madaraja na kuna minara ya Mawasiliano ambayo imejengwa ndani ya hifadhi hivyo imekuwa tofauti na miaka ya nyuma sasa Watalii wanaweza kuwasiliana kwa uzuri wakiwa ndani ya hifadhi”alisema

Naye Afisa Utalii katika hifadhi ya Burigi-Chato, Aldo Mduge alisema upekee wa hifadhi hiyo ni uwepo wa ndege aina ya Domo Kiatu (African Shoebill), vyanzo vya maji na maziwa yanayo zunguka hifadhi, aina nyingi za wanyama pamoja na jamii za ndege zipatazo 400.

Kwa upande wake Kaimu mkuu idara ya utalii hifadhi  hiyo, Emmanuel Nyundo alisema uwekezaji walio ufanya ikiwemo kujenga kambi ya wageni ya kudumu huku  akiwakaribisha   wageni kuwekeza Burigi kwani kuna maeneo mazuri.

Burigi-Chato  ina kilomita za mraba 4,707 na eneo la hifadhi limepita katika wilaya za Biharamulo, Chato, Karagwe, Ngara na Muleba ambayo imo ndani ya mikoa ya Kagera na Geita.

Hifadhi hii mpya pia imezungukwa na maziwa matano yaliyopo ndani ya hifadhi ikiwemo ziwa burigi, sehemu ya ziwa victoria, Ziwa Ngoma, ziwa kasinga , pamoja na ziwa Nyamarebe