Habari, Utamaduni, Historia na Simulizi za Tanzania na Afrika Mashariki

Miaka 40 tangu kufariki wa Edward Moringe Sokoine: Watanzania wanamkumbuka waziri huyo mkuu wa zamani

Maandalizi kwa ajili ya ibada maalum ya kumbukumbu ya miaka 40 tangu kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine yameanza rasmi kijijini kwake Monduli-Juu.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza tukio maalum ya kuadhimisha miaka 40 tangu kifo cha kiongozi huyo ambaye pia alikuwa ni mbunge wa kwanza wa jimbo la Monduli, enzi hizo likijumuisha na wilaya ya Longido.

Awali msemaji wa familia, Lembris Kipuyo alisema kuwa viongozi wengine kutoka serikalini na hata nje ya Tanzania wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo la kumbukumbu ya Hayati Sokoine siku ya Ijumaa ya tarehe 12, April 2024.

Rais wa awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete yeye alihudhuria na kuongoza tukio la kuadhimisha miaka 30 ya kifo cha Sokoine mwaka 2014, ambapo serikali yake ilimjengea mjane wa kiongozi huyo nyumba mpya.

Na wakati kuadhimisha miaka 20 tangu kifo cha Sokoine, mnamo mwaka 2004, mawaziri wakuu wa zamani, wakiwemo Salim Ahmed Salim, Joseph Sinde Warioba na aliyekuwa waziri mkuu kipindi hicho, Frederick Sumaye walihudhuria ibada hiyo rasmi.

Hadi anafariki, Hayati Sokoine alimiliki nyumba moja ndogo, kule Monduli na hakuwa na gari.

Rais wa awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ndiye aliyenunua gari kwa ajili ya familia ya Sokoine katika miaka ya 90.

Sokoine, aliyekuwa ni kiongozi kutoka jamii ya kifugaji, hususan kabila maarufu la Wamasai katika Ukoo wa Mollel, alizaliwa mwaka 1938.

Edward Sokoine (Kulia) na Mwalimu Nyerere

Kiongozi huyo alifariki dunia mwaka 1984 katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Dakawa wilayani Morogoro.

Gari lake aina ya Mercedes Benz, lilipamiwa na gari jingine aina ya Toyota Land-Cruiser lililokuwa katika mwendo mkali likiendeshwa na Dumisan Dube aliyekuwa mpigania uhuru wa Afrika Kusini, enzi hizo kambi yao ikiwa Morogoro.

Hiyo ilikuwa ni mwaka mmoja tu baada ya kuteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu mwaka 1983 ambapo alisikika sana kwenye operesheni dhidi ya wahujumu uchumi nchini.

Awali Sokoine alishika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya awamu ya kwanza chini ya Rais Julius Nyerere.

Nafasi alizotumika ni pamoja na unaibu waziri, Waziri wa Nchi, Waziri wa Ulinzi na ile ya Uwaziri Mkuu kuanzia mwaka 1977 hadi alipojiuzulu mwaka 1980.

Mara baada ya kifo chake mwaka 1984, nafasi ya waziri mkuu ilichukuliwa na Salim Ahmed Salim.

Sokoine aliacha wake wawili pamoja na watoto 11. Mmoja wao, Namelok Sokoine amejiingiza katika shughuli za siasa.

Watanzania wamkumbuka

Hata baada ya miongo minne tangu aondoke duniani, watanzania wengi bado wanamkumbuka waziri mkuu huyo wa zamani akiwemo Jacob Timothy, aliyesoma naye Monduli, ambaye anasema Sokoine alikuwa ‘Mtu Serious’ tangu wakiwa shuleni.

Rashid Gutta, mtaalamu wa Kilimo ambaye sasa amestaafu anasema kiwango cha uadilifu alichoonesha Sokoine enzi za uhai wake pengine kisiweze kufikiwa na mtu mwingine kwa haraka.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari