Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Shirika la Nyumba lajenga Makazi Mapya 560 eneo la Kawe Tangayika Packers

Eneo la Tanganyika Packers ambako mara nyingi Mtume Boniface Mwamposa huendesha ibada za maombezi, panajengwa majengo mapya 560 kwa ajili ya makazi na tayari nyumba zaidi ya 320 katika eneo hilo, zimekwisha kupata wanunuzi.

Serikali, kupitia Shirika la Nyumba la Taifa, imeanza kutekeleza ujenzi wa nyumba za makazi zipatazo 5000 katika majiji ya Dar-es-salaam, Dodoma na maeneo mengine nchini, mradi unaokadiriwa kugharimu shilingi Bilioni 466.

Na hadi kufikia mwisho wa wiki ya kwanza ya Januari 2023, nyumba 321 zinazojengwa eneo la Kawe zimepata wanunuzi, huku ujenzi wa majengo mengine 560 ukiendelea kutekelezwa jijini.

Muungano Saguya ni Meneja wa Idara ya Mawasiliano ya Umma katika Makao Makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Meneja huyo anafafanua kuwa shirika linatekeleza ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kupitia mradi maalum wa Samia Housing Scheme.

 “Tunatarajia kujenga nyumba zipatazo 5000, na nusu ya hizo zitakuwa jijini Dar-es-salaam, asilimia 30 zingine zitajengwa Dodoma na asilimia 20 zilizobaki zitasimamishwa katika miji mingine mikubwa ya Tanzania Bara,” anaongeza Saguya.

Kwa Mujibu wa msemaji wa shirika la nyumba lengo la mradi wa Samia Housing Scheme, ni kuwawezesha watanzania walio wengi kumiliki makazi bora kwa gharama nafuu. Pia nyumba hizo hujengwa kwa ukubwa tofauti kulingana na mahitaji binafsi ya wanunuzi husika.

Awali Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), lilijiwekea malengo ya kujenga nyumba 400 za makazi zenye ukubwa tofauti jijini Dar-es-salaam.

Hata hivyo, kutokana na uhitaji mkubwa uliojitokeza, ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakizilipia nyumba hizo hata kabla ya ujenzi kukamilika, shirika lililazimika kuongeza idadi hiyo, hadi kufikia nyumba Zaidi ya 560 zinazoendelea kujengwa muda huu.

Na shirika limekuwa likiuza nyumba hizo mpya zilizopo eneo la Kawe, Tanganyika Packers, jijini Dar-es-salaam, kwa wastani wa nyumba 37 kwa wiki, tangu mwezi Novemba mwaka 2022 hadi wiki ya pili ya Januari 2023.

Saguya anasema kuwa watanzania wengi wameonesha shauku ya kununua nyumba hizo na shirika linaendelea kutoa ofa maalum ya punguzo la bei, itakayodumu kwa miaka saba hadi mwaka 2030.

Wakati huo huo, zaidi ya makampuni 66 ya ndani na nje ya nchi yamejitokeza kuomba kuingia ubia na Shrika la Nyumba la Taifa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kadhaa ya ujenzi wa kisasa nchini.

Unaweza pia kuisoma habari hii katika lugha ya KIINGEREZA