Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Spika Tulia Ackson Apendekezwa kuwania Urais wa Umoja wa Mabunge ya nchi 189 Duniani

Afrika imempendekeza Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson, kuliwakilisha bara zima katika kinyang’anyiro cha Urais wa Jumuiya ya Mabunge yote 189 Duniani.

Spika Tulia amepitishwa jukwaa la mabunge ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kugombea nafasi ya Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani(IPU).

Uchaguzi wa Urais wa IPU unatarajiwa kufanyika Tarehe 27 Oktoba 2023, jijini Luanda nchini nchini Angola.

Awali Dakta Tulia Ackson alikuwa tayari amependekezwa kugombea nafasi hiyo kubwa duniani na Bunge la Umoja wa Afrika (PAP) pamoja na Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA) na vile vile nchi yake ya Tanzania.

Mbunge kutoka jimbo la Gauteng, Afrika ya Kusini, Darren Bergman ndiye aliwasilisha hoja katika kikao cha Bunge la SADC kutaka nchi hizo wanachama wa Jumuiya, kumuunga mkono Tulia Ackson katika Urais wa Umoja Mabunge Duniani.

Bergman aliungwa mkono na Mbunge wa Angola, Pedro Sebastio katika kikao cha 53 cha jukwaa la mabunge ya Jumuiya ya Maendelo ya Kusini Mwa Afrika, kilichokuwa kinafanyika jijini Arusha, Tanzania.

Bergman ametoa hoja ya  kupitishwa Dk Tulia  kuwania nafasi hiyo, kwa mujibu kwa  kanuni ya 26(4) ya utaratibu katika bunge hilo na pia kutokana na uwezo mkubwa wan chi ya Tanzania katika masuala ya kimataifa.

Alisema amewasilisha hoja ya kupata mgombea mmoja kutoka SADC, licha ya kuwepo wagombea wengine walioonesha nia kugombea nafasi hiyo kutoka  Afrika.

Wagombea hao  ni Catherine Gotan Hara wa nchini Malawi na Jacob Fransis Nzwidamilimo Mudenda wa Zimbabwe  na Adji Diarra Megane Kanoutee wa mbunge kutoka Senegal.

Bergman alisema ili kuonesha Umoja katika kuwania nafasi hiyo,ni vyema kumpitisha Dk Tulia Spika wa Bunge la Tanzania, kutokana na sifa  alizonazo kuwa mgombea wa SADC katika uchaguzi huo.

Alisema ili kuhakikisha ushindi unapatikana  alipendekeza Mabunge ya SADC kuunda timu ya kampeni ya wabunge sita kutokana kanda  za Afrika ili kurahisha kampeni na kuhakikisha mgombea huyo wa SADC anashinda nafasi hiyo.

Hoja ya Mbunge huyo wa Afrika Kusini, iliungwa mkono na wabunge wengine kutoka Zambia, Zimbabwe Lesotho na Namibia.

Wote walieleza kwa kuwa kwa muda mrefu nafasi hiyo, imekuwa ikishikwa na wabunge wanaume kumpitisha Dk Tulia ambaye ni msomi na kijana kuwania nafasi hiyo ushindi utapatikana.

“Tunaunga mkono hoja hii na ninawaomba wabunge wenzangu tuunge mkono,ili kuonesha umoja na mshikano ndani ya SADC hasa kuwa na mgombea mwanamke kijana,” walisema kwa pamoja.

Akizungumza baada ya kutolewa hoja hiyo, Rais wa Bunge la SADC, Roger Mancienne alitoa fursa ya wabunge kuchangia hoja hiyo, ambapo wabunge kutoka nchi za Zimbabwe, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho, Zambia, Eswatini, Namibia, Afrika Kusini, Mauritania walieleza kumuunga mkono Dk Tulia.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchaguliwa kuwania nafasi hiyo, Dk Tulia aliwapongeza wabunge wote kwa kumpitisha na kuwania nafasi hiyo ya kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani.

Alisema heshma aliyopewa ni kubwa kwani kuteuliwa kugombea nafasi hiyo katika bunge hilo lililoanzishwa tangu mwaka 1889 hadi sasa likiwa na wawakilishi wa mabunge 179 duniani.

Dk Tulia alisema, miongoni mwa mambo ambayo akichaguliwa atasimamia ni kuhakikisha mabunge yanakuwa na uwakilishi wa makundi maalum katika jamii, ikiwepo wenye ulemavu na wanawake na vijana.

“Lakini pia kwa kuzingatia sheria na kanuni za bunge hilo nitajitahidi kutoa demokrasia pana zaidi katika uendeshwaji wa bunge la Dunia”alisema.

Dk.Tulia amekuwa ni Mbunge wa kwanza Tanzania, kuteuliwa kugombea nafasi hiyo ya Urais wa Umoja wa Mabunge Duniani.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari