Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Black Mamba: Jitu la Kutisha Katika Vita Dhidi ya Idd Amin

Wakati wa vita ya Kagera, kulikuwa na Brigedi namba 207 ambayo ndiyo hasa ilikuwa ya kwanza kuusogelea mstari wa adui , hii iliongozwa na askari aliyetisha akijulikana kama ‘Black Mamba.’

Jina lake halisi hasa ni Meja Jenerali Walden.

Kwa Usiku mitatu, wa vita vya Kagera Meja Jenerali Walden alipita katika maji na matope ambayo yalikuwa ni hatari kabisa kwa kuwa kulikuwa na mamba wengi.

Baada ya kufanikiwa kupenya, wanajeshi wengine walishambulia Mamba hao na kumfikia. Hapo alipata jina Black Mamba kwa Ujasiri wake!

Katika eneo la Masaka, vita vilikuwa vikali sana kiasi kwamba, Idi Amin alimtuma Luteni Kanali Abdu Kisuule kutuliza ‘mambo’, Lakini haikufaa kitu.

Baadae wakapata msaada wa wanajeshi elfu moja toka Libya lakini Jeshi la Tanzania lilikuwa imara chini ya Black Mamba.

Black Mamba alikuwa ni Bingwa wa shabaha, alikuwa na mbinu imara za kupigana kwenye hali ngumu na misituni.

Baada ya Mapambano hayo, Luteni Kanali Kisuule alikuja kukiri kwamba mapambano ya eneo la Masaka ndio hasa yalidhoofisha jeshi la Uganda, ‘Kama ni kushindwa vita tulishindwa pale Masaka’.

Baadae ‘Black Mamba’ aliongoza jeshi la Tanzania kuvamia makazi ya Nduli Idd Amin jijini Kampala.

Black Mamba ni nani?

John Walden alizaliwa Tunduru, Kusini mwa Tanzania mwaka 1939.

Baba yake alikuwa ni Mwingereza na Mkuu wa wilaya ya Tunduru kwa wakati huo Bwana Stanley Arthur Walden, Mama yake alikuwa ni mtanzania Violet Nambela.

Akiwa na miaka mitatu tu, John na Bibi yake upande wa Mama walihamia Mbeya.

Wakati vita vya pili vilipomalizika mwaka 1945, John aliungana na baba yake mzee Stanley Walden ambaye alikuwa amehamishiwa Njombe, Iringa.

John Walden alisoma shule ya Msingi ya bweni TosaMaganga, alihitimu darasa la kumi mwaka 1956. Mwaka ulifuatia yaani 1957 alijiunga na jeshi la kikoloni The King’s African Rifles (KAR).

Ndani ya Jeshi, alikuwa kijana mchangamfu na ambaye alikuwa mwepesi kujifunza. Alikuwa ni mtunza ‘stoo’, mpiganaji, mara nyingine karani na hata ukalimani pale ilipohitajika.

Baada ya uhuru, John Walden alikutana na vikwazo vingi kwani alikuwa wa uzao wa ‘baba mzungu’. Kwa wakati huo, wazungu wote hata wale ‘machotara’ walionekana wakoloni tu.

Alivumilia ubaguzi wote jeshini, alikuwa mtu mcheshi na mara nyingi wanajeshi wengine ‘weusi’ walisahau kuwa Walden alikuwa ‘Mweupe’.

Uwezo wake wa kulenga shabaha, kugundua aina ya silaha kwa sauti na mbinu za kivita zilimfanya akubalike Zaidi.

Kati ya mwaka 1962 na 1963 alihudhuria mafunzo maalumu katika shule ya kijeshi ya Aldershot, Uingereza. Mwaka 1963, Mwalimu Nyerere alimwapisha kuwa luteni, pamoja na luteni mwingine mzawa ‘Elisha Kavana’.

Baadae aliteuliwa kuwa mkuu wa kambi ya JKT Mafinga, kwenye miaka ya 1970 aliongoza operesheni za kijeshi kusini mwa Afrika, Kusaidia kuzikomboa nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Angola.

Vita vya kagera, Walden au Black Mamba alikuwa kati ya makomandoo wachache walioteuliwa kufanya jaribio la kuiteka Kampala. Walden aliongoza kikosi kilichovamia makazi ya Iddi Amin.

Na walifanikiwa kupata tuzo na nyaraka kadhaa ndani ya chumba alichokuwa analala Idd Amin.

Baada ya vita vya Kagera, wengi waliamini angeteuliwa kuwa mkuu wa majeshi ya Ulinzi, Lakini haikuwa hivyo! Siha yake ya uchangamfu iliendelea kama kawaida, alikuwa ni mtu mzalendo, aliyejitoa kwa ajili ya nchi sio vyeo na sifa.

Aliitwa miaka ya 1989 kuongoza operasheni maalumu dhidi majangili waliokuwa wakishambulia wanyama hasa Tembo, Kazi hiyo aliifanya kwa ufanisi mkubwa. Iliitwa operesheni UHAI, nyakati za usiku alitembea nyikani kwa ujasiri na kikundi cha askari wanyama pori.

Kazi hiyo ilipunguza mno matukio ya kuuliwa kwa tembo.

Meja jenerali John Butler Walden au Black Mamba alifariki Julai 7, 2002. Na kuzikwa Mbeya.

Huyu ndio ‘Black Mamba’, Komandoo hodari wa operasheni za misituni na mlenga shabaha ambaye hajapata kutokea katika Historia ya Jeshi la Tanzania.