Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Nyanda Nyasele: Sehemu Takatifu kwa Wangoni Iliyoharibiwa na Wazungu

Wajerumani baada ya kufaulu kuangamiza mahali patakatifu palipotumiwa na Wangoni kiimani, NYANDA NYASELE, eneo la Maposeni, walijenga ngome yao kwa mtindo wa Kijerumani.

Ni baada ya kupata misukosuko kule Pugu. 

Zamani zile kutoka Buguruni hadi kufika Ukonga palikuwa pori tu.

Wazungu walipotafuta eneo jingine ili wasikazane pale St. Joseph Cathedral, Posta-Kivukoni, walienda hadi eneo moja na kupata hifadhi kwa kupokelewa na mtu aliyejulikana kama JUMBE UKONGA.

Pengine hawakutarajia kwamba wangelipata hifadhi kwa kuwa walilazimika kupita porini ili wasikutane na Waarabu.

Katika shukran yao ya kumuenzi Jumbe Ukonga, eneo walilopata hifadhi ambapo ni kwa Jumbe Ukonga walijenga kanisa kubwa lenye umbo la mwamvuli.

Umbo la mwamvuli wakimaanisha kuwa ni hifadhi waliyopewa na Jumbe Ukonga ili kuwakinga na matatizo mbalimbali hasa ya Kijiografia na kisasa wakati huo.

Basi hata eneo lile likatwa UKONGA hadi sasa.  Kanisa hilo liko jirani na Hospitali ya Kardinali Laureano Rugambwa, Ukonga-Madafu.

Sasa turudi Peramiho. Kabla ya kufika Peramiho, hapo Ukonga walisonga mbele hadi Pugu. Leo Pugu ni moja ya maeneo yanayotembelewa na wengi.

Haikuwa rahisi kupata eneo Kusini mwa Tanganyika (sasa Tanzania).

Baada ya mvutano wa muda mrefu hatimaye mahali patakatifu palipotumiwa na Wangoni kiimani, NYANDA NYASELE, eneo la Maposeni paliharibiwa vibaya na Wazungu.

Ingawaje Wangoni kwa miaka mingi walitamba kwa nguvu za kijeshi upande wa Kusini hata kuwaburuza Wahehe vibaya na pia kuwaburuza Wasokasoka kando ya ziwa Nyasa jirani na Msumbiji, hatimaye Wangoni walizidiwa nguvu na Wazungu.

Lakini baadae mapambano ya kudai uhuru yakaibuka. Ndipo wakipojitikeza watu kama “Jenerali” Kinjeketile Ngwale wa Matumbi na wengine wengi.

Habari za Wajerumani hao kusini ni nyingi mno.

Pamoja na kibano wakichowapa wenyeji na kutaabika kwa wenyeji, kwa kufikiri chanya wazungu hao wametoa mchango wao katika maeneo mbalimbali ya maisha ya binadamu; afya, elimu, imani, na mengine mengi.

Leo Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Joseph Peramiho ni moja ya Hospitali muhimu sana Kusini mwa Tanzania. Katika Mkoa wa Ruvuma Wazungu hao waliokuja kwa namna mbaya wameifanya sekta ya afya kuwa ya kutiliwa maanani na wenyeji.

Peramiho

Kuna hospitali ya Peramiho, Litembo, Lituhi na vituo vingine vya afya.

Hawakuishia hapo tu. Katika sekta elimu pia leo pana shule nyingi huko. Wangoni washindwe wenyewe tu! Pia, Seminari Kuu ya Peramiho ni moja ya vituo vikubwa Afrika vinavyotoa elimu ya Theolojia.

Shule ya Sekondari ya Kigonsera ni mfano mmojawapo pia.

Peramiho sasa ni eneo la kitalii. Limetunzwa na bado linaunzwa vema na kubaki na muonekano wake tangu lilipoanza kutumika miaka mingi iliyopita.

Waafrika wengi kwa nje ya mioyo yao wanalalamika sana kuhusu ukoloni ulivyokuwa, ni kweli taabu zilikuwa nyingi bila kutarajiwa; hata hivyo ndani ya mioyo yao Waafrika hao hao kimyakimya tu mioyoni mwao pengine wanaona ahueni fulani iliyoletwa na ukoloni.

Lakini kwa kuwa wanaangalia upande mmoja tu hasa wa kisiasa basi mengine hayaonekani. Hakuna anayefurahia shida na mshike mshike wa ukoloni, hata hivyo yapo mengine mazuri yamefanywa nao.

Yapo maeneo mengine pia mbali na Peramiho ambayo yamesanifiwa kwa muonekano wa mtindo wa zamani wa ujenzi huko Ujerumani. Peramiho ni urithi wa kikoloni wenye kuvutia wengi.

Peramiho ni mahali panapofaa kwa ajili ya Hija kwa watu wa imani husika. Nimeandika kwa kifupi tu. Kwa urefu zaidi ni siku nyingine na kwa mtindo mwingine pia.

Habari Zingine
Tuachie majibu

Anwani yako ya Email haitaonekana