Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Wasifu wa Siti Binti Saad: Muimbaji wa kwanza kurekodi Muziki Chini ya Jangwa la Sahara

MTUMWA

Siti binti Saad alizaliwa katika kijiji cha Fumba, Zanzibari mwaka 1880.

Alipozaliwa alipewa jina la ‘Mtumwa’ hii ni kwa vile alizaliwa katika kipindi cha utumwa.

Baba yake bwana Saadi alikuwa ni Mnyamwezi kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga, lakini wote wawili walizaliwa Zanzibari.

Hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana na walijishughulisha zaidi katika shughuli za kilimo na ufinyanzi kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.

Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji.

Kipaji hiki kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake kwani alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza.

Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali wa masafa marefu na hii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo.

Wengi walisema kuwa Siti alikuwa na mapafu yenye nguvu kama ya simba kutokana na jinsi alivyoweza kupaza sauti yake mbali na bila kuachia pumzi.

Kutokana na wakati huo elimu kwa watoto wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Qur’an. 

JOGOO LA SHAMBA NA MSASA WA NADI IKHWANI

Mwaka 1911 aliona ni bora ahamie mjini ili kubooresha maisha yake zaidi.

Ujio wake wa mjini ulikuwa wa neema kwani alikutana na bwana mmoja wa kundi la muziki wa Taarabu la “Nadi Ikhwani Safaa” aliyeitwa Muhsin Ali Maarufu kwa jina la “Oud”

Katika kipindi hicho Nadi Ikhwaan Safaa ndilo lilikuwa kundi pekee la muziki wa taarabu Mjini Zanzibar, Kundi hili lilikuwa ni la wanaume pekee , wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni.

Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Siti na hivyo akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki na lugha ya kiarabu.

Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa “Nadi Ikhwani Safaa” ambao bila kusita wakaanza kufanya naye maonyesho mbalimbali katika jamii. 

Walipata mialiko mingi hasa kutoka kwa Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia walialikwa katika maharusi na sherehe zingine mbalimbali. Inasemekana ulifika wakati ambapo sherehe ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo kutumbuiza.

MKATABA ULIOWEKA REKODI.

Siti alikuwa ni moto wa kuotea mbali na jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la Afrika kwa Kipaji chake Maridhwawa cha Utunzi na Uimbaji.

Punde Siti alianza kufananishwa na ‘Umm Kulthum’, mwimbaji mahiri mwengine wa kike aliyetamba wakati huo kutoka Misri.

Mwaka 1928 kampuni ya kurekodi muziki ya ‘Columbia and His Master’s voice’ yenye makazi yake Bombay (Sasa Mumbai) nchini India ilisikia umaarufu wa Siti binti Saadi na hivyo ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili kujaribu kama muziki wake kama utauzika.

Kampuni ile haikuweza kuamini jinsi muziki ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo, na hadi kufikia 1931 santuri 72,000 zilikuwa zimeuzwa.

Kutokana na kusambaa kwa santuri hizi, umaarufu wa Siti ulizidi maradufu na watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakija Zanzibari kuja kumwona.

STUDIO, WIVU NA VIJIBA VYA ROHO.

Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua kujenga studio ya kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti binti Saadi.

Hatua hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza wengi wenye wivu, hivyo wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumshusha hadhi yake na hasa wakitumia kigezo kwamba hana uzuri wa sura, nyimbo nyingi zilitungwa na kuimbwa dhidi yake lakini huu ndio uliovuma sana:-

Siti binti Saadi kawa mtu lini?,

Kaja mjini na kaniki chini?,

Kama si sauti angekula nini?.

Na yeye kwa kujua hila za wabaya wake, akaona isiwe taabu akajibu shambulio namna hii:-

Si hoja uzuri,

Na sura jamali,

Kuwa mtukufu,

Na jadi kebeli,

Hasara ya mtu,

Kukosa akili.

SITI ALIISHI NA JAMII, ALITUNGA NA KUIIMBIA JAMII.

Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna yake aliwafunga midomo wale wote waliokuwa wakifumatafuata.

Siti pia alikuwa ni mwanamke wa kwanza mwanaharakati katika kipindi chake, alitetea wanawake na wanyonge kwa ujumla, kwani katika kipindi chake watu matajiri walikuwa wakiwaonea masikini na walipofikishwa mbele ya haki waliweza kutoa hongo na kuachiwa huru halafu wewe uliyeshitaki ndiye unayefungwa.

Utunzi wake wa wimbo wa Kijiti ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta mwanamke mmoja mgeni kutoka bara, mwanamke huyu alipofika visiwani alikutana na Tajiri mmoja ambaye alijifanya amempenda, hivyo akamchukua na kulala naye halafu baadaye akamuua.

Tajiri yule alishitakiwa na bahati nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile, lakini kwa vile ni Tajiri alitoa pesa na kesi ikawageukia wale mashahidi na kufungwa.

Siti akatoa wimbo huu :-

Tazameni tazameni,

Eti alofanya Kijiti,

Kumchukua mgeni,

Kumcheza foliti,

Kenda naye maguguni,

Kamrejesha maiti.

SITI NA UKUZAJI TAARAB, UENDELEZAJI SANAA NA KISWAHILI.

Siti bint Saad (1928) ndiye nyota wa kwanza wa taarab ambaye kwa mara ya kwanza badala ya kuimba kwa Kiarabu aliimba kwa Kiswahili.

Alifyatua mamia ya santuri za nyimbo na wapenda muziki wa enzi hizo hakuna aliyekosa wimbo wake nyumbani.

Mazoea ya Wasanii wengi wa wakati huo ilikuwa ni kuimba Nyimbo za kukopi za wasanii wa nje au hata kuimba kwa lugha za kigeni(aidha kiarabu au kiingereza), lakini kitendo cha Siti Bint Saad kuimba kwa Lugha ya Kiswahili kiliamsha ari ya wasanii wengi kuimba kwa lugha zao za asili na huo ndio ukawa mwanzo wa wasanii mbalimbali kuimba kwa lugha ya kiswahili.

Muziki wa taarab asili hauna tofauti na ‘Classical Music’ wa Ulaya au ‘Country Music’ wa Marekani.

Miziki hiyo ilikuwepo, imekuwepo na itakuwepo bila kubadilika wala kuitwa kwa jina jingine wala kupigwa kwa namna nyingine tofauti na ilivyokuwa, ilivyo sasa na itakavyokuwa kesho.

Ni sehemu ya kudumu ya utamduni wa watu na sio kitu cha kupita na kusahaulika.

Aina hizo za miziki pamoja na kuzuka kwa miziki ya kila aina Ulaya na Marekani bado inatambulika kwa nembo na jina lake.

Country ni country na classical ni classical. Hapajakuwapo muziki mwingine uliopewa umodern kuhusiana na miziki hii, hakuna kitu kama modern country au modern classic.

Rouget katika Music and Trance anafafanua kwamba neno taarabu linatokana na neno la kiarabu ‘tariba’ likiwa na maana ya hisia za kusisimka, kudhihirisha au kutaka kufanya kitu Fulani, kama vile kuimba au kucheza taarab.

Mchango wa Siti kwenye kuasisi Matumizi ya Lugha ya Kiswahili kwenye Muziki huu wa Mwambao ni Mkubwa na Usiomithilika, kitendo chake hicho kilishajiisha Uandikaji wa Mashairi ya Kiswahili kwa kasi kubwa mno na kuchochea Matumizi makuu ya Lugha husika kwa kazi za Sanaa. 

Siti ameelezwa kuwa msanii si katika kuimba tu bali pia aliendeleza fani ya utunzi kwa kutunga nyimbo kadhaa.

Nyimbo za Siti ziliwavutia wasikilizaji mbalimbali kwa sababu ziliweza kugusa sehemu na nafasi mbalimbali za jamii.

Aligusia nyimbo za mapenzi (kama wimbo wake “Sahibu mwandani”), zinazowagusa wanyonge, watawala na pia kufichua matukio maovu yaliyokuwa yakitendeka (kama wimbo wake wa “Kijiti”) na pia kupambana na wale waliondelea kumdharau na kumpiga vita (kama nyimbo zake “Nauliwani, Kigalawa”). 

Katika fasihi simulizi kwenye michezo ya watoto kuna baadhi ya Nyimbo zinazotumika zilikua ni sehemu ya nyimbo za Siti (kama nyimbo zake “Mtoto mnara, Hakuna gogo pumbavu”). Siti aliweza kuendeleza fani hii ya uimbaji kwa kujiweka na kuhifadhi akiwa mwanamke mwenye heshima yake wakati wote.

Maisha binafsi ya Siti Bint Saad ni kioo kinachomweleza Siti na wAanawake wengi Wachapakazi wa Tanzania.

Moyo wa kujidhatiti katika kujifunza na msukumo kutoka kwa mwalimu wake kuliimarisha juhudi yake katika kufikia mafanikio. Ustahamilivu wake ni mfano bora wa mwanamke katika kupata maendeleo.

Aliweza kuendeleza kazi yake na kutunza heshima yake bila ya kujali maneno ya kuvunja moyo. Wasifu wake ni fumbo kwa kejeli aliyokuwa akifanyiwa, na mafanikio yake yalikomfikisha.

Alitoka katika tabaka la chini bali alithaminika kutokana na ujuzi wake. Siti aliweza kueneza utamaduni na Ustaarabu wa taarabu katika Afrika Mashariki, nchi za Bara Hindi na Arabuni.

Siti alijifunza zaidi katika safari hizo na pia alijifunza mengi alipokutana na mwimbaji maarufu wa Misri, Ummukulthum.

Kazi zilihifadhika kwa kujitokeza waliosaidia kuweka kumbukumbu za rikodi za nyimbo zake kwenye santuri.

Siti Bint Saad ni Makutaa yanayotoa taswira ya mwanamke wa Afrika ya Mashriki aliyepata mafanikio kwa juhudi za kujifunza kwa taabu.

Ni kitabu kinachotoa mafunzo na kueleza kuwa bidii inahitajika katika kufikia ufanisi. Pia moyo wa kujitolea aliokua nao Siti umeweza kuweka alama katika historia ya fani taarabu Afrika Mashariki.

Ni kitabu kinachohitaji kusomwa katika kuongeza ujuzi katika sanaa ya taarabu na kujifunza kuwa mafaniko hupatikana kwa mbinu, juhudi na kujidhatiti.

SITI BINT SAAD, MWANAMKE WA CHUMA WA ZAMA ZAKE.

Historia yake imemchora Bibi Siti kwa kueleza tabia yake ya kukabiliana na matatizo yake tokea utotoni kwake.

Siti hakuwahi kupata elimu ya madrasa wala ya skuli bali alipata kujifunza na kushiriki katika kazi za kijijini kwake ikiwemo kazi ya ufinyanzi.

Alionyesha heshima kwa jamii yake na aliishi nje ya kijiji chake pale alipokua katika ndoa na kurudi kijijini kuendelea kuishi kwao ndoa yake ilipovunjika. Siti hakuacha kujitafutia njia ya kujikimu alipokuwa katika hatua mbalimbali za maisha yake.

Alipokuwa kijijini alikuwa akifinyanga vyungu na kuuza hata walivyofinyanga wengine. Hasara aliyoipata katika kazi hii ya kuanguka na kuvunjika vyungu vyote ilimtia Siti katika mtihani mwingine.

Aliendelea kukaa kijijini na baadae aliolewa tena na kwenda kuishi mjini. Ndipo, Siti alipoanza kupata kujifunza kuimba.

Kwa shauku aliyokua nayo aliweza kuanza kazi hiyo bila ya kusubiri mume wake ambaye alikuwa kasafiri. Baada ya mume wake kurudi na kupata tetesi ya maisha ya mke wake wakati aliposafiri kulipelekea kuvunjika kwa ndoa hiyo.

Haya alipambana nayo na kupiga moyo konde na kujidhatiti katika kuimarisha lengo lake.

Historia ya Siti inaleta mvuto kwa kuonyesha uimara wake katika matendo yake. Aliweza kufunzwa kuimba wakati hakujua kusoma wala kuandika Kiarabu wala Kiswahili, lugha kuu ambazo zilifundishwa katika visiwa vya Zanzibar wakati huo.

Kwanza alifundishwa kusoma Kurani na alifaulu kupata lafudhi nzuri ya Kiarabu.

Kutokana na kipaji chake cha kuwa na moyo mwepesi wa kuhifadhi na kupata lafudhi nzuri, Siti alinyanyukia kuwa mwimbaji bora katika Kiswahili, Kiarabu hata na nyimbo za Kihindi.

VITA PANDE ZOTE, UHODARI NI KUJIFUNGA KIBWEBWE.

Siti alibaki katika kufikia mafanikio yake licha ya kuendelea kusemwa maneno dhidi yake hasa ya kukiuka utamaduni wa mwanamke wa wakati wake na kujiweka mjini kwa kushirikiana na wanaume katika kuimba, pia alipata kejeli za watu wa mjini kumuona yeye anatoka shamba – atayawezaje ya mjini.

Siti alijidhatii kuendelea na kazi yake na chini ya uongozi wa mwalimu wake alipata moyo wa kuendelea mpaka kufikia siku ya kutokeza hadharani.

Naandika maandiko haya kwa kutoa msukumo wa kuvutia katika kueleza kwake na kutaka kufuatilia zaidi maisha ya Siti ambayo mafanikio yake hayakupatikana kwa urahisi.

Mbali na juhudi aliyoichukua katika kujifunza na uhodari aliokuwa nao, mkosi ulimfika siku yake ya kwanza katika kuonesha ubingwa wake wa kuimba, sauti kamwe haikutoka! Wapinzani wake walipata kuendeleza bezo juu yake na kufikiri kweli Siti hatoweza kupambana na mambo ya mjini.

Kitendo hicho kilimvunja moyo lakini hakukata tamaa. Juhudi yake ya kuanza tena kwa mbinu mpya ndio ikawa mwanzo wa kufanikiwa kwa Siti katika uimbaji wa taarabu.

Ikawa Siti anapoimba washabiki waliongezeka siku hata siku; hivyo Siti aliweza kustawisha uwanja huu wa taarabu ambao mpaka leo ni maarufu katika Zanzibar na mwambao wa Afrika ya Mashariki.

SHAABAN ROBERT NA WASIFU WA SITI USIOMITHILIKA.

Siti aliendelea na shughuli yake ya muziki hadi uzeeni, muda mfupi kabla ya kifo chake alikutana na mwandishi maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert ambaye alimhoji na kuweza kuandika wasifu wake katika kitabu alichokiita ” Wasifu wa Siti binti Saadi”.

Wasifu huu unaonekana kuwa ndio “bora zaidi” uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hiki kimewahi kutumika kufundishia shule za sekondari za Tanzania.

Pia Mwandishi Nasra M. Hilal (Aliyetunga Kitabu “Mfinyanzi Aingia Kasri – Siti Binti Saad, Malkia wa Taarab”) amekiri kuwa amepata mengi kwa mwandishi Shaaban Robert, gwiji wa Kiswahili.

Kuna tafauti kubwa kati ya vitabu viwili hivyo, kimoja kimetungwa mwaka 1967 na kingine kimetungwa mwaka 2007.

Tarehe 8 Julai, 1950 Siti binti Saadi alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu.

Ingawa pengo hilo haliwezi kuzibika lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa kuimba taarabu kupitia kwake, mfano hai ni Bi Kidude

Hata baada ya kifo chake jina lake bado linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake, Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA), kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao “Sauti ya Siti”.

Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa Taarabu. Na anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika mashariki kurekodi muziki katika santuri.