Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Mfalme Charles III na Siri ya Mti wa Mkuyu katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha

Mwaka 2023, hasa Mwezi Mei ndio Mfalme mpya wa Uingereza alitawadhwa rasmi kushika wadhifa huo mkubwa katika nchi hiyo tajiri barani ulaya.

Lakini kipindi ambacho Mfalme Charles III akiapishwa jijili London, Askari pekee mtanzania aliyeandamana na kiongozi huyo wakati wa ziara yake nchini Tanzania mwaka 2011 alijitokeza na kutoboa siri iliyojificha kwa Zaidi ya miaka 12.

Huyo ni Askari mwandamizi wa uhifadhi Michael Ngatoluwa ambaye alifunguka kuhusu jambo la ajabu aliloliona kwa kiongozi huyo, enzi hizo akijulikana kama ‘Mwana wa Mfalme,’ (Prince of Wales) wakati akimuongoza ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha, iliyopo chini ya Mlima Meru.

Ngatoluwa alisema kuwa Mfalme Charles alipofika hifadhini novemba 9, 2011 alichagua kufanya utalii wa kutembea kwa miguu pamoja na kuwa alivaa suti nyeupe.

“Mfalme Charles na mkewe Malkia Camila walibahatika kuwaona wanyama mbali mbali kama Twiga, Tembo, Nyati, Mbega lakini kilichomvutia Zaidi ni kitu tofauti kabisa na matarajio yetu,” alisema Askari huyo.

Alisema kuwa kwa kawaida watalii wengi wanaokuja kutembelea hifadhi zote za Tanzania wanapendelea zaidi kuona wanyama mbali mbali na ndege au maporomoko ya maji.

“Lakini cha ajabu ni kwamba Mfalme Charles alivutiwa zaidi na mti mkubwa aina ya Mkuyu ulioko katika maporomoko ya maji ya Tululusia na kuomba kupiga picha ya pamoja katika eneo hilo kabla ya kuendelea na safari yake ya kutalii ndani ya hifadhi,” alisema Askari Mhifadhi Ngatoluwa.

Mti huo mkubwa wa Mkuyu upo hatua chache kutoka eneo la Maporomoko ya Maji ambako Mfalme Charles III alilitembelea mchana huo.

 “Mfalme Charles alioneshwa kushangazwa na ukubwa wa mti huo wa Mkuyu ambapo alilazimika kusimama na kuanza kuuliza maswali kuuhusu huku akidai kuwa nchini kwao Uingereza miti kama hiyo huwa inaoteshwa katika bustani za watu binafsi majumbani au mashambani lakini kamwe huwa haijawahi kufikia ukubwa wa kutisha kama huo mkuyu wa Arusha,” aliongeza.

Mfalme Charles III akiushangaa Mkuyu

Lakini wengi wamekuwa wakijiuliza, je ni Ukubwa tu wa Mkuyu ndio ulimshangaza Mfalme Charles III au kuna siri nyingine iliyojificha?

Ngatolua alisema kuwa msafara wa Mfalme Charles uliokuwa na magari matano pekee ulianza utalii majira ya saa tano asubuhi na kumalizika saa saba au nane za mchana.

Maeneo yote waliyoyatembelea hifadhi hapo hakuna lililomvutia Charles na Mkewe Camilla kama huo Mkuyu.

Akizungumzia ziara ya kitalii ya mfalme Charles ndani ya hifadhi ya Arusha, Kamishna msaidizi wa hifadhi, Yustina Kiwango alisema kufuatia tukio hilo wanatarajia kuweka kibao maalum cha kumbukumbu katika eneo hilo.

“Ni tukio lililotushangaza na katika kuhifadhi kumbukumbu hii maalum tunatarajia kuweka kibao kikubwa katika eneo ambalo Mfalme alisimama kwa muda mrefu kujifunza kuhusu miti ya mikuyu,” alisema Mhifadhi Kiwango, akiongeza kuwa si ajabu kunaweka kukaibuka utalii mpya wa watu kufika hifadhini hapo kwa ajili ya kujionea mikuyu mikubwa.

Mfalme Charles III aliapishwa rasmi tarehe 6 mwezi Mei 2023 Katika Kasri ya Saint James jijini London Uingereza.

Anamrithi Mama yake, Malkia Elizabeth II aliyefariki mwishoni mwa Mwaka 2022.

Charles anakuwa Mfalme Mpya wa Uingereza baada ya Miaka Zaidi ya 70.

Mama yake, yaani Malkia Elizabeth II alipata alirithi uongozi wa kifalme wan chi hiyo wakati alipokuwa ziarani nchini Kenya mwaka 1952.

Lakini je. Kuna siri gani kati ya Mkuyu wa Arusha na Jumba la Mfalme la Uingereza?

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari