Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Historia kuhusu miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania

Mwezi Agosti 2023, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania lilifanya sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya KKKT.

Hata hivyo Dhehebu hilo la Kikristo ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini limekuwepo Tanzania kwa miaka mingi zaidi tangu enzi za Tanganyika na utawala wa Ujerumani.

Kwa mujibu wa maelezo rasmi kutoka Makao makuu ya kanisa hilo jijini Arusha, KKKT limekuwepo Tanzania kwa miaka mingi lakini maaadhimisho ya Miaka 60 yaliyofanyika katika chuo kikuu cha Tumaini, Makumira yalikuwa ni miongo sita ya muungano wa mishenari kadhaa zilizokuwa zikifanya kazi nchini.

“Ni kweli KKKT tunasherekea Miaka 60 lakini hiyo haimaanishi kuwa ndio Kanisa lilianza kipindihicho,” inafafanua taarifa hiyo.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Kilutheri au Evangelical Lutheran Church in Tanzania (ELCT) ni matokeo muungano wa misheni mbalimbali za kilutheri zilizoingia nchini tangu mwaka 1887.

Misheni ya Kwanza kuja Tanzania ni Chama Cha ‘Mision ya Berlin III,’ Kutoka nchini Ujeruman mwaka 1887, na kituo chao kikuu kikiwa katika eneo la kigamboni, Mzizima (Dar-es-salaam).

Chama Cha pili kuingia nchini ni ‘Berlin Mission I’ na hiki pia kilikuwa ni Kutoka Ujerumani.

Berlin Mission 1 kiliingia nchini kupitia Afrika Kusini mwaka 1891. Wahusika wa misheni hii walikwenda kuanzisha Dayosisi ya konde.

Baadae tena mwaka 1893 kiliingia Chama Kingine kutoka German, kikiitwa ‘Misioni ya Leipzig,’ nacho kikaanza kazi ya utume maeneo ya Kaskazini na kambi yao ikiwa katika eneo la Kidia, Moshi, Kilimanjaro.

Moja ya makanisa ya awali ya Lutheran, eneo la Mamba Kilimanjaro

Hawa Leipzigi mwaka 1910 walifunga safari kuelekea Rwanda na wakiwa njiani walipitia Bukoba (Kagera) ambako walifungua kituo kingine cha umishenari.

 Baada ya hapo, vyama vingine viliendelea kuingia nchini safari kutoka maeneo mengine ya bara la Ulaya na Marekani.

Misheni hizi mpya hasa zilianza kueneza injili baada ya vita vya kwanza vya dunia (1914-1918) na Vita vya Pili au WWII (1939-1945)

Kutoka na vyama vyote vile Kufika maeneo mbalimbali kukawa na makanisa kila eneo walipofikia

Mwaka 1938 makanisa saba ya Kilutheri yaliungana na kutengeneza ‘Muungano wa Makanisa ya Kiluheri Tanzania,’ au Tangayika Lutheran Churches Federation.

Na ilipofika Tarehe 19 Juni 1963 Muungano huo ulizaa Kanisa moja, ambalo linajulikana kama ‘Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.’

Baada ya KKKT kuanzishwa Kanisa la Ubena-Konde (eneo la Nyanda za Juu Kusini) likaitwa Dayosisi ya Kusini.

Kanisa la Uzaramo-Uluguru likaitwa Dayosisi Mashariki na Pwani.

Kanisa la Usambara-Digo likaitwa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Kanisa la Kaskazini likaitwa Dayosisiya Kaskazini.

Kanisa la Mbulu likaitwa Dayosisi ya Mbulu.

Kanisa la Iramba Turu likaitwa Dayosisi ya Kati na Kanisa la Kaskazini Magharibi likaitwa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.