Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Iringa yamaliza tatizo la wananchi kupachikiwa bili kubwa za maji kinyume na matumizi yao

Matumizi ya dira za maji za malipo kabla zimetajwa kuwa suluhisho la malalamiko ya wananchi kubabikiziwa ankara na mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira nchini.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) Mhandisi David Palangyo, alibainisha hayo jana jijini hapo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo.

Alisema, hadi sasa mamlaka hiyo imefunga dira za malipo ya maji kabla kwa wateja na taasisi mbalimbali zaidi ya 6,700 ambazo zimesaidia kupunguza malalamiko kwa wateja.

“Tangu kuanza kufunga mita hizi za maji mwaka 2015 kumekuwa na mafanikio makubwa sana tumefanikiwa kupunguza malalamiko ya wateja kubambikiziwa ankara za malipo ya maji pia tumepunguza malimbikizo ya madeni kwa wateja wetu wakiwemo wadaiwa sugu” alisema

Aidha, alisema hadi sasa mamlaka hiyo inadai zaidi ya Shilingi bilioni mbili kwa wateja wadogo ikiwa ni sehemu ya deni lililokuwepo kabla ya kufungwa kwa dira za malipo ya maji kabla.

“Taasisi zote za serikali tumewafungia dira hizi hivyo kusaidia kuondokana na changamoto za kudai madeni ya malipo ya ankara kama ambavyo maeneo mengine wamaekuwa na changamoto hizo”alisema Palangyo

Kadhalika, alisema lengo la mamlaka hiyo ni kuwafungia dira hizo wateja wote ambao wanatumia huduma ya mamlaka hiyo ili kupunguza malalamiko na kuongeza mapato ya ili waweze kujiendesha bila kutegemea fedha za serikali.

Vile vile, alisema hadi sasa huduma ya maji safi katika mji wa Iringa imewafikiwa wananchi kwa zaidi ya asilimia 97 na mikakati ya kuwafikia wananchi wote inaendelea.

“Tunaishukuru sana serikali yetu ya awamu ya sita kwa kutupatia fedha ambapo hivi sasa tunatekeleza miradi ya maji inayogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 220” alisema

Pia, alisema pamoja na mafanikio hayo mamlaka hiyo bado inakabiliwa na vikwanzo mbalimbali ikiwemo uharibifu wa mazingira unaosababisha ukame na kupungua kina cha maji.

“Uharibifu wa mazingira ikiwemo uendejai shughuli za kibinadamu umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kukauka kwa vyanzo vya maji na kusababisha utoaji wa huduma kuwa wa mgao”alisema

Hata hivyo, alisema mamlaka hiyo inaendelea ni jitihada mbalimbali za kuongeza huduma ya uondoshaji maji taka ambapo hivi sasa imewafikia watu kwa asilimia 6.8.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari