Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Kitambulisho cha Taifa alichopewa Mchina Chazua Maswali

Vitambulisho vya Taifa bado ni kitendawili kwa watanzania walio wengi

Je! Mchina au mtu yeyote kutoka nje ya Tanzania anaweza kupewa Kitambulisho cha Taifa?

Ndilo swali wanalojiuliza watanzania wengi baada ya picha ya nakala ya Kitambulisho cha Taifa chenye jina la mtu kutoka China, kusambaa mitandaoni.

Na picha ya mhusika kwenye hicho kitambulisho, yaani bwana Zhu Jin Feng ikionesha wazi kuwa mmiliki ni mtu kutoka China.

Kitambulisho kinaonesha kuwa tarehe yake ya mwisho kutumika ni May 2026, hii ikimaanisha kuwa kilitolewa mwaka 2016.

Kwa Watanzania wengi, kitambulisho hicho cha Mchina kimewarejeshea kumbukumbu zisizo nzuri za miaka mingi ya mahangaiko ya kujaza fomu na kutembea kutoka ofisi moja hadi nyingine, tena kwa siku au wiki kadhaa bila kufanikiwa.

Hizo zote zikiwa ni juhudi za kupata nakala ya vitambulisho hivyo. Hadi leo Watanzania wengi hawana vitambulisho hivyo na baadhi wakiwa wameambulia namba tu.

Na hivyo wengi waliokuwa wakitoa maoni mitandaoni wanahoji kwa nini iwe rahisi kwa wageni lakini wao wapate ugumu kuwa na “ID” hizo.

Kuna hata wengine waliodai kwamba pengine kitambulisho hicho pia ni “Mchina” yaani bandia kilichotengenezwa kwa ajili ya kufurahisha watu kwenye mitandao.

Mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) imelazimika kutoa ufafanuzi kupitia taarifa rasmi.

NIDA imethibitisha kwamba kitambulisho cha Zhu Jin Feng ni cha ukweli sio cha kutengenezwa mitaani.

Pili Mamlaka hiyo inasema kuwa mhusika, Jin Feng alikipata kihalali. Nakala ya barua ya NIDA hii hapa.

Kwa mujibu wa barua ya NIDA, mhusika, ingawa ana asili ya China, alikwisha kuomba na kupata uraia wa Tanzania.

Taarifa zingine zinasema kuwa Zhu Jin Feng aliyekuja Tanzania tangu 2003 aliomba kupewa uraia mwaka 2012.

Unaweza Pia kuisoma habari hii katika lugha ya Kiingereza

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari