Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Monduli na Mbio za Pikipiki Kuruka Viunzi Nyikani

mbio za pikipiki monduli

Hivi karibuni, Kelvin Gabriel aliibuka mshindi wa mbio za pikipiki za nyika wilayani Monduli.

Ni aina tofauti kidogo ya mchezo wa kutumia vyombo vya moto ambapo waendesha pikipiki huruka viunzi huku wakishindana mbio sambamba.

Na hizi zilizofanyika wilayani Monduli mwaka huu zilishirikisha waendesha pikipiki wapatao 35.

Mashindano hayo yajulikanayo kama ‘Ace of Diamonds Enduro challenge’ yalimshuhudia Gabrieli akishinda kwa kundi la wakimbiaji Bingwa.

Alifuatiwa na Simon Vitalis huku nafasi ya tatu ikimwendea Caleb Simonson.

hizi mbio hazijawahi kuwa kazi rahisi

Akizungumzia ushindi huo Gabriel alisema kiujumla mashindano yalikuwa magumu kwani njia ina changamoto nyinyi hivyo  lazima uwe na mazoezi na pikipiki nzuri kwani vikwazo milima ni mikubwa  .

Kwa upande wa waendeshaji wakongwe au veterans, Muhel Allard alishinda akifuatiwa na  Derek Hurt huku Buddy akishika nafasi ya tatu.

Wakimbiaji wa daraja la kati mshindi alikuwa Diamond Mohammed.

Washindi kwa daraja la chini  alikuwa ni  Jimmy Morrill akifuatiwa na Graham Hurt  huku  Haje Botmen akimaliza nafasi ya tatu.

Haya ni mashindano pekee nchini ya mbio za pikipiki kuruka viunzi ambayo hufanyika kila mwaka wilayani Monduli mkoani Arusha.

Kwa mwaka 2022 mbio hizo ziliandaliwa kumuenzi Baba wa taifa hayati Julius Kambarage Nyerere.

Zilifanyika chini ya udhamini wa Kampuni ya  Double Diamond Holdings Limited kupitia bidhaa zake za vinywaji aina ya ‘Ace of Diamonds’.

Cosmas Joseph ambaye ni meneja  wa Kampuni ya  Double Diamond Holdings Limited alisema wamekuwa wakidhamini kwa msimu wa tatu sasa.

Na aliongeza kuwa katika mashindano hayo wanalenga zaidi vijana wanaopenda kujaribu michezo tofauti.

Double Diamonds wamekuwa wakijikita katika michezo mbalimbali ikiwemo netiboli, riadha na kuongeza kuwa wataendelea pia kudhmanini mashindano hayo ya pikipiki kwa msimu ujao ili kuongeza hamasa zaidi.

“Hivi karibuni tunaenda kudhamini mashindano ya Ndondo Cup kwa mpira wa miguu  ambayo yatafanyika  Arusha  lengo kuibua vipaji kwani tunajua michezo ni ajira  na ni fursa ambayo inajenga mahusiano mazuri kwa watu ,”alisema Joseph.

Katibu wa  chama cha mbio za pikipiki mkoa Arusha, Adam Gunda alisema mashindano yalishirikisha waendesji 34 kutoka  maeneo mbalimbali nchini.