Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Kuhamisha watumishi waharibifu ni kusambaza matatizo katika taasisi na idara za umma

WAZIRI wa nchi, Ofisi ya rais, menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, George Simbachawene ameonya kuhusu utaratibu uliozoeleka wa kuwahamisha watumishi wanaofanya vibaya katika idara au taasisi zao.

“Suala la mtumishi wa umma akiharibu mahali halafu badala ya kumuadhibu, anahamishiwa idara shirika au taasisi nyingine ni kusambaza uharibifu, mtu kama huyo anatakiwa kupewa adhabu,” alisema Waziri Simbachawene.

Waziri huyo alitoa angalizo hilo katika  ufunguzi wa kikao kazi cha wakuu wa idara za utawala na rasilimaliwatu katika wizara, idara zinazojitegemea, wakala, taasisi za umma, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

Kikao hicho kilifanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa Arusha (AICC) ambapo amesisitiza Watumishi kusimama katika misingi ya maadili ya kazi.

Amewataka Watumishi kuwa na Utumishi wenye tija pamoja na utekelezaji wa miundo na mifumo ya uendeshaji na utoaji huduma kwani majukumu hayo ni  makubwa na muhimu katika kuhakikisha taasisi yoyote ya Umma inakuwa na tija kwa Taifa.

Simbachawene amesema Watumishi wanapaswa kuzingatia  umuhimu wa maadili kwani ofisi yake imeendeleea kupokea malalamiko kuhusu vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwemo Rushwa.

Amesema pia ukosefu wa maadili umepelekea watumishi kuwa na lugha zisizofaa, kufanya udanganyifu wa nyaraka ikiwemo kughushi barua za masuala mbalimbali ya kiutumishi kama uhamisho wa kwenda sehemu zenye maslahi mazuri.

“Wote wanao jihusisha na tabia hii kuacha mara moja na hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa wahusika”amesisitiza.

Akizungumzia suala la uhamisho kwa Watumishi amesema kumekuwepo  tabia ya baadhi ya waajiri kukataa kuwapokea watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi hizo na kutoruhusu watumishi kuhama hata pale inapoelekezwa na mamlaka.

Ameesema vitendo hivyo ni kinyume na Sheria, Kanuni na taratibu kwa kuwa kitendo hicho ni kukosa utii  na amewaelekeza waajiri wa aina hii waache tabia hizo.

 “Maadili ni msingi wa utendaji kazi katika Utumishi wa Umma, Utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika ofisi ya wa Umma uliofanywa  mwaka 2022 ulibaini uwepo wa vitendo visivyo vya kiuadilifu katika Utumishi wa Umma ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka kwa manufaa binafsi, mgongano wa kimaslahi na  matumizi mabaya ya mamlaka,”amesema Simbachawene

 “Mtumishi anayeharibu achukuliwe hatua za kinidhamu mahali alipo na siyo kukimbilia kumhamisha na nasisitiza kuendelea kusimamia, kuboresha utendaji na pale ambapo tutabaini mapungufu kuanzia sasa tutachukua hatua stahiki”ameongeza Simbachawene.

Aidha katika hatua nyingine ameeleza kuwa hivi karibuni Serikali kupitia Ofisi yake  ilitoa vibali vya kuwapandisha madaraja watumishi wa Umma 120,210 na kuwabadilisha Kada Watumishi 8,080 na kusema pia Serikali imetoa nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa watumishi wake na itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kulingana na uwezo wa uchumi.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari