Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Wanafunzi elfu moja katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wanufaika kwa misaada ya samani za shule

Zaidi ya wanafunzi 1000 kutoka shule tisa za Arusha na Kilimanjaro wamefanikiwa kupewa misaada ya samani za madarasani na mabweninini vyenye thamani ya shilingi Milioni 108.

Misaada hiyo iliyotolewa na Benki ya NMB, ni pamoja na viti na meza 400, madawati 100 pamoja na vitanda 160 katika shule tatu za msingi, na sita za Sekondari.

NMB imetoa misaada hiyo ikiwa ni katika kuadhimisha  wiki ya huduma kwa wateja duniani iliyoanza octoba 2 na itafikia tamati kesho jumapili octoba 8, 2023.

Shule za Sekondari zilizopata msaada wa viti na meza kwa upande wa Kilimanjaro ni pamoja na Hai day (100), Shirimatunda (100) kutoka Wilaya ya Hai huku Anna Mkapa (50) na Mawenzi (50) zikitokea Same na Sombetini Sekondari (100) kutoka Arusha.

Kwa upande wa vitanda shule ya sekondari Kimala na msingi ya wenye mahitaji maalum ya Same walikabidhiwa vitanda 40 kila kimoja kikiwa na sehemu za juu na chini (double deck) na shule ya msingi Kibaoni walipewa 80 sambamba na shule ya msingi Uhuru walipewa madawati 100.

Akizungumza katika kuhitimisha ziara ya kukabidhi samani hizo, meneja wa NMB kanda ya kaskazini Baraka Ladislaus alisema kuwa lengo ni kurudisha faida wanayoipata kwa jamii katika kuboresha sekta ya Elim na Afya.

“Kutatua changamoto zilizoko kwenye jamii  ni jukumu letu sote kuhakikisha tunamsaidia Rais wetu Samia Suluhu katika kuifikia ndoto ya namna anataka Tanzania iwe katika huduma za kijamii na sisi kama NMB tumejipambanua katika sekta za Afya, Elimu, mazingira lakini pia katika majanga” alisema Baraka

Alisema kuwa misaada hiyo yote yenye thamani ya milioni 107.7 zimetolewa katika ziara maalum ya kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja duniani kwa sekta ya Elim ikiwa ni moja ya kipaumbele Chao.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha uendeshaji na mdhibiti ubora kutoka Benki ya NMB, Salie Mlay alisema kuwa misaada hiyo imetokana na sehemu ya faida waliyoitenga kwa ajili kuhudumia jamii ambayo ni bilioni 6.2.

“Tunatambua juhudi kubwa za serikali chini ya Rais wetu Samia Suluhu za kusimamia upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, na sisi kama wadau tunao wajibu wa kuunga mkono, kusaidia na kuwa mstari wa mbele katika kuchagia utatuzi wa  changamoto zinazojitokeza katika jamii hivyo hatutachoka kuendelea kutoa misaada hii mara kwa mara itakapohitajika, alisema.

Alisema kuwa katika utekelezaji wa kuhakikisha wanaongeza kiasi cha gawio serikali kutoka  shilingi billion 45.5 ya mwaka 2021/2022  Ili kusaidia serikali kutimiza majukum yake kupitia fedha za ndani na kuomba taasisi na mashirika mengine yawaunge mkono.

Kwa niaba ya wakuu wa Wilaya nufaika, mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa alisema kuwa manufaa makubwa wanayoipata kupitia Benki ya NMB, serikali haina cha kuwalipa zaidi ya kuwahakikishia usalama na mazingira rafiki ya kutekeleza majukum yao ya kuikuza taasisi hiyo.

“Haya ni mambo makubwa sana ambayo mnayafanya kuisaidia serikali katika kutatua changamoto za sekta ya Elim, kwanza tunashukuru sana na  sisi cha kuwalipa hatuna zaidi tunawahakikishia ushirikiano, ulinzi na usalama na mazingira ya ufanyaji kazi wenu na msichoke kwani bado tuna mahitaji mengi” alisema. 

Mmoja wa wazazi Wilayani Same, Yusto Mapande aliishukuru kwa misaada hiyo ambayo ingeigharimu serikali lakini pia wananchi katika michango kuwasaidia watoto wao.