Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Kurejea kwa Viongozi wa Upinzani waliokuwa uhamishoni Nchini, Tanzania yaanza kufufuka kisiasa

Ni shamra shamra kubwa katika jiji la Arusha na vitongoji vyake katika tukio la kurejea kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Godbless Jonathan Lema.

Lema anarejea kutoka Canada siku ya kwanza ya mwezi Machi 2023.

Na kwa mwanasiasa huyo ni kwamba ‘Zege Halilali,’ mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, ni moja kwa moja hadi viwanja vya reli ambako kumeandaliwa mkutano mkubwa wa hadhara.

Lema anayetokea nchini Canada alikokuwa uhamishoni kwa zaidi ya miaka mitatu, pia ameandaliwa ziara kadhaa ili kufanya mikutano ya hadhara katika mikoa na wilaya za kanda ya Kaskazini.

Yeye ni wa pili kurejea nchini baada ya kuwasili kwa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA), Wakili Msomi, Tundu Lissu.

Hatua ya wanasiasa hao wa upinzani kurejea nchini inakuja baada ya kuruhusiwa tena kwa shughuli na mikutano ya siasa nchini.

Hii ni baada ya vyama vya upinzania kufungiwa kwa zaidi ya miaka saba sasa, kutokufanya Mikutano ya Hadhara na hata wakati mwingine vikao vya ndani vikiwa vinavamiwa na polisi.

Hivi sasa mikutano ya vyama vya siasa imeruhusiwa kuendelea kufanyika kote nchini.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa mkutano wake na viongozi wa vyama vya siasa, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pia amesema kuwa Serikali yake inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba, uliokwama kwa zaidi ya miaka 8, toka mwaka 2014.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar-es-salaam Rais Samia amesema kuwa Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba.

“Kwa jinsi tutakavokuja kuelewana huko mbele’, wengine wanasema tuanze na katiba ya warioba, wengine tuanze na katiba pendekezwa, lakini kuna mambo ya ulimwengu yamebadilika’, alisema.

Rais Samia ameongeza kuwa itaundwa kamati maalumu kwa ajili kutoa ushauri wa namna ya kwenda kupata katiba.

“Muda si mrefu tutakwenda kuanza na kamati itakayokuja kutushauri, hata hivyo ningependa kusema kuwa katiba hii ni ya watanzania, sio ya vyama vya siasa’,” alisema.

Tanzania iliadhimisha miaka 30 tangu uwepo wa siasa za vyama vingi, July 2022.

Mbali na dai la Katiba mpya, kwa muda mrefu nchini kulikuwa na kilio hasa kutoka kwa wanasiasa na jamii za kimataifa kuhusu haki ya kufanya mikutano ya hadhara, hususan ile ya siasa ambayo ipo kisheria.

‘Hii ni haki kwa sheria zetu, ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara’, uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutangaza, lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka’, alisema.

Mikutano ya siasa ilipigwa marufuku na aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano, John Pombe Magufuli.

Katazo hilo la Magufuli hasa lililenga vyama vikuu vya upinzani hasa kile cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ACT Wazalendo.

Kwa hiyo zuio la mikutano ya hadhara lilionekana kulenga zaidi vyama vya upinzani ambavyo ndio pekee ambavyo havikuruhusiwa kufanya mikutano ya nje na ndani.

Chama Tawala, yaani CCM kiliendela kufurahia uhuru wa kufanya harakati za siasa bila kuzuiliwa.