Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mwaka Mpya 2023: Mama Maria Nyerere Atimiza Miaka 93

Mama Maria (Kulia) akiwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni (Maktaba)

Mke wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mama Maria Nyerere anaingia mwaka 2013 akiwa anatimiza miaka 93 tangu kuzaliwa kwake.

Mama huyo wa Taifa, alizaliwa tarehe 31 Desemba, Mwaka 1930, siku moja kabla ya Mwaka Mpya, kwa mujibu wa mwanaye, Madaraka Nyerere.

Alipozaliwa alipewa jina la Maria na kujulikana kama Maria Waningu Gabriel Magige.

Hii ni kwa sababu Mama Maria alikuwa ni mtoto wa saba kati ya watoto tisa wa Gabriel Magige, wa Baraki, Tarime na mke wake Hannah Nyashiboha.

Maria alisoma katika shule “White Sisters’ School” iliyokuwa Nyegina, na baadae akajiunga na shule ya Ukerewe.

Baada ya masomo ya Msingi na Sekondari, Mama Maria alijiumga na  chuo cha ualimu cha Sumve, chenyewe kikiitwa “Sumve Teacher Training College.”

Alihitimu kwa kupata cheti cha ualimu na katika ajira yake ya awali alianza kufundisha katika Shule ya Msingi Nyegina iliyoko wilayani Musoma mkoani Mara.

Kwa hiyo, Mama Maria alikuwa ni Mwalimu kama ambavyo mumewe, Julius Kambarage Nyerere alivyokuwa Mwalimu na akaendelea kuitwa Mwalimu hata wakati akiwa Rais wa Tanganyika na Baadae Tanzania.

Mama Maria aliolewa na Julius Kambarage Nyerere mwaka 1953, kipindi ambacho Mwalimu amenza harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Muingereza.

Walibahatika kupata watoto saba, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere ambaye awali aliwahi pia kuwa mbunge wa bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Baada ya Uhuru mwaka 1961, Mwalimu Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadae Rais wa Tanganyika na Tanzania hadi alipostaafu Novemba 1985, akimrithisha kiti Rais Ali Hassan Mwinyi.

Mama Maria alienziwa kwa wimbo maalum, ‘Kwaheri Mama Maria Nyerere,’ uliorekodiwa na Bendi ya Maquis Original ukiwa ni utunzi wa Marehemu Fred Ndala Kasheba.

Mumewe, Rais Mstaafu Mwalimu Nyerere alifariki tarehe 14 Oktoba 1999 jijini London, Uingereza alikokuwa amekwenda kwa ajili ya matibabu katika hospitali ya Mtakatifu Thomas.

Mwalimu Nyerere alifariki akiwa na umri wa miaka 77.

Mama Maria kwa sasa ni miongoni mwa wajumbe saba wa baraza la wazee wa “Alliance for Tanzania Youth Economic Empowerment” (Atyee), pamoja na rais wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi na rais wa zamani wa Zanzibar Amani Abeid Karume ambaye alikuwa mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar.