Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Watalii Sasa Wataweza Kucheza Gofu Mbugani wakiwa kwenye Hifadhi ya Serengeti

Mbali na kuitembelea Serengeti kwa ajili ya safari za kujionea vivutio asili pamoja na wanyama pori, sasa watalii wataweza kushiriki michezo ndani ya Mbuga hiyo ya tatu kwa ukubwa nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Jenerali (Mstaafu) George Mwita Waitara ameweka jiwe la msingi katika eneo ambalo hivi karibuni litatumika kama uwanja wa michezo ya Golf.

Gofu ni mchezo ambao hasa unapendwa na matajiri duniani.

Uwanja wa gofu unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Fort Ikoma, wilayani Serengeti, umepewa jina la ‘Serengeti National Park Golf Course.

Jenerali Mstaafu Waitara ambaye pia ni mchezaji mzuri wa Gofu anabainisha kuwa hili ni zao jipya la utalii na kwamba ni moja ya mikakati ya kuhakikisha kuwa Tanzania inapata watalii wasiopungua Milioni 5 ifikapo mwaka 2025.

Tanzania pia imejipanga kuzalisha mapato yatokanayo na shughuli za utalii yaweze kufikia Bilioni 2 kea mwaka.

“Ni Dhahiri kwamba kutokana na umaarufu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti tuna kila sababu ya kuamini kwamba zao hili jipya la utalii litakuwa kivutio kikubwa na chachu ya kuongeza mapato yatokanayo na utalii katika shirika letu na Taifa kwa ujumla” alisema Waitara.

Akifafanua zaidi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo alisema kwamba sehemu ya kwanza ya mradi huo imekamailika ambapo mashimo mawili na sehemu ya mazoezi (range) yamekamilika na kwamba mtandao wa mashimo mengine 16 pia umekamilika.

Aidha, Waitara ametoa wito kwa wawekezaji na wafanyabiashara ya utalii kutambua uwepo wa zao hili, kulitangaza na hatimaye kuleta wachezaji wa golf ambao pia watatalii katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Akizungumza katika taarifa yake juu ya mradi huu, Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilma wa TANAPA amebainisha kuwa mradi huu unatekelezwa na kampuni ya Uwekezaji ya shirika TANAPA INVESTMENT LIMITED ambayo imeanzishwa kwa maelekezo ya Serikali ili kutekeleza shughuli mbalimbali za ujenzi ndani nan je ya Shirika.

Jenerali Mstaafu George Waitara (Kulia) na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema (Kati) katika uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya uwanja maalum wa Gofu Serengeti

“Kukamilika kwa mradi huu kunategemea kuwavutia wacheza golf zaidi ya 3,000 kwa mwaka kutoka ndani nan je na shirikila linatarajia kupata Shilingi billion 2 kwa mwaka.” Alisema Kamishna Mwakilema.

Akiwasilisha salamu za kihandisi, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa wahandisi (ERB), Mhandisi Wakili, Menye Manga aliahidi kufanya kazi kwa karibu na kampuni ya TANAPA Investment Ltd na kupongeza uanzishwaji wa kampuni hiyo ambayo ina wataalam wa kutosha na vifaa vya kutekeleza kazi mbalimbali za kihandisi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha gofu nchini, Gilman Kasiga aliishukuru TANAPA na hasa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kwa kuendeleza michezo nchini hususan mchezo huu wa gofu na kuahidi kuleta mashindano makubwa ya kimataifa katika kiwanja hicho kwani kinakidhi viwango vya kimataifa.

Ujenzi wa uwanja huu wa golf unatarajiwa kugharimu jumla ya shillingi bilioni 7.5 mpaka kitakapokamilika.