Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Moto Kilimanjaro ulivyodhibitiwa Mlimani mwaka 2022 na jinsi ya kujiandaa dhidi ya matukio kama hayo mwaka huu

Mlima Kilimanjaro

Mioto katika Mlima Mrefu Barani Afrika umeuwa ukilipuka mara kwa mara.

Matukio ya hivi karibuni ni pamoja na mlipuko wa 2020 na baadae 2022′

Mara baada ya tukio la mwisho kudhibitiwa, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa, William Mwakilema aliwakilisha taarifa rasmi kuhusu milipuko ya moto Mlima Kilimanjaro na zoezi zima la kukabiliana nayo.

Ripoti

Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ilipokea taarifa ya uwepo wa moto katika bonde la Karanga majira ya saa 02:30 usiku siku ya Ijumaa ya tarehe 21.10.2022.

Taarifa hiyo ilitolewa na mwalimu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kutokana na eneo hilo kuonekana vizuri kutokea maeneo ya chuo.

Juhudi mbalimbali zilifanyika kuhakikisha moto huo unadhibitiwa kwa kushirikisha na wadau mbalimbali waliojitoa kushiriki nasi kuzima moto.

Lilikuwa ni zoezi gumu kutokana na hali ya hewa ya ukanda wa juu kuwa ya upepo mkali ambao ulikuwa unabadilisha mwelekeo wa moto mara kwa mara.

Uwepo wa miinuko mikali na makorongo makubwa pamoja na mlundikano wa mboji ambayo huhifadhi moto kwa muda mrefu iliongeza ugumu wa zoezi hili.

Uoto wa mimea ya asili aina ya “Erica” ambayo inashika moto kwa urahisi na hivyo kusababisha moto kusambaa kwa kasi, ilikuwa sababu nyingine ya kuleta ugumu katika zoezi zima la kudhibiti moto huo.

Taarifa za awali zilibaini kuwa chanzo cha moto ni shughuli za kibinadam.

Hata hivyo kitengo cha usalama cha Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama linaendelea na utafiti ili kubaini wahusika wa tukio hilo.

Jalada la uchunguzi lilifunguliwa kituo cha Polisi Moshi MOS/RB/9563/ 2022 MOS/IR/877/2022.

Shirika litachukua hatua stahiki kwa atakayebainika pasi shaka kuhusika na tukio hilo baada ya uchunguzi kukamilika.

Zoezi la uzimaji wa moto lilianza kufanyika kuanzia tarehe 21 Oktoba 2022 na kuendelea mpaka tarehe 28 Oktoba 2022 ambapo moto uliweza kudhibitiwa katika maeneo mengi korofi.

Hata hivyo, tarehe 29 Oktoba 2022 moto ulilipuka tena katika eneo la korongo la Mto Karanga na kusambaa kuelekea maeneo ya Umbwe na Baranco kutokana upepo mkali uliosababisha kulipua mioto midogo iliyokuwa kwenye magogo na ardhini (kwenye mboji).

Aidha, mpaka tarehe 01/11/2022  kumekuwepo na mafanikio makubwa ya kuudhibiti moto huo ambapo maeneo mengi yalikuwa yamezima kabisa.

Hata hivyo, kutokana na upepo mkali na mrundikano wa mboji ambayo imesababisha kuwepo kwa (underground fire), moto mdogo (inactive fire) umekuwa ukiendelea kulipuka katika sehemu mbalimbali ambapo vikosi viliendelea na udhibiti. 

Jitihada za uzimaji moto zimehusisha vyombo vya usalama nchini ikiwemo Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Jeshi la Uhifadhi na Jeshi la Polisi.

Kulikuwa pia na Jeshi la Zimamoto, Jeshi la akiba, viongozi wa chama na serikali, wananchi pamoja na wadau wakiwemo wamiliki wa makampuni ya utalii (waongoza wageni na wapagazi).

Mbinu mbalimbali zilitumika katika kuzima moto zikiwemo kulinda miundombinu ya utalii dhidi ya moto na kutengeneza kinga ya moto ili kupunguza makali na kuuzima.

Moto wa Ubetu na  Samanga

Usiku wa tarehe 28 Oktoba 2022, moto mpya uliibuka kwenye msitu wa asili katika eneo la Ubetu / Samanga lililoko Wilayani Rombo.

Kikosi cha Askari wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na wananchi wa Rongai walifika kwenye eneo la tukio kwa ajili ya kuukabili.

Moto huu ulithibitiwa kwa siku mbili ambapo kufikia tarehe 30 Oktoba 2022 moto huu ulikuwa umezimwa kabisa. Chanzo cha moto huo pia kinasadikika kuwa ni shughuli za kibinadamu.

Moto wa Mandara karibu na Maundi Crater

Jioni ya tarehe 29 Oktoba 2022, moto mpya uliwaka katika eneo la Mandara- upande wa Marangu.

Moto huu ulikuwa unasambaa kushuka kwenye msitu wa asili.

Hata hivyo kufuatia upepo kubadili uelekeo mara kwa mara, moto huo ulianza kusambaa kwa kufuata uelekeo wa Kwa-Masheu na Mlima Kifinika.

Chanzo cha moto huo hakikuweza kujulikana, ingawa inasadikika kuwa ni shughuli za kibinadamu.

Juhudi za kuukabili moto huo zilifanywa na askari wa Jeshi la Uhifadhi, Jeshi la Akiba (Rombo na Longido), Jeshi la Polisi (mkoa wa Kilimanjaro) na Jeshi la Wananchi.

Moto huu uliweza kudhibitiwa tarehe Mosi Novemba 2022.

Madhara yaliyosababishwa na moto huo

Moto huu umesababisha madhara katika nyanja tofauti:-

Kujenga hofu kwa wageni

Kuteketeza kilomita za mraba 34.2 za uoto wa asili wenye mimea aina ya aina mbalimbali yakiwemo majani, Erica, Protea, Kniphonia thomsonii, Herichrysum, Bracken ferns (Aquillinum pteridium), Myrica salicifolia, Lobelia deckenii, mountain gladiolus na Senecio kilimanjarica.

Eneo hili ni sawa na Asilimia 1.9 ya eneo zima la Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro yenye Kilometa za Mraba 1,712. 

Uharibifu wa mandhari ya ukanda wa juu wa hifadhi 

Kuleta taharuki kwa jamii ya watanzania na dunia kwa ujumla kutokana na umuhimu na umaarufu wa Mlima Kilimanjaro

Kuteketeza viumbe wadogo ambao uwezo wao wa kutembea ni mdogo wakiwemo mamalia wadogo, wadudu, herpatofauna na kadhalika.

Baadhi ya viumbe walionekana kwenye eneo lililoungua ni pamoja na nyoka, digi digi, panya na mijusi

Changamoto zifuatazo zilijitokeza wakati wa kuzima moto;

Uzoefu mdogo wa uzimaji moto katika mazingira ya mlimani kwa baadhi ya wadau hususani ambao hawana uzoefu wa kupanda mlima na kufanya kazi kwenye maeneo yenye mwinuko mkubwa (high altitude)

Umbali mrefu wa maeneo yaliyoathirika, hivyo wazima moto kuchelewa kuyafikia

Kuwepo kwa kipindi cha ukame na upepo mkali kulichangia kwa kiasi kikubwa kusambaa kwa haraka kwa moto mlimani.

Kuwepo kwa makorongo makubwa ambayo ni vigumu kuyafikia kwa miguu hususani makorongo Karanga, Baranco, Umbwe, Lyamungo na Mweka

Kuwepo kwa mimea aina ya “Erica” inayoshika moto kwa haraka

Mlundikano wa mboji kwenye udongo iliyokuwa inahifadhi moto ardhini (underground fire)

Teknolojia hafifu ya uzimaji moto

Mafanikio ya kuzima moto katika uwanda wa juu wa Mlima Kilimanjaro yalitokana na ushirikiano mkubwa ambao Wizara ilipata kutoka kwa wadau mbalimbali.

Vyombo vya usalama katika Mkoa wa Kilimanjaro hususani Kamati za Usalama Mkoa na Wilaya, Jeshi la Zimamoto, Jeshi la Akiba, Jeshi la Uhifadhi (TFS, TAWA), Jeshi la Polisi.

Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lilileta askari 885 pamoja helikopta 2 na magari yaliyosaidia sana katika jitihada za uzimaji moto

Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO) kwa kushiriki uzimaji na kutoa mchango mkubwa wa chakula cha wazima moto pamoja na mafuta ya diesel

Makampuni ya Utalii yaliyotoa wapagazi na waongoza watalii kupanda mlimani kuzima moto.

Kundi hili lilikuwa na mchango mkubwa sana hasa kutokana na ustahimilivu na uzoefu wao wa kufanya kazi kwenye uwanda wa juu wa mlima Kilimanjaro.

Chuo cha polisi Moshi kwa kutoa usafiri na kuruhusu wanafunzi wao kushiriki moja kwa moja kwenye uzimaji moto

Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori – Mweka kwa kutoa usafiri na wanafunzi wao kushiriki kwenye uzimaji moto

Wananchi wa kutoka vijiji jirani waliojitokeza na kushiriki katika uzimaji moto

Waliochangia vyakula na mahitaji mbalimbali ya uzimaji ni pamoja na  TFS, TAWIRI, TATO, TPC, Pangani Basin Office, MUWASA, Africado na Sukos Kova Foundation, China Tanzania Partners- Peaceland foundation).

Wengine ni Mweka na Kilimanjaro plantation limited, Afro Liones, Jumuiya ya Makalasinga  – Moshi (Moshi Sigh Community), TPC, Tanzan, Mauly Tours, Key Tours, Kilimanjaro Plantation Limited, Save Wildlife and Wildlife Corrdiors, Kijani Pamoja, Bonde la Mto Pangani, Tanzania Local Tour Operator, Bonite Bolters Ltd, Kadco, Africado Siha,TFS Moshi, GF Trucks & Equipment Co.