Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Alphonce Simbu na Gabriel Geay Kushiriki Mbio za Mnara wa Saa jijini Arusha

Wanariadha wa kimataifa Alphonce Simbu na Gabriel Geay wanatarajia kushiriki mbio kubwa za ‘Clock Tower Marathon’ zinazotarajia kukimbiwa ndani ya jiji la Arusha August 6, mwaka huu.

Wanariadha hao wataungana na wakimbiaji wengine zaidi ya 1000 kutoka maeneo mbali mbali nchini watakaoshiriki mbio hizo umbali wa kilomita Ishirina na Moja, Kilometa Kumi na Kilometa Tano.

Mbio hizo ni katika madhumuni ya kuhamasisha utalii lakini pia utunzaji na usafi wa mazingira ikiwemo kampeni ya uoteshaji miti.

Mwenyekiti wa Klabu ya Arusha Runners ambao ndio waandaji, Issack Shayo alisema kuwa maandalizi ya mbio yamekamilika ikiwemo zawadi mbali mbali za washindi na washiriki.

“Mbio zetu za msimu wa tatu zitaanzia eneo la mnara wa clock tower ulioko ndani ya jiji la Arusha kuelekea barabara ya relini na kumalizikia kwenye viwanja vya Gymkana ambapo washiriki na washindi watapatiwa zawadi mbali mbali”

Alisema usajili wa mbio hizo umeanza katika mitandao ya Arusha runners na ofisi zao lakini pia katika viwanja vya sheikh amri abeid kwa gharama ya shilingi 35,000 ambapo washiriki wote watapatiwa fulana, namba ya kukimbilia, bangili maalum lakini pia watavishwa medali watakaomaliza.

Katibu wa shirikisho la riadha mkoa wa Arusha Rogath Steven alisema kuwa clock tower marathon zimekuwa na umuhimu kwa wanariadha wengi nchini kupata jukwaa la kushindana lakini pia kufanya mazoezi kwa ajili ya mbio kubwa wanazowakilisha taifa.

“Uanzishwaji wa mbio nyingi nchini ikiwemo Clock tower zimekuwa na msaada mkubwa kwa chama hasa kuwaibua wanariadha chipukizi lakini pia wale waandamizi kuzikimbia kimazoezi ili kuona mda wao bora kwa ajili ya mashindano mbali mbali ya kimataifa na kitaifa hivyo nitoe rai kwa wanamazoezi wote kuja kushiriki kwa ajili ya afya zao pia”

Alisema kuwa kutokana na umuhimu huo, wao kama chama wanayo kazi kubwa kutumia mbio hizo kupata wanariadha wapya hivyo watawashawishi wanariadha wao wengi kushiriki wakiwemo Simbu na Geay ambao lazima washiriki  na ndio wanaridha wa mfano kwa sasa wanaoangaliwa na chipukizi wengi nchini kufikia mafanikio ya malengo waliyonayo kupitia mchezo huo.

Akizundua rasmi mbio hizo, Mea wa jiji la Arusha Maximmilian Iranghe alisema kuwa halmashauri yake inajivunia mbio za clock tower kutokana na kuhamasisha utalii lakini zaidi kujinasua katika kuisaidia serikali kuboresha mazingira ikiwemo kufanya usafi na kupanda miti kupitia kampeni yao ya ‘Tanzania ya Kijani’

“Hakuna mji mchafu watalii watakuja, hivyo niwapongeze sana na katika kusaidia kufanikisha nitahamasisha wafanyakazi wote wa jiji waje kushiriki lakini pia marafiki zangu ili kuwasaidia afya zao na pia  kufikia malengo ya jiji la kuleta watalii wengi na kukuza utalii wa michezo”

Mbali na hilo Mea Iranghe aliwataka klabu ya Arusha runnes kuanzisha vitalu vya miche ya vivuli na matunda na kuotesha katika maeneo mbali mbali hasa taasisi za umma na maeneo yenye nafasi ili kufanikisha Azma ya kampeni yao vema lakini pia kupunguza hewa ya okaa.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari